Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(OR-TAMISEMI) George Simbachawene amewaagiza wadau wa mradi wa mabasi
yaendayo haraka yanayosimamiwa na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka
(DART) kuhakikisha wanampatia taarifa ifikapo Aprili 3, 2016 ni lini
mradi huo utaanza kutoa huduma.
Uamuzi
huo wa Waziri Simbachawene unafuatia makubaliano yaliyofikiwa wakati wa
kikao na wadau hao Machi 31, 2016 kilichofanyika ofisi za DART jijini
Dar es salaam ili kuhakikisha wanatoa huduma ya usafiri wa uhakika kwa
Watanzania na hasa wakazi wa jiji hilo.
“Kama
mambo yote yataenda vizuri mradi huu utaanza mapema angalau mabasi 50
yaanze kutoa huduma mapema iwezekanavyo,” alisema Simbachawene.
Simbachawene
alisema kuwa hadi sasa mabasi mawili yamesha anza kufanya majaribio
katika barabara za mradi huo na kuwahimiza wadau hao waongeze idadi ya
mabasi yanayofanya majaribio angalau yafike 15 ili madereva wazoee
barabara kabla ya mradi kuanza kutoa huduma rasmi.
Ili
kuongeza kasi ya kukamilisha mradi huo, Simbachawene amewataka wadau
hao wa mradi wa mabasi yaendayo haraka wawe na utaratibu wa kukutana
kila siku kwa kuzingatia kazi walizojipangia na kuangalia utekelezaji
wake umefikia wapi na kumpatia taarifa kila baada ya siku mbili.
Aidha,
Simbachawene amewaasa wakazi wa jiji la Dar es salaam kuwa watulivu kwa
kuwa kazi kubwa ya mradi huo imekamilika na mradi umekaribia kuanza
kuleta matunda na hivyo waitunze miundombinu hiyo ikiwemo barabara na
vifaa vitakavyokuwa vinatumika wakati wa kutoa huduma.
“Kuhujumu
miundombinu ya DART ni kulihujumu taifa letu, watu wote ni lazima wawe
na uzalendo kwa mali yao ili mradi uwe wa tija kwa manufaa ya nchi
yetu,” alisema Simbachawene.
Simbachawene
alisema kuwa utunzaji wa miundombinu hiyo utafanikiwa iwapo kutakuwa na
ushirikiano mzuri kati ya wananchi, wadau wa mradi wa DART na Serikali.
Katika
kikao hicho na wadau wa mradi wa DART, Waziri Simbachawene aliambatana
na Naibu Waziri wake Selemani Jaffo pamoja na viongozi mbalimbali wa
Serikali.
Mabasi
ya Mradi wa Mabasi yaendayo haraka yatakuwa yanafanya safari zake ya
kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi kupitia eneo la Kimara, Ubungo,
Morocco, Magomeni, Feri na Kariaakoo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Takwimu UDART, Hamdi Al-Hadj amesema kuwa
kutakuwa na jumla ya mabasi 140 ambayo yanatarajiwa kutoa huduma katika
mradi wa DART jijini Dar es Salaam.
Kikao
cha Waziri Simbachawene kilihuwahusisha wadau wa mradi huo ambao ni
DART, TANROAD, Msajili wa Hazina, Kampuni ya Simon Group, SUMARTA,
Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) na Jeshi la Polisi.
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO


0 comments :
Post a Comment