……………………………………………………………………………..
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. MAKAME MBARAWA
amesema Serikali imejipanga kuhakikisha ujenzi wa daraja la mto
Kilombero unakamilika ifikapo mwezi Novemba mwaka huu ili kumaliza
changamoto ya usafiri inakabili wanachi wa wilaya za KILOMBERO na ULANGA
mkoani MOROGORO.
Prof. MBARAWA ametoa kauli hiyo Wilayani KILOMBERO mkoani
MOROGORO mara baada ya kukagua maendeleo ya kivuko cha MV- KILOMBERO
kilochokuwa kikikarabatiwa kufuatia kuzama mwishoni mwa mwezi Januari
ambapo amesema tayari Serikali imemlipa mkandarasi zaidi ya shilingi
bilioni kumi na moja ili kuhakikisha ujenzi wa daraja katika mto huo
linakamilika kwa wakati.
Amesema tayari mkandarasi anayejenga daraja hilo kutoka China
ameshalipwa shilingi bilioni 11.2 katika kipindi cha wiki mbili
zilizopita ambapo hivi sasa kazi inayoendelea kwa mkandarasi huyo ni
kutengeza vifaa maalumu kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo huko nchini
China .
“ Ifikapo novemba mwaka huu tutakuwa tumelipatia ufumbuzi wa
kudumu swala la daraja la Kilombero na hivyo mpapita kwa uhakika na
kufanya biashara zenu kwa uhakika”, amesema Prof.MBARAWA.
Aidha Prof. Mbarawa amekagua na kuruhusu kuanza tena kwa
shughuli za usafirishaji katika kivuko cha Mv Kilombero ambazo zilikuwa
zimesimama kwa takribani kipindi cha mwezi mmoja tangu kivuko hicho
kupata ajali mnamo Januari mwaka huu kufuatia mvua kubwa iliyoambatana
na upepo.
Ukabati wa kivuko hicho umegharimu
shilingi milioni 342.5 ambapo Prof.MBARAWA amewataka wananchi kufuata
maelekezo ya wasimamizi wa kivuko wakati wa safari zao na kulipa nauli
stahili.
“Lazima mlipe nauli kwa sababu nauli hiyo ndio tunayotumia
kuendeshea vivuko na pia mzingatie usalama wenu na kusikiliza maelekezo
ya wasimamizi wa kivuko ili kuepuka kadhia “amesisitiza Prof.MBARAWA.
Ujenzi wa daraja katika mto Kilombero ni sehemu ya mkakati wa
Serikali tangu awamu ya kwanza uliolenga kujenga madaraja makubwa ni
daraja la mto Rufiji mkoani Pwani, daraja Kirumi mkoani Mara, daraja la
Malagarasi mkoani Kigoma na Kigamboni la jijini Dar es salam.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO


0 comments :
Post a Comment