Nkupamah media:
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro.
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti jana katika kijiji cha
Churwi kata ya Mtambani Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, wananchi hao
walisema majambazi watatu waliuawa katika eneo hilo baada ya wananchi
kushiriki kikamilifu kusaidia polisi kuwakamata.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Mohamed Kimimbi, alisema mmoja wa
majambazi alitekeleza pikipiki yake na kutaka kuingia ndani ya nyumba
yake, lakini alimzuia, hali iliyomfanya jambazi huyo atoe kisu
kumtishia.
Hata hivyo, alisema kabla jambazi huyo hajamdhuru, wananchi walifika.
“Alikuwa anachuruzika damu, lakini nilipata ujasiri wa kumwambia
asimame asizidi kusogea, alitii ila alitoa kisu bahati nzuri wananchi
walifika na kumzingira hadi polisi walipofika,” alisema na kuongeza:
“Kinachotusikitisha ni Polisi kuwakamata ndugu zetu ambao
walishiriki kikamilifu kusaidia majambazi hao kukamatwa, mfano mimi
nilikuwa na uwezo wa kumuonyesha njia ya kukimbia na kujificha, lakini
sikufanya hivyo kwa kuwa tulishasikia milio ya risasi kuashiria hali ya
hatari.”
Shuhuda mwingine, Bakari Ally, alisema polisi walipofika kwa
Kimimbi na kuonyeshwa jambazi huyo, walimpiga risasi mguuni akaanguka
chini.
“Polisi mmoja alituambia asanteni kwa ushirikiano wenu. Huyu mtu
tunataka tuondoke naye akiwa hai, mwananchi mmoja alisema huyo jambazi
ana kisu na ndipo askari mmoja akatoa maelekezo ya kupigwa risasi kwa
jambazi huyo,” alisimulia na kuongeza:
“Askari mmoja alitoa maelekezo ya kumuua jambazi huyo na ndipo
walipomgeuza na kumlaza kifudifudi na kumpiga risasi na kufariki dunia
kisha walimbeba kwenye gari na kuondoka naye.”
Alisema majambazi wawili waliuawa na polisi eneo la Kwajoto na
kwamba hadi wanafika eneo hilo walikuwa wanachuruzika damu kwa kuwa
polisi waliokuwa wanatumia pikipiki waliwakimbiza huku wakiwafyatulia
risasi.
MSITU WAHUSISHWA NA UJAMBAZI
Diwani wa kata ya Tambani, Ally Hassan, alisema hakuwapo eneo la
tukio, lakini alipigiwa simu na wananchi wake kuelezwa kilichotokea.
Alisema mwananchi huyo alimueleza kuwa saa 5:00 asubuhi pikipiki
tatu zilipita eneo hilo kuelekea uelekeo wa Mbagala na ndizo
zilizotumiwa na majambazi hayo hadi wanakamatwa.
Hassan alisema msitu wa hifadhi ya maliasili Mlamleni Vikindu
unaopakana na eneo hilo, unatumika kama kichaka cha ujambazi kwani wengi
huenda kufanya matukio katika eneo hilo wakitokea msituni.
Alieleza kuwa katika tukio hilo, wakati majambazi hao wakikimbizwa na polisi, walielekea katika msitu huo.
“Mara kwa mara miili ya watu waliouawa katika eneo lingine, huletwa
kutupwa hapa, majambazi wanapofanya tukio mjini huja kujificha humo.
Hawa wa juzi nao walikuwa wanakimbilia humu, tumelalamika sana kwa
serikali ichukue hatua kwa msitu huu bila mafanikio,” alisema Hassan.
Diwani huyo alisema zaidi ya miaka 20 iliyopita, serikali ilimega
sehemu ya msitu huo na kuwapa wananchi wauendeleze, lakini baadaye
uamuzi huo ulibatilishwa na msitu huo kuendelea kuwa hifadhi, ambayo
sasa inaendelea kutumiwa na majambazi.
Mbali ya uhalifu katika msitu huo, pia alidai wananchi jirani wanaendelea kukabiliwa na matukio ya uhalifu majira ya usiku.
UKAMATAJI SIKU YA HARUSI
Mjumbe wa Serikali ya Kijiji katika eneo hilo, Abbas Mahegale,
anayeishi mita chache kutoka Msikiti wa Masjid Hassan, alisema siku moja
baada ya kuuawa kwa majambazi hao, polisi walivamia msikiti huo na
kuwakuta wananchi wakiwa kwenye shughuli za harusi ambapo walipekua na
kuwakamata ndugu 22 wa maharusi.
Akisimulia tukio hilo Februari 26, mwaka huu, Imamu Msaidizi wa
Msikiti huo, Sheikh Hamas Athuman, alisema wakati wa swala ya Ijumaa,
aliwatangazia waumini mwaliko wa harusi ya mpwa wake ambayo ingefanyika
nyumbani kwake.
“Nikiwa katika manunuzi ya bidhaa mbalimbali Mbagala, nilipigiwa
simu na mke wangu akidai kuwa polisi wamewavamia na wamewakamata.
Niliongea na polisi kwa simu. Nilirudi kwa haraka na kukuta watu
waliokuwa msikitini wamelazwa chini na wengine wameingizwa katika magari
ya polisi,” alidai Imamu huyo.
Alisema alijitambulisha kwa polisi kama mlinzi wa amani na
waliongea naye kwa muda mfupi kueleza kuwa wanachokifanya ni upepelezi
wa kina kwa kuwa zipo taarifa za uwapo wa baadhi ya waliohusika.
“Waliopondoka niliingia msikitini na kukuta viatu na kofia vimezagaa ovyo,” alisema.
MAMA WA BI. HARUSI ANENA
Siku ya Jumapili katika msikiti huo, kulikuwa na harusi ya
aliyowataja kuwa ni Omari Mpeta, kutoka Tabata na Aisha Said, wa
Charambe Magengeni, Mbagala.
Mama wa bibi harusi, Mapambano Juma, alismulia mkasa huo kwamba
mwanawe alipata mchumba na waliamua kufanya harusi kwa kaka yake, Sheikh
Hanas.
“Wanaume walikuwa msikitini, nasi tulikuwa nyumbani tukisubiri
waoaji. Ghafla tulisikia milio ya risasi na amri kutoka kwa polisi
kututaka wote tulale chini na kutoa kila tulichonacho. Walitupekua na
kututaka tutambae kutoka nje,” alisimulia mama huyo.
“Walituamuru kila mwenye simu aikabidhi. Nikiwa natoka nje kwa
kuburuzika kwa tumbo, huku nimembeba mwanangu wa miaka tisa, polisi
waliniamuru nisimame nikae pembeni. Walikamata baadhi ya watu na kuvunja
milango ya vyumba viwili vilivyokuwa vimefungwa na kufanya upekuzi
katika nyumba ya Hanas.
“Wakati wanafanya upekuzi, walikuwa wanasema mnafanya harusi huku
watu wameiba benki. Niliumia sana kwa kuwa sherehe ya mwanangu
niliyoiandaa kwa muda mrefu, imeharibika na hadi sasa hatuna amani,”
alisema.
WALIOKAMATWA SIYO MAJAMBAZI
Diwani huyo alilalamika kuwa waliokamatwa siyo majambazi, bali ni
ndugu wa bibi harusi ambao walikuwa msikitini wakiwasubiri waoaji na
wengine waliokuwa nyumbani kwa Imamu Hanas.
“Polisi walifanya upekuzi nyumbani kwa Ustadhi Daudi eneo la Mzinga
na kwa Hanas ambako waliondoka na baadhi ya CD, wakidai zinaonyesha
picha za Al Shaabab na kuanza kuwahusisha na ugaidi. Waliwahoji wananchi
kama ndani ya msikiti huo wamekuwa wakijifunza kareti,” alibainisha.
Diwani huyo alisema kuwa viongozi na wananchi hawana kipingamizi na
polisi kufanya kazi zao za kipelelezi hasa kama eneo hilo wamelitilia
shaka, wanachotakiwa ni kutenda haki kwa waliokamatwa kuwachuja na
kuwaacha wasiohusika.
“Hadi sasa watu watatu kati ya 22 wameachiwa kwa dhamana na wengine
wamesema dhamana yao inaruhusiwa, tunachofanya ni kukamilisha
masharti,” alieleza.
USHIRIKIANO WA MSIKITI NA JAMII
Diwani huyo alikiri kuwapo kwa ushirikiano wa miradi ya kijamii
kati ya Msikiti huo na jamii, kwani hivi karibuni walishiriki katika
ujenzi wa kivuko cha Mzinga na baadhi ya vikao vimekuwa vikifanyika
msikitini.
WAPONGEZA POLISI
Aidha, wananchi hao walipongeza polisi walioongoza msako huo kwa
jinsi walivyopambana na kuwakimbiza majambazi hao hadi kijijini humo na
kuhakikisha wanawajeruhi na baadaye kuwaua.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro,
alipotakiwa na Nipashe kutoa ufafanuzi wa baadhi ya madai yliyojitokeza
katika tukio hilo na watu wanaoshikiliwa alieleza: "Nitatoa ufafanuzi
wangu kesho (leo) kama nilivyoweka utaratibu wa kuongea na waandishi.”
Tukio la uporaji katika benki hiyo lilitokea Februari 26, mwaka huu
na watu 12 wanaosadikiwa kuwa majambazi waliohusika na kuua watu
watatu, akiwamo polisi, askari wa kampuni za ulinzi na mfanyakazi wa
benki.
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya majambazi wenye silaha
kuvamia duka la jumla umbali wa mita 100 kutoka ilipo benki hiyo na
kupora mamilioni ya fedha, kuua mtu mmoja na kujeruhi mwingine.
Mwaka jana, majambazi waliua polisi wawili waliokuwa katika kizuizi
cha Polisi eneo la Shule ya Sekondari St. Matthew wilayani Mkuranga na
kukimbilia katika msitu huo.
0 comments :
Post a Comment