Wazazi
na walezi wa wanafunzi 122 wa darasa la awali katika shule ya msingi
Kinampundu, tarafa ya Nduguti, wilayani Mkalama wameulalamikia uongozi
wa shule ya msingi Kinampundu kwa tuhuma za kuwachangisha kila mmoja
shilingi 5,000/= kwa ajili ya kuandikisha wanafunzi wanaoanza masomo ya
darasa la awali katika shule hiyo.
Kuchangishwa
kwa kiasi hicho cha fedha kwa wazazi na walezi wa shule hiyo ni
ukiukwaji wa agizo la Rais Dk.John Pombe Magufuli alilotangaza juu ya
elimu bila malipo kwa wanafunzi wa kuanzia darasa la awali mpaka
sekondari.
Kauli
hiyo imetolewa na wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule hiyo katika
mkutano wa hadhara ulioandaliwa na mbunge wa jimbo la Iramba
Mashariki(CCM), Allani Joseph Kiula aliyekuwa katika ziara yake ya
kuwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kumchagua ikiwa ni pamoja na
kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa
nguvu za wananchi katika jimbo hilo.
Mmoja
wa wazazi, Pendaeli John alifafanua kwamba licha ya kiongozi mkuu wa
nchi kuagiza kwamba wanafunzi wa kuanzia darasa la awali hadi sekondari
watanufaika na elimu bila malipo lakini cha kushangaza agizo hilo
limeendelea kupuuzwa na baadhi ya walimu wa shule hiyo huku watendaji
wenye mamlaka ya kutoa maamuzi katika kata hiyo wakiwa kimya.
Aidha
kwa upande wake mzazi mwingine, Cosmas Amasi aliweka wazi kwa kuzitaja
sababu zinazochangia wao wadaiwe shilingi 5,000 kwa mwaka, kutokana na
maelezo ya walimu wa shule hiyo sababu ya kuweka malipo ni idadi ndogo
ya walimu waliopo shuleni hapo,jambo ambalo lipo ndani ya uwezo wa
serikali.
“Tunaambiwa
kwamba ni lazima kila mzazi au mlezi achangie shilingi elfu tano kwa
mwaka kutokana na idadi ya walimu waliopo katika shule hii ni wachache
hivyo ni jukumu la wazazi kuchangia ili mwalimu anayefundisha watoto hao
aweze kulipwa posho yake ya mwezi”alifafanua Amasi.
Naye
Lazaro Kingu akizungumzia ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule ya
sekondari ya kata hiyo alisisitiza kwamba wananchi wa kata hiyo
walichangishwa pia shilingi 65,000/= kila mmoja kwa ajili ya ujenzi wa
vyumba vya maabara lakini tangu kuanza kwa ujenzi huo mpaka sasa jengo
hilo bado halijakamilika kujengwa licha ya fedha nyingi kukusanywa na
uongozi wa kata hiyo.
Hata
hivyo walipotaka kuzungumzia malalamiko ya wananchi hao, Afisa Mtendaji
wa kata hiyo, Richard Laizer pamoja na mwalimu mkuu wa shule hiyo,
Hamisi Mbutu walikiri wananchi kuchangia kiasi hicho cha fedha lakini
kwa upande wao hawakuhusika katika zoezi zima la ukusanyaji wa michango
hiyo.
Kwa
upande wake Mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki, Allani Joseph Kiula
alisema kwamba wazazi pamoja na walezi wa shule hawana budi kutambua
kwamba shule ni mali yao kwani ni kwa kiasi kikubwa sana wao wameshiriki
katika ujenzi wa shule hiyo.
Alibainisha
pia kwamba kutokana na ukweli huo wa ushiriki wao katika ujenzi wa
shule hivyo kunapohitajika mchango wowote ule uongozi wa shule na kata
kwa ujumla hawana budi kukubaliana katika vikao vya maamuzi ya pamoja na
kisha kwenda kuomba kibali cha kuchangisha,ambacho mwenye mamlaka ya
kutoa kibali hicho ni mkuu wa mkoa peke yake.
“Kwa
kuwa shule ni mali ya wananchi,kwani hakuna anayebisha kuwa wao ni
washiriki wakuu katika ujenzi wa shule hii,hivyo kunapotokea mchango
wowote wa shule mnawajibika kukutana katika vikao halali na kisha
kupeleka maaombi kwa mkuu wa wilaya na hatimaye kwa mkuu wa mkoa ambaye
ndiye mwenye mamlaka pekee ya kuruhusu michango yeyote ile,” alisisitiza
Mbunge huyo.
Na Jumbe Ismailly, Mkalama
Afisa elimu wilayani Mkalama (aliyesimama huku akiwa na karatasi mkononi) akifafanua jambo kuhusu suala la elimu bila malipo.
Mbunge
wa jimbo la Iramba mashariki(CCM), Bwana Allani Kiula(wa pili kutoka
kushoto) akiwa na diwani wa kata ya Ilunda, Bwana Mohamedi Imbele(wa
pili kutoka kushoto) wakiwa katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha
Kinampundu.
Mbunge
wa jimbo la Iramba mashariki(CCM)Bwana Allani Kiula(wa kwanza kutokaa
kulia) akimtambulisha afisa mtendaji wa kata ya Kinampundu kwa wananchi
waliohudhuria mkutano huo.
Baadhi ya wanawae waliohudhuria mkutano wa mbunge na kutoa kero zao zinazowasumbua.
0 comments :
Post a Comment