Deni la Taifa limeongezeka kwa Sh7.05 trilioni, kutoka Sh26.49 trilioni Juni 30, 2014, hadi Sh33.54 trilioni sawa na ongezeko la asilimia 27.
Kwa
 mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali 
(CAG), Profesa Musa Assad, deni la ndani ni Sh7.99 trilioni huku deni la
 nje likiwa ni Sh25.55 trilioni.
Akiwasilisha ripoti hiyo jana bungeni, alisema kiwango hicho cha ongezeko la deni ni kikubwa katika kipindi cha muda mfupi. 
“Uchambuzi
 wangu umeonyesha kuwa malipo ya kugharimia madeni ya Sh4.6 trilioni 
mwaka huu ni sawa na asilimia 46 ya makusanyo ya ndani ya Serikali 
ambayo ni Sh10.8 trilioni,” alisema. 
Alisema gharama hizo 
zikijumuishwa na gharama nyingine kama mishahara ya wafanyakazi na 
malipo ya likizo, Serikali hubaki na kiasi kidogo cha fedha za 
kugharimia miradi ya maendeleo na huduma nyingine za kijamii. 
Profesa Assad alipendekeza mambo matatu kama sehemu 
ya mikakati ya kukabiliana na ongezeko la deni hilo, ikiwamo Serikali 
kuongeza jitihada za ndani za kuhamasisha ukusanyaji mapato ili kujenga 
wigo mpana wa kulipa madeni. 
Pia, alishauri kuwapo kwa mpango mkakati kuhusu fedha, hasa upunguzaji wa gharama na mikopo yenye masharti. 
Jambo
 la tatu, alishauri Serikali kuwa na uratibu mzuri wa shughuli 
zinazohusisha miamala ya fedha za kigeni, akisema hatua hiyo inawezekana
 kama kutakuwapo usimamizi thabiti. 



0 comments :
Post a Comment