WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema vitendo vya
dhuluma, ufisadi na jeuri vinavyofanywa na watoaji na wapokeaji rushwa
vinasababisha wananchi kukosa haki zao na maisha yao kuwa duni, hivyo
amewataka wajumbe na Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania
(ALAT) kupiga vita rushwa katika ngazi zote za utawala kwenye mamlaka
zao na kwa nchi.
“Sote tunakumbuka msemo wa rushwa
ni adui wa haki na kwamba sitapokea wala kutoa rushwa,” amewasisitiza
juu ya umuhimu wa msemo kwa sababu kuna dalili kwamba rushwa ni kikwazo
kikubwa katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo katika ngazi
mbalimbali zikiwemo za halmashauri, serikali kuu na taasisi mbalimbali
za umma.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
mchana wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa ALAT
uliofanyika mjini Dodoma ambapo amesema vitendo vya rushwa
vinalalamikiwa sana na wananchi, katika maeneo yote, hususan katika
huduma za afya, elimu, ardhi na utoaji leseni mbalimbali katika Serikali
za Mitaa.
“Kutokana na ukweli huo, wapo
wananchi ambao wameanza kupoteza imani kwa serikali yao kutokana na
kuendeleza vitendo vya rushwa miongoni mwa jamii. Natoa wito kwenu
mkiwa wajumbe wa chombo hiki muhimu kupiga vita vitendo vyote
vinavyoashiria rushwa katika ngazi zote za utawala kwenye mamlaka zenu
na kwa nchi yetu,” amesema.
Amesema hata wakati Mheshimiwa
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli
anazindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba,
2015 alibainisha maeneo mbalimbali ambayo ni kero kwa Wananchi mojawapo
ni tatizo la rushwa miongoni mwa jamii.
Waziri Mkuu, Majaliwa amesema kuwa
wakati wa kampeni za uchaguzi rais alipata fursa ya kusikiliza
malalamiko mengi ya wananchi ikiwa ni pamoja na kushindwa kwa serikali
za mitaa kutekeleza majukumu yake na kuwajibika kwao kama katiba, sheria
na sera zinavyoelekeza.
Amesema changamoto nyingine
aliyoizungumzia Mheshimiwa Rais ni upotevu wa mapato na kushindwa
kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na madaraka,
ambapo utekelezaji wa baadhi ya miradi upo chini ya viwango huku
kukiwepo na wizi, uzembe katika mamlaka za serikali za mitaa. hivyo
kusababisha upotevu mkubwa wa fedha.
Waziri Mkuu, Majaliwa amesema kuna
uvujaji mkubwa wa mapato yanayokusanywa na mamlaka za serikali za mitaa
kupitia mawakala au hata baadhi ya watumishi wachache wasio waaminifu,
ambapo alitumia fursa hiyo kuwasisitiza usimamizi mzuri wa mapato ya
halmashauri na kuhakikisha yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ambapo
imebainika kuwa ni salama na itasaidia kupunguza kupovu huo.
“Ninatambua kwamba bado zipo
changamoto za utaratibu huu wa kukusanya mapato kwa njia ya
elektroniki. Aidha, zipo taarifa kuwa, baadhi ya watumishi wa
halmashauri ndiyo wenye kampuni za uwakala wa kukusanya kodi na tozo
mbalimbali za halmashauri, hivyo nawakumbusha watendaji wote kwamba
taarifa hizi zikibainika ni za kweli, hatua za kinidhamu zitachukuliwa.
Ni vyema wahusika waache tabia hiyo mara moja kwani ni kinyume na
maadili ya utumishi wa umma,” amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu,
Majaliwa ameyataka mabaraza ya Madiwani yafanye kazi zake kwa mujibu wa
sheria, ambapo amekemea tabia ya baadhi ya watendaji wa halmashauri
kutokutaka kuulizwa chochote na mabaraza hayo kwa kisingizio kwamba wao
ni watalaamu.
Amesema Mabaraza ya Madiwani ndiyo
mamlaka ya wananchi katika kusimamia halmashauri hivyo kuwazuia
Madiwani kuhoji chochote hata pale ambapo wataalam wamekwenda kinyume na
maadili ya taaluma na utumishi wa umma siyo sahihi kiutendaji, hivyo
amewataka watendaji hao kuyaachia Mabaraza hayo yafanye kazi zake na
kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wakea Naibu Waziri wa
Nchi, Osisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo
amesema watahakikisha wanatoa maelekezo wanazisimamia vizuri halmashauri
katika ukusanyaji wa kodi kwa mfumo wa kielektroniki.
Pia Jafo amempongeza Waziri Mkuu
Majaliwa kwa utendaji wake na kwamba amewathibitishia Watanzania kuwa
Rais Dk. John Magufuli hakukosea katika uteuzi huo na kwammba umakini
wake katika kuchapakazi umeleta tija nchini.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti
wa ALAT Taifa, Steven Muhapa akitoa hutuba ya shukurani kwa Waziri
Mkuu, amesema maelekezo na maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu
wameyapokea na wataenda kuyafanyia kazi.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu


0 comments :
Post a Comment