Shilingi
trilioni 107 zinahitajika kugharamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa
Maendeleo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka
2016/21, ambao utategemea sana makusanyo ya kodi na ukijikita katika
kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda.
Akiwasilisha
bungeni jana Mpango huo wa Pili wa Maendeleo, Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk Phillip Mpango alisema katika fedha hizo, Sh trilioni 59
zitatolewa na serikali, huku kiasi kilichobaki cha Sh trilioni 48
zitachangiwa na sekta binafsi pamoja na mikopo na misaada kutoka nje.
Akitoa
mchanganuo wa ugharamiaji mpango huo, Dk Mpango alisema kila mwaka
serikali itatoa Sh trilioni 11.8 na kwamba katika kipindi cha miaka
mitano ya mpango huo, serikali itakuwa imetoa jumla ya Sh trilioni 59.
Alisema
eneo la pili la gharama za mpango huo, litabebwa na sekta binafsi,
mkopo na misaada kutoka nje na kuwa serikali inaweka mazingira mazuri
kwa sekta binafsi kuwekeza katika miradi ya maendeleo.
Alisema
katika mpango huo, kuna ongezeko kubwa la fedha za kugharamia mpango
huo, ukilinganisha na ule wa kwanza na sababu ya ongezeko hilo ni ukubwa
wa miradi tarajiwa sambamba na nia ya kuchochea upatikanaji wa
mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji.
Alisema
nchi ikiwekeza kwenye ujenzi wa viwanda, huvutia misaada kutoka nje na
hiyo imetokana na uzoefu wa nchi nyingine zilizoweka mikakati kwenye
uwekezaji wa viwanda.
“Mantiki
yetu ni kwamba nchi haina budi kuwa na mkakati mahususi wa kukusanya
fedha kuwezesha utekelezaji wa mpango huu kwa ufanisi,” alisema Dk Mpango.
Kwa
upande wa serikali, Dk Mpango alisema fedha za kugharamia mpango huo,
watazipata kwenye makusanyo ya kodi na yale yasiyo ya kodi, ambapo
serikali imeainisha miradi mikubwa ya kielelezo kama ile ya makaa ya
mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga.
Aidha, eneo jingine ni ujenzi wa Reli ya Kati na kuboresha miundombinu mingine, zikiwemo barabara na usafiri wa anga.
Hata
hivyo, Dk Mpango alisema katika eneo la kufungamanisha maendeleo ya
uchumi na maendeleo ya watu, bado kiwango cha umaskini nchini ni
kikubwa.
Alisema
hivi sasa nchini kuna watu maskini zaidi ya milioni 10, idadi ambayo ni
kubwa kuliko baadhi ya nchi Afrika na kusema Mpango wa Taifa wa
Maendeleo wa Mwaka 2016/17 hadi 2021, umelenga kupunguza kiwango hicho.
Dk
Mpango alisema hatua hiyo inatokana na ule mpango wa kwanza 2011/16
kufikia ukomo wake ifikapo Juni mwaka huu huku kukiwa bado na changamoto
nyingi.
Alisema
pamoja na mpango unaoisha muda wake kutekelezwa kwa kiasi, lakini bado
zipo changamoto kubwa zinazopaswa kupewa kipaumbele katika mpango huo
mpya ili kuhakikisha jitihada zinawekwa katika kuleta maendeleo ili
kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
“Tanzania
ina watu maskini zaidi ya milioni 10, idadi hii ni kubwa kuliko baadhi
ya nchi barani Afrika na idadi hii haishiriki kikamilifu katika
uzalishaji, kaya nyingi zimebeba mzigo mkubwa wa wategemezi kufuatia
kasi kubwa ya kuzaliana na athari za magonjwa yakiwemo Ukimwi,” alieleza Dk Mpango.
Aidha,
aliongeza changamoto nyingine inayoongeza kasi ya umaskini wa watu ni
ukosefu wa ajira na kwamba kati ya vijana 800,000 wanaoingia kwenye soko
la ajira kila mwaka baada ya kumaliza masomo, ni 200,000 ndio
wanaobahatika kupata ajira katika sekta rasmi.
Hivyo
mpango huo wa maendeleo kwa mwaka 2016/17 umelenga kuongeza kasi ya
ukuaji uchumi kwa kuhakikisha unaongezeka kutoka asilimia 7.0 ya mwaka
2015 hadi kufika asilimia 10 ifikapo mwaka 2020.
Aidha,
mpango huo umelenga kuongeza pato la wastani kwa kila mwananchi kutoka
Dola 1,006 kwa mwaka 2015 hadi kufikia Dola 1,500 ifikapo mwaka 2020 na
pia kuhakikisha mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani yanaongezeka kutoka
asilimia 24 mwaka juzi hadi kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2020.
Mpango
wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka 2016/17, umeweka vipaumbele vikuu vinne
vilivyolenga ukuzaji viwanda kwa lengo la kuifanya nchi itimize malengo
ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Vipaumbele hivyo ni;
- Kuwa na viwanda vya kukuza uchumi
- Kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu,
- Kuweka mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na
- Kipaumbele cha nne ni kusimamia utekelezaji wa mpango huo.
Katika
vipaumbele hivyo, sekta zote zitaangaliwa na kuwekewa mikakati ya
kuziboresha ikiwemo viwanda, kilimo, afya, elimu, miundombinu,
rasilimali watu kwa kuhakikisha nchi inafikia malengo yake ya kuwa nchi
ya uchumi wa kati.
Katika
utekelezaji huo, viwanda vilivyokufa na vile visivyoendeshwa kwa tija
vitafufuliwa na vingine kuanzishwa ili visaidie kuongeza uzalishaji wa
mazao yenye thamani na kukuza kipato cha watanzania na taifa kwa ujumla.
Aidha,
Dk Mpango amewaasa Watanzania kuacha na kuukana utamaduni wa kuishi
maisha ya kipato wasichoweza kukimudu na badala yake wafanye mageuzi ya
mfumo wa maisha kwa kujizatiti kuzalisha mali huku serikali ikiweka
nguvu kwenye ukusanyaji mapato ya kodi na yale yasiyo ya kodi.
Akihitimisha hotuba yake hiyo bungeni, alisema hakuna budi kwa Watanzania kubadilika na kubadilisha mfumo wa maisha.
“Desemba
9, mwaka huu tutaadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa nchi yetu, maana yake
ni kuwa kiumri nchi yetu si changa tena, ina umri wa mtu mzima
anayepaswa kuwa na familia na uwezo wa kujitegemea kimaisha, hatupaswi
kuwa wategemezi, sharti tujijenge,” alisema Dk Mpango.
Alisema
katika hilo hakuna njia ya mkato na kwamba nchi inapaswa kujizatiti
kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kutoka vyanzo vyetu vya ndani
kwa nguvu zote na kuacha matumizi ya starehe.
Dk
Mpango alisema matumizi ya starehe katika maisha ya sasa na ya uchumi
wa nchi hayapaswi kuendekezwa na Watanzania, ikiwa wanataka kuondokana
na umaskini na utegemezi wa kibajeti.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuondokana na umaskini na
kuwasaidia wananchi kuzalisha mali hivyo vita vya mageuzi ya mfumo wa
maisha ni lazima ufanywe kuanzia ngazi ya familia ili kuishi maisha ya
kipato wanachoweza kukimudu na sio kuisha maisha ya ufisadi.
“Ndio
sababu Rais Dk John Magufuli amekuja na kauli ya kutumbua majipu
inayoendelea na dhana nzuri ya kukubali tiba kwa kuwa wapo wengi
miongoni mwetu watajitahidi kukataa kupokea maumivu haya, japo hii ndiyo
njia pekee ya kupona,” alisema Dk Mpango.
Akizungumzia
ukuaji wa uchumi kwa kuwekeza kwenye viwanda, alisema hiyo ndiyo njia
ya uhakika kufikia maendeleo endelevu inayotumiwa na nchi nyingi duniani
na Tanzania imeamua kujipanga upya kiuchumi kufikia huko.
“Ni
dhahiri katika njia hii kutakuwa na vikwazo pamoja na ushindani katika
masoko ya mitaji ya bidhaa, ila ili tuvuke tunahitaji dhamira ya dhati
kuibadilisha nchi yetu kuwa sehemu bora zaidi ya kuishi kwa wananchi
wote,” alisema Dk Mpango.



0 comments :
Post a Comment