Mkazi wa Mtaa wa Mateka,
Manispaa ya Songea, Denis Komba (26) kafa baada ya nyoka wake aliyekuwa
amembeba kwenye mfuko wa jaketi kuuawa na wananchi.
Komba alifariki dunia
katika hospitali ya Rufaa Songea mkoa wa Ruvuma (Homso) ambako alilazwa
baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na fimbo nyoka wake huyo.
Mashuhuda wanaeleza kuwa
kabla ya wananchi kumuua nyoka huyo, Komba aliwasihi wasifanye hivyo
kwa kuwa wakimuua na yeye angekufa, lakini ombi lake hilo
halikusikilizwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda
wa tukio hilo, siku ya tukio Komba alikodi pikipiki ya Kassian Haule
(24) ambaye ni mkazi wa Mpitimbi, yenye namba za usajili MC 724 AKB ili
apelekwe nyumbani kwake mtaa wa Mateka.
Akisimulia tukio hilo,
alisema alipofika katika eneo la Benki ya Posta ya zamani barabara kuu
ya Sokoine, dereva wa pikipiki alihisi kuna kitu kinamtekenya na
kumgonga gonga kwa nyuma, ndipo alipogeuka nyuma na kumwona abiria wake
amebeba nyoka mkubwa huku amesimamisha kichwa.
Haule alisema, baada ya
kumuona nyoka huyo aliruka kutoka kwenye pikipiki na kuanguka pembeni
mwa barabara na abiria wake alimwachia yule nyoka ambaye alikimbilia
kwenye kalavati la maji.
Aliongeza kuwa ndipo
alipopiga kelele za kuomba msaada na kundi la vijana waendesha pikipiki
wenzake walifika eneo hilo la tukio kwa lengo la kumsaidia mwenzao juu
ya maswahiba yaliyompata hadi kumfanya apige kelele.
Alisema kabla ya vijana
hao hawajafanya jambo lolote, Komba aliwaomba vijana hao na watu wengine
waliofika katika eneo hilo wasimpige nyoka wake kwani iwapo watampiga
na kufa yeye pia atapoteza maisha. Kutokana na maneno hayo, Haule
alimtoa nyoka huyo ndani ya kalavati na kwa kushirikiana na vijana
wenzake walianza kumpiga nyoka huyo hadi kufa.
Alisema wakati wanampiga
nyoka huyo, Komba ambaye ndiye mmiliki wa nyoka huyo naye alianza
kulegea kisha akaanguka chini huku akitokwa na mapovu mdomoni na puani.
Habari zinasema
kuwa,baada ya Komba kuanguka alikimbizwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa
matibabu; hata hivyo juhudi za madaktari na wauguzi wa hospitali za
kuokoa maisha yake zilishindikana kwani Komba alifariki.
Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kuongeza kuwa mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote na
umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya rufaa
Songea.
Alisema nyoka aliyeuawa
na wananchi amechukuliwa na idara ya maliasili na uchunguzi zaidi ya
tukio hilo unaendelea ili kubaini kiini cha tukio hilo la kuuawa kwa
nyoka na kisha mmiliki wake naye kufa. Kamanda Mwombeji alisema, kwa
upande wa dereva wa pikipiki yeye anaendelea vizuri na anapatiwa
matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma.
Aidha Kamanda Mwombeji,
ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja kumiliki nyara za serikali
zinazoweza kuwaletea madhara kama vile majeraha au vifo
Source: Habari Leo
0 comments :
Post a Comment