Nkupamah media:
Na Lorietha Laurence-Maelezo
Serikali imedhamiria kumalizia deni la Makandarasi la kiasi cha zaidi ya bilioni 800 ifikapo Juni mwaka huu ambapo tayari kiasi cha bilioni 400 zimeshalipwa katika kufanikisha ujenzi wa barabara za ndani ya jiji la Dar es Salaam
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa barabara hizo leo jijini Dar es Salaam lengo ikiwa ni kupunguza msongamano katika njia kuu.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa inapunguza msongamano na hivyo kuwarahisishia wananchi wake usafiri , kukamilika kwa ujenzi huo ni afueni kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam” alisema Prof.Mbarawa.
Aliongeza kuwa ujenzi huo umegharimu kiasi cha shilingi Tilioni 1.2 chini ya ufadhili wa serikali yenyewe kwa asilimia 100 kupitia Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB) .
Prof.Mbarawa aliongeza kuwa kumekuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo ujenzi holela pamoja na ulipwaji wa fidia na kuwaomba wananachi pale wanapofanya ujenzi kujenge mbali na barabara ili kuepeukana na usumbufu wa mara kwa mara.
Naye Mkurugenzi Mkuu waWakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Patrick Mfugale ameeleza kuwa tayari baadhi ya wananchi wameshalipwa fidia kwa wale waliopisha ujenzi katika maeneo ambayo barabara zinatakiwa kupita na hivyo kurahisisha usafirishaji kwa wananchi wake.
“Natoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kupisha maeneo yale yote yaliyowekewa alama kwa ajili ya ujenzi ili kukamilisha ujenzi mapema iwezekanayo “ alisema Mfugale.
Ziara hiyo ya kukagua ujenzi wa barabara za ndani ilianzia katika barabara ya Tanki Bovu kwenda Goba kilomita 9.0,baadaye kuelekea ,Mbezi , Malambamawili,Kinyerezi hadi Banana yenye urefu wa kilomita 14 na Tabata Dampo-Kigogo na ile ya Ubungo Maziwa ,mabibo hadi External kilomita 2.25.
Maradi huo wa ujenzi wa barabara za ndani upo katika awamu mbili huku awamu ya kwanza ya kilomita 27 ikiwa inatarajia kukamilika mwezi Aprili mwaka huu na baadaye kumalizia awamu ya pili ya kilomita 28 tayari kwa kuanza ujezni wa awamu ya tatu barabara ya Goba-wazo hill kilomita 13.0,Mbezi Mwisho Malambamawili –kifuru kilomita 6, na Goba –Makongo-Ardhi kilomita 9.


0 comments :
Post a Comment