Taarifa ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) iliyowasilishwa jana kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imekataliwa baada ya kubainika upungufu, ukiwamo udhaifu wa Sera ya Uwekezaji na kiasi cha fedha kilichowekezwa katika miradi iliyopita.
Uamuzi
huo umekuja wiki moja baada ya kamati hiyo kuagiza kusimamishwa miradi
yote mipya inayotarajiwa kutekelezwa na NSSF hadi Serikali itakapopitia
ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na
kujiridhisha na utendaji wa mfuko huo.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Mohamed Mchengulwa alitoa agizo hilo baada ya kufanya
ziara katika ofisi ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya
Hifadhi ya Jamii (SSRA) ambapo baada ya kupokea ripoti ya SSRA, alisema:
“Kamati inaagiza kwamba SSRA isimamie miradi yote mipya inayotarajiwa
kutekelezwa hivi sasa isimame haraka, ili iweze kujiridhisha na hesabu
ambazo zimefanyika.”
Akizungumza
baada ya kikao kati ya kamati hiyo na NSSF jana, Mchengulwa alisema
mbali ya mfuko huo kutoonyesha gharama za uwekezaji katika miradi
iliyopita, pia alisisitiza taarifa ya mfuko huo haijaonyesha miradi
ambayo imeidhinishwa mwaka huu wala miradi ambayo iko kwenye hatua za
mwisho za umaliziaji.
Mchengulwa
alisema baada ya kubaini upungufu huo wanasubiri kwanza ripoti ya CAG
iwasilishwe bungeni, Dodoma, Aprili 25, mwaka huu ili iweze kuijadili
kwa kina.
“Baada
ya kubaini mapungufu haya, tumeamua kusubiri kwanza Serikali iwasilishe
bungeni ripoti ya CAG ili nasi tuanzie hapo.Kwa sasa hatuwezi kupata
taarifa ya CAG kwa sababu bado iko kwa Rais,” alisema Mchengulwa.
Mchengulwa,
ambaye pia ni mbunge wa Rufiji alisema, “Sisi hatufanyi kazi kwa
kusikiliza vyombo vya habari ila tunataka kujiridhisha baada ya kusoma
ripoti ya CAG. Baadhi ya wanachama wanajitoa NSSF kwa sababu ya kashfa
za ufisadi tunazoziona kwenye mitandao na magazeti.”
Kilichowashtua
wabunge hao ni ripoti za vyombo vya habari kuhusu harufu ya ufisadi
katika miradi mbalimbali ya mfuko huo; ardhi kuthaminishwa kwa kati ya
Sh800 milioni na Sh1.8 bilioni kwa ekari moja; kampuni mbili kulipwa kwa
kandarasi moja, mkandarasi kuzidishiwa malipo, na ukiukwaji katika
utolewaji wa zabuni.
Miradi
iliyoanzishwa na NSSF ambayo vyombo vya habari vimeonyesha kwamba ina
harufu ya ufisadi ni wa ujenzi wa mji mpya wa Dege Eco Village,
Kigamboni ambao thamani ya ekari moja ni Sh800 milioni; Arumeru ardhi
imethaminishwa kwa Sh1.8 bilioni, mkandarasi wa ujenzi wa jengo la
Mzizima ameongezewa Sh5 milioni.
Vyombo
vya habari vilinukuu ripoti ya ukaguzi wa miradi uliofanywa na CAG
pamoja na kampuni ya kimataifa ya Ernst & Young ambayo CAG
amewasilisha kwa Rais John Magufuli, ingawa inadaiwa baadhi ya mambo
yameondolewa baada ya majibu kupatikana kutoka NSSF.
Mchengulwa
alisema baada ya ripoti ya CAG kuwasilishwa bungeni, kamati yake
itamwita CAG kueleza ukaguzi wake na itawahoji pia SSRA kwa kushindwa
kusimamia mfuko huo.
“Ni
wazi kwamba wanachama wengi wa NSSF wameanza kujitoa kwa sababu ya
taarifa mbalimbali wanazoziona kwenye mitandao. Sasa hali hiyo
ikiendelea mifuko mingi itakufa na wananchi watakosa imani na mifuko
hiyo,” alisema.
Aidha,
Mchengerwa alisema kamati yake imeitaka serikali na SSRA kuangalia
namna wanavyoweza kupunguza mifuko ya hifadhi kwani mingi, inafanya kazi
moja na baadhi ya mifu- ko ina hali mbaya kifedha kiasi cha kushindwa
kulipa wanachama.
Ofisi ya Makamu wa Rais
Wakati
huohuo, kamati hiyo imebaini ukiukwaji wa sheria katika ujenzi wa
jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais ambalo tayari lina nyufa kuanzia chini
mpaka juu na milango mibovu, jambo linaloashiria kwamba jengo hilo lina
matatizo makubwa.
“Kuna
baadhi ya kasoro katika kumbi za mikutano iliyopo katika jengo la
makamu wa rais, kwa mfano, kumbi za mikutano zina milango midogo ya
kutoka mtu mmoja, kama kuna dharura watu wanaweza kupata matatizo,”
alisema Mchengulwa baada ya kutembelea jengo hilo.
“Nimeshaagiza
Katibu wa Bunge aandike barua kumpa maelekezo CAG kuhusu ukaguzi wa
jengo hilo. Wakala wa Majengo (TBA) wamejitetea hapa lakini tunataka
kupata taarifa kamili ya value for money kutoka kwa CAG,” alisema.
Mwenyekiti
huyo alisema sheria inaruhusu mkandarasi kulipwa asilimia 90 ya gharama
zote na baada ya kukabidhi jengo analipwa asilimia 10 ya fedha
zilizobaki, lakini alilipwa asilimia 98 ya fedha zote ambazo ni Sh8
bilioni na kubaki na asilimia mbili ambayo ni Sh200 milioni.
0 comments :
Post a Comment