Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwataka wahitimu wa
mafunzo ya uongozi mdogo kutumia mafunzo waliyoyapata ili kuleta
mageuzi makubwa ya utendaji katika sehemu zao za kazi.
Balozi
Seif ameeleza hayo leo katika sherehe za ufungaji wa mafunzo ya Jeshi
la Polisi ngazi ya koplo, sajenti na staff sajenti yaliyofanyika katika
viwanja nya Polisi Ziwani mjini Zanzibar.
Amesema
kuyatumia mafunzo hayo vizuri katika utendaji wa kazi itapelekea
kupunguza uhalifu na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
“Nategemea
mtabadilika na kuwa watendaji wazuri wanaochukia rushwa, kesi
zitaendeshwa kwa haraka , haki itatendeka katika kutekeleza majukumu na
haki za binaadam zitazingatiwa kwa lengo la kujenga heshima ya Serikali
na kuleta uhusiano wa karibu baina yenu na Wananchi “Alisema Balozi.
Aidha
alilitaka Jeshi la polisi kutopuuza uhalifu mdogo mdogo kwani uhalifu
huo hatimae hupelekea uhalifu mkubwa na kusababisha uvunjifu wa amani
katika nchi.
Nae
Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdani Omar Makame amewakumbusha wahitimu
hao kuwa wanawajibu mkubwa wa kuwalinda raia na mali zao pamoja na
kulinda sheria za nchi.
Hata
hivyo amewataka kufanya kazi kwa kutumia elimu waliyoipata chuoni kwa
vitendo, kuwaelimisha na kuwaongoza kwa uweledi askari huko vituoni
mwao.
Kwa
upande wake Mwalimu mkuu wa chuo cha Polisi Zanzibar Deusdedit
Kaizilege Nsimeki amesema Jeshi la polisi litaendelea kuwaelimisha na
kuwahamasisha wananchi ili kuwajengea uwezo na uwelewa wa umuhimu wa
utii wa sheria bila ya kushurutishwa.
Mafunzo
ya uongozi mdogo wa vyeo vya Koplo, Sajenti na Staff sajenti
yalifunguliwa rasmi tarehe 16/02/2016. Yakiwa na jumla ya wanafunzi 1532
kati ya hao kozi ya koplo 591, kozi ya Sajenti 706 na kozi ya Staff
sajenti 235.
Na Khadija Khamis /Maryam Kidiko –Maelezo Zanzibar
Maafisa na wahitimu wa uongozi mdogo wa Jeshi la Polisi wakitoa saluti
kwa mgeni rasmini Makamu wa pili wa Raisi Balozi Seif Ali.
0 comments :
Post a Comment