Baada ya jana Jumatano Afisa Habari wa Yanga, Jerry Muro kuwaomba wapinzani wao Simba kuwashangilia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, wapinzani wao Simba wamezungumzia ombi hilo.
Akizungumza na E Fm katika kipindi cha E Sports, Simba kupitia kwa msemaji wake, Haji Manara wamesema wao hawawezi kuwaambia mashabiki wao kuwashangalia Yanga au kuacha kuwashangilia.
Manara amesema mashabiki wa Simba wataenda uwanjani kuangalia mpira kama mashabiki wengine na maamuzi ya kushangilia mchezo huo ni uamuzi wao wenyewe.
“Mimi siwezi kuwaambia washangilie Simba au waache kuwashangilia wataenda kutazama mpira kama mashabiki wa soka nchini na wataamua wenyewe wakae upande upi,” amesema Manara.
Aidha ameongeza kuwa anashangazwa na kitendo cha Muro kuwaomba kuishangilia Yanga kwani kwa miaka iliyopita Simba ilipokuwa na michezo ya kimataifa walikataa kuwasapoti na kutolea mfano mchezo wa TP Mazembe uliochezwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kuwepo tuhuma kuwa mashabiki wa Yanga walivaa jezi za Mazembe na kuishangilia.