Nkupamah media:
WASANII
wa muziki mbalimbali hapa nchini, Jumamosi hii wanatarajiwa kukinukisha
vilivyo katika Viwanja vya Mwembe Yanga Temeke jijini Dar es Salaam,
katika tamasha la Amsha Mama Festival.
Akizungumza kwa niaba ya wasanii
wenzake, Balozi wa tamasha hilo Khalid Ramadhani ‘Tundaman’, ambaye
amepewa Ubalozi huo kupitia waandaaji wa tamasha la (AFWAB) AMSHA MAMA
Festival 2016, lililo chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa lebo ya Candy na
Candy Records Joe Kariuki, alisema tamasha hilo linalotarajiwa
kufanyika Machi 5 mwaka huu katika uwanja wa Mwembe Yanga jijini Dar es
Salaam.
Tundaman na Muandaaji wa tamasha
hilo Kariuki, wamesema kwamba maandalizi ya shoo hiyo tayari
yameshakamilika kwa kiasi kikubwa hivyo angependa kutumia fursa hii
kuwaalika wakazi wote wa jiji la Dar, kujumuika siku hiyo kushuhudia
burudani mbalimbali zitakazotolewa na wasanii kibao ambao tayari
wemedhibitisha kufanya makamuzi siku hiyo.
“Tunapenda kuwaalika Watanzania
wote kwa ujumla siku ya jumamosi hii ya Machi 5, mwaka huu waje kwa
wingi katika Viwanja vya Mwembe Yanga Temeke jijini Dar Salaam, ili
tujumuike kwa pamoja katika tamasha la kuhamasisha wanawake kujikwamua
katika shughuli zao mbalimbali za kiuchumi.
Tamasha hili litakuwa ni la wazi
kwa maana kwamba watu wote watapata burudani kibao bila malipo yaani
bure kabisa hivyo waje kuwashuhudia wasanii kama, Khadija Kopa, Mr Blue,
Snura, Msaga Sumu, Ali Chocky na Tunda Man wakitoa burudani ya hali ya
juu kwani ulinzi na usalama siku hiyo ni wa uhakika,” alisema Tunda
Man.
Kwa upande wake, Joe Kariuki
ambaye ni mratibu mkuu wa tamasha hilo ametumia muda huu kuongea na
baadhi ya akinamama wanaojishughulisha na biashara za vitu mbalimbali
hususani mama ntilie, wauza matunda na wauzaji wa mitumba ili nao
wajitokeze kwa wingi kuja kunadi bidhaa zao siku hiyo kwani hiyo ndiyo
fursa yao ya kipekee ya kujitangaza bure.
0 comments :
Post a Comment