Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) limetoa tamko
kuhusiana na hali ilivyo sasa Zanzibar likisema linafadhaishwa na
kusikitishwa nayo na kwamba linaamini isingefikia hapo endapo Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingechukua hatua katika kutatua
mgogoro huo.
Katika tamko hilo lililosambazwa kwenye vyombo vya habari
jana baada ya kikao cha TCF juzi, yamo mapendekezo manne likiwamo la
kuitaka Serikali kurejesha mchakato wa Katiba kwa kuzingatia maudhui
yaliyomo katika Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kuondoa utata
wa Serikali kushiriki masuala ya Zanzibar.
“Sisi viongozi wa dini
tuliokutana leo tarehe 15.03.2016, tunafadhaishwa na kusikitishwa na
hali ya Zanzibar kwa sasa.
"Hali ya Zanzibar isingefika hapo ilipo iwapo
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingechukua hatua ya kutatua
mgogoro huu.
"Hali hii ya Zanzibar na udhaifu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano vinapelekea kushindwa kwa Serikali ya Muungano kuchukua hatua
ya kusaidia hali ya Zanzibar. Hata hivyo, udhaifu huu wa Katiba hauondoi
wajibu wa Serikali ya Muungano kuhakikisha haki na amani vinatawala
Zanzibar,” ilisema sehemu ta tamko hilo lililotiwa saini na Askofu Mkuu
wa Dayosisi ya Mwanza, Jude Ruwa’ichi.
Jukwaa halikufafanua hali ya
Zanzibar kwa sasa inay- osababisha maaskofu hao kufadhaika lakini huenda
limekusudia kueleza hofu iliyotanda katika visiwa hivyo tangu Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilipofuta uchaguzi na matokeo yote ya uchaguzi
wa Zanzibar, na baadaye kutangaza kuwa utarudiwa Machi 20.
Vyama tisa
kikiwamo Chama cha Wananchi (CUF) vilitangaza kujitoa lakini ZEC
imesisitiza vyama vyote vitashiriki.
Hali imeendelea kuwa tete na hivi
karibuni yamekuwapo matukio ya uchomaji moto makazi ya watu katika
visiwa hivyo yanayoonyesha uvunjifu wa amani kipindi hiki cha kuelekea
uchaguzi wa marudio Jumapili ijayo.
Baadhi ya matukio hayo ni kuchomwa
moto maskani za CCM na CUF, nyumba 11 za watu ikiwamo ya Kamishna wa
Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame iliyoko Kijichi, Mkoa wa Mjini
Magharibi.
Baada ya kutathimini hali hiyo, TCF imesema pamoja na udhaifu
wa Katiba, Serikali ya Muungano bado ina wajibu wa kuhakikisha uhuru,
haki na amani vinatawala Zanzibar kuelekea uchaguzi huo wa marudio.
“Hata hivyo, Serikali ya Muungano pamoja na taasisi zinazosimamia
mchakato wa uchaguzi, zinao wajibu wa kuhakikisha kuwa suala la uhuru,
haki na amani Zanzibar vinalindwa na kuheshimiwa. Suala la uhuru, haki
ni wajibu wetu sisi viongozi wa dini na Watanzania wote na halina
mbadala,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Jukwaa limesisitiza kwamba ni
jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake kulinda uhuru, haki na amani
na kuweka uzalendo kwanza kuliko kutanguliza maslahi binafsi au ya vyama
vya siasa.
Mbali ya pendekezo la kuitaka Serikali kurejesha mchakato wa
Katiba, pia limewataka viongozi wa dini kuwahimiza Watanzania wote
kuendelea kuiombea Tanzania (Bara na Zanzibar) ibaki kuwa Taifa
lililojengwa katika msingi ya uhuru, haki na amani.
Pili, limelitaka
Jeshi la Polisi, vikosi vya ulinzi na usalama na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania, kwa wakati huu kuendelea kutimiza wajibu wa kusimamia amani na
taratibu kwa haki bila upendeleo.
Mwisho limesisitiza kwamba viongozi
wa dini wabaki kuwa sauti ya kinabii na wahubiri wa uhuru, haki na amani
wakati huu, wakati wa uchaguzi na haada ya uchaguzi.



0 comments :
Post a Comment