Nkupamah media:
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.
Mbunge huyo ambaye jana mchana alikamatwa na polisi nyumbani kwake
baada ya kuizunguka kwa saa kadhaa, anashikiliwa kutokana na vurugu
zilizotokea Februari 27, mwaka huu kwenye ukumbi wa Karemjee baada ya
uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kuahirishwa kwa kile
kilichoelezwa ni kutokana na zuio la mahakama.
Mbali na Mdee, watu wengine watatu wakiwamo Diwani wa Kata ya
Saranga, Efraim Kinyafu na Diwani wa Kata ya Mbezi, Hamfrey Sambo wote
wa Chadema na kada wa chama hicho kata ya Mabibo, Shafii Juma,
wanashikiliwa na polisi kuhusiana na vurugu hizo.
Baada ya polisi kuzunguka nyumba yake, Mdee alikataa kuondoka kwa
magari ya polisi na badala yake akatumia gari lake kwenda Ofisa
Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Baada ya kufika kwenye kituoni hapo saa 7:20 mchana, mbunge huyo alihojiwa mpaka saa 12:54 polisi walipoamua kumlaza rumande.
Awali, askari polisi sita walifika nyumbani kwa Mdee, maeneo ya
Makongo, majira ya saa 2:00 asubuhi na kuomba kumchukua ili kuondoka
nae.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye pia ni mmoja wa familia ya Mdee,
alisema askari hao ambao waliokuwa wamevalia nguo za kiraia walimtuma
kijana waliyemkuta nje ya nyumba kuwa wanamuhitaji mbunge huyo kwa
mahojiani.
"Kijana yule kumbe hakumfikishia taarifa Mdee na askari walikaa nje
kwa takribani saa mbili hadi majira ya saa 4:00 asubuhi alipokwenda
kijana mwingine kumfuata na kutoka nje," alisema shuhuda huyo.
Alisema baada ya Mdee kutoka aliwahoji askari hao sababu ya
kujazana nyumbani kwake nao walieleza kuwa walitumwa na Jeshi la Polisi
kumkamata kwa mahojiano.
"Walikuwa hawana barua ya kumkamata ndipo Halima (Mdee)
alipowafukuza na kuwaambia kama hawana barua wakachukue ndio wanaweza
kwenda naye au wampigie simu yeye binafsi aende polisi badala ya
kumkamata," alisema shuhuda huyo.
Alisema baadae majira ya saa 5:45 asubuhi, askari hao wakiwa na
barua walimchukua Mdee na kuongozana naye hadi Kituo cha Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kuhusuiana na vurugu
zilizotokea siku ya uchaguzi wa Meya mwishomi mwa wiki iliyopita.
Wakili wa Mdee, Prof. Abdallah Safari, aliwaambia waandishi wa
habari kwamba, polisi wanamuhusisha Mdee na kumpiga aliyekuwa msimamizi
wa uchaguzi huo Theresia Mmbando, ingawa walisema hawana ushahidi wa
suala hilo.
Alisema anawashangaa polisi hao kumlaza Mdee ndani wakati ni Mbunge
anaruhusiwa kujidhamini mwenyewe na kwamba kosa linalomkabili haliwezi
kumfanya alale rumande.
Baadhi ya watu waliokuwa kituoni hapo walisema, Mdee pia anadaiwa
kuchukua nyaraka za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakati wa
vurugu za uchaguzi.
Chanzo kimoja cha habari kiliimbia Nipashe kuwa, wafuasi wengine wa
Chadema wanahojiwa kutokana na kuhusishwa na vurugu hizo pamoja na
kumshambulia Mmabando.
Kwa mujibu wa Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Said kubenea, madiwani
hao waliitwa kituoni hapo kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na vurugu za
uchaguzi wa Meya wa jiji.
Alisema akiwa kituoni hapo kwa shughuli nyingine za kufungua kesi,
alipata taarifa kuwa mwingine anayetafutwa ni Mbunge wa Jimbo la
Ukonga, Mwita Waitara, ambaye hadi jana jioni alikuwa hajafika kituoni
hapo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments :
Post a Comment