Bingwa wa baiskeli Chaptele Muhumba wa Uchukuzi SC akiwa amekumbatia kombe alilotwaa kwenye mashindano ya Mei Mosi.
………………………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
TIMU ya Uchukuzi SC iliyopo chini
ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imeibuka kinara kwenye
mashindano ya Mei Mosi baada ya kutwaa vikombe 11 vya michezo
mbalimbali.
Timu hiyo imetwaa ubingwa katika
michezo ya netiboli, baiskeli na bao (wanaume), kamba (wanawake na
wanaume); huku vikombe vya ushindi wa pili ni vya michezo ya bao
(wanawake) na draft (wanaume); wakati vya ushindi wa ni katika soka,
karata (wanaume), riadha (wanawake na wanaume).
Hatahivyo, kutokana na uwingi wa
vikombe timu hiyo inatarajia kutangazwa mshindi wa jumla kesho kwenye
sherehe za Mei Mosi na kukabidhiwa kombe na Mh. Rais John Magufuli.
Timu nyingine na idadi ya vikombe
zilizopata ni Tamisemi saba kikiwemo cha ubingwa wa soka baada ya
kuwafunga GGM katika fainali kwa magoli 2-0, huku TPDC wakiwa na vikombe
vitano sawa na Tanesco.
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),
wamejikusanyia vikombe vinne, Ujenzi vikombe viwili, na Mawasiliano,
Ukaguzi na Halmashauri ya Nyasa kila mmoja wana kikombe kimoja kila
mmoja.
Awali katika michezo iliyochezwa
jana timu ya Uchukuzi SC iliwafunga Tamisemi kwa magoli 18-15 katika
mchezo wa netiboli, ambapo wafungaji wake Tatu Kitula na Matalena
Mhagama waliwapeleka puta wapinzani wao na hadi mapumziko walikuwa mbele
kwa magoli 11-7.
Washindi wote walikabidhiwa kombe
na mgeni rasmi Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania
(TRAWU), Mussa Kalala, ambaye katika hotuba yake aliwashutumu viongozi
walioshindwa kupeleka timu zao kwenye mashindano hayo na kusema michezo
mahala pa kazi husaidia kuijenga miili ya wafanyakazi kuendelea kuwa
mikakamavu na kuwa na afya bora, ambapo hutoa huduma bora iliyotukuka na
kuzalisha tija zaidi.
Naye Kaimu Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya mashindano ya Mei Mosi, Joyce Benjamin alisema wamesikitishwa
na ushiriki wa timu chache mwaka huu, ambazo ni 11 pekee ukilinganisha
na mwaka jana zilikuwa 28.
“Pamoja na kamati yetu kusikitika
kwa uchache wa timu zilizoshiriki katika michezo ya mwaka huu, hata mkuu
wa mkoa katika hotuba yake ya uzinduzi wa michezo hii naye alisikitika
ambapo wote kwa pamoja tumesikitishwa sana na viongozi wengi kutoleta
timu zao hatujii kwa sababu ya kumuogopa Mh. Rais pengine kwanza labda
amekataza michezo, au wana sababu zingine tu zao binafsi,” alisema
Benjamin.


0 comments :
Post a Comment