Nkupamah media:
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bi. Emmy Hudson
Aidha, Rita imesema viongozi wa dini ambao watafungisha ndoa bila
leseni au wakiwa na leseni ambazo muda wake umekwisha watapelekwa kwenye
bodi ya muunganisho wa wadhamini; ambako hatua zaidi huchukuliwa dhidi
yao.
Katika hali inayoonyesha kuwa kuna ndoa nyingi batili zinazofungwa
hata kwenye nyumba za ibada, Rita ilitoa tangazo katikati ya wiki
ikitaka wale wote wanaofungisha ndoa kwenye madhehebu kuwa na leseni
zilizo hai.
Tangazo hilo lilitolewa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Rita, ambaye pia ni Msajili Mkuu wa Ndoa na Talaka.
Rita ilitaka viongozi wa madhehebu hayo ya dini wasajiliwe na kuwa na leseni iliyo hai ambayo hutolewa na RITA.
Akizungumza na Nipashe jijini jana, Msemaji wa RITA, Jafari Malema,
alisema viongozi wa dini ambao hawatatekeleza agizo hilo, mamlaka zao
zitachukuliwa hatua.
“Mfano kama ni dhehebu la Roman tunajua wapi tuandike barua na
kuipelekea na kwa Waislam nao tunawaandikia barua ili kuwakumbusha
kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni zilizopo ili mambo yasifanyike
kiholela,” alisema.
Alisema RITA haitawapeleka mahakamani viongozi wa dini watakaokiuka
sheria bali wataitwa kwenye bodi na kuongeza kuwa ndoa ambazo
zitafungishwa na viongozi hao wasio na leseni, hazitatambuliwa
kiserikali.
“Kiongozi wa dini akifungisha ndoa bila kuwa na leseni kwa imani ya
dini husika ndoa hiyo itakuwa halali, lakini kwa upande wa serikali
haitakuwa halali kwa sababu mtu aliyefungisha ndoa hajafuata taratibu na
sheria za nchi,” alisema.
Aidha, alisema kati ya viongozi hao wapo ambao leseni zao zimeisha na wengine hawajawahi kujisajili kabisa.
Tangazo hilo lilisema kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 2002
sura ya 29, ni lazima viongozi hao wawe wamesajiliwa na kuwa na leseni
iliyo hai inayotoka kwa wakala.
Rita iliwakumbusha viongozi hao kujisajili ili wapate leseni za
kufungisha ndoa na kwa wale ambao zimeisha muda wake wazihuishe ili
waweze kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria.
Pia Rita iliwakumbusha viongozi hao kuwa kufungisha ndoa bila ya
leseni ni kosa kisheria na kwamba RITA haitasita kuchukua hatua.
CHANZO:
NIPASHE


0 comments :
Post a Comment