Ni
rahisi sana kutamka neno afya, neno hili linajenga dhana ya hali ya
ukamilifu kimwili, kiakili, kijamii na kutokuwepo kwa maradhi ambayo
huleta hali ya kuwa huru na kutokuwa na hali ya kuumwa au udhaifu wa
mwili.
Kuwa
na afya tu haitoshi, mwanadamu anapaswa kuwa na afya bora ambayo
huchukuliwa kama nguzo na raslimali muhimu katika kuchangia maendeleo ya
mtu binafsi, familia na nchi hususan katika kuleta maisha bora na
kupunguza umaskini.
Kwa
mantiki hiyo, afya bora inalenga kuwa na ustawi endelevu kwa jamii, kwa
kuzingatia mchango wa mtu binafsi kulingana na nafasi, uwezo na fursa
zilizopo katika kuleta maisha bora.
Upatikanaji
wa afya bora unahitaji uwezeshaji wa jamii yenyewe iwe na uwezo wa
kushiriki, kuamua, kupanga na kutekeleza mikakati yao ya kuwaletea
maendeleo katika ngazi mbalimbali.
Ili kuwa na afya bora ni vizuri kujiuliza maswali kadhaa ambayo ndiyo yatajenga msingi imara wa afya ya mtu binafsi au jamii.
Maswali
hayo ni pamoja na Unakula nini? Unakula kiasi gani? Unakula aina gani
ya vyakula? Una lala kwenye nini? Unalala masaa mangapi kwa siku?
Unafanya mazoezi? Unakula mara ngapi kwa siku?Unakunywa nini? Unapata
hewa safi unapokuwa kazini au nyumbani? Unapata muda wa kwenda hospitali
mara kwa mara kupima afya yako?
Maswali
haya ni ya msingi katika kujenga afya bora kwa kuzingatia elimu ya afya
na uhamasishaji miongoni mwa jamii unapaswa kuwa njia muhimu katika
utoaji wa huduma za afya.
Njia
hiyo inatumia utaalamu wa mawasiliano kwa kutayarisha na kuwasilisha
ujumbe mbalimbali kwa mtu binafsi, familia na jamii kwa lengo la
kubadilisha mienendo na tabia zinazochangia kuwepo au kutokuwepo kwa
maradhi katika jamii.
Hali
hiyo ya afya bora inapokuwa tofauti maana nayo hubadilika, watu wengine
husema “Ninaumwa, ninahoma, sijisikii vizuri, ni mgonjwa n.k”.
Misemo
hiyo ambayo hutumiwa kila mara huonesha mtu au jamii fulani afya yao
sio nzuri, mara nyingi watu hawa na wale anaojiona ni wazima wanasahau
wapo miongoni mwao wenye uzito mkubwa kupita kiasi ambapo hali hiyo
inawafanya waonekane wanene kupita kiasi ambao huo ni ugonjwa.
Unene
wa kupindukia hupelekea mwili kuwa na mafuta ya ziada ambayo
hulimbikizana hadi kiwango kinachoweza kuathiri afya na kupelekea
kupungua kwa matarajio ya mtu kuishi muda mrefu au kuwa na ongezeko
kubwa la matatizo ya kiafya.
Utafiti
mpya umeonesha watu wazima wengi duniani ni wanene kupita kiasi na
kwamba hakuna matumaini ya kufikia lengo la kupunguza idadi ya watu
wanene duniani.
Wanasayansi
waliofanya utafiti huo ambao walitoka Chuo cha Imperial cha London,
waliandika katika jarida la kimatibabu la Lancet la Uingereza, wanasema
miongo minne iliyopita, kuwa na uzani wa chini kupita kiasi lilikuwa
tatizo kubwa kuliko unene.
Wanasayansi hao wanasema kuwa idadi ya wanaume wanene imeongezeka mara tatu, na idadi ya wanawake nayo imeongezeka mara dufu.
Profesa Majid Ezzat, ambaye ndiye aliyeongoza utafiti huo, anasema ni kana kwamba kuna “mkurupuko wa unene”.
Wanasayansi
hao wameonya kuwa tatizo hilo ni kubwa sana kiasi kwamba haliwezi
kutatuliwa kupitia njia za kawaida za matibabu au kutenga maeneo ya
kuendeshea baiskeli.
Baada
ya kuchunguza takwimu kutoka nchi 186, watafiti hao walibaini kuwa
idadi ya watu wanene duniani imeongezeka kutoka milioni 105 mwaka 1975
hadi milioni 641 mwaka 2014.
Idadi ya watu walio na uzani wa chini ya kuwango nayo imeongezeka kutoka 330 milioni hadi 462 milioni katika kipindi hicho.
Kiwango
cha unene miongoni mwa wanaume kimepanda kutoka asilimia 3.2 mwaka 1975
hadi asilimia 10.8, na miongoni mwa wanawake viwango vya unene
vimepanda kutoka asilimia 6.4 mwaka 1975 hadi asilimia 14.9 mwaka 2014.
Hali hiyo ina maana kuwa kulikuwa na wanaume wanene 266 milioni na wanawake wanene 375 milioni mwaka 2014.
Kwa
mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Bara la Ulaya ndilo
limeonekana kuwa lenye watu wengi wanene kupita kiasi.
Ripoti
hiyo inayojulikana kwa jina European Health Report iliyotolewa 2015
inasema asilimia 59 ya watu wanaoishi Ulaya wana uzani uliozidi au ni
wanene sana.
Shirika
hilo limesema eneo la Ulaya lililochunguzwa pamoja na baadhi ya maeneo
ya Bara la Asia, ndiyo yenye viwango vya juu zaidi vya unywaji pombe na
uvutaji sigara duniani.
Kutokana
na hali hiyo, maafisa wa WHO wameonya kuwa huenda vijana wa eneo hilo
“wasiishi muda mrefu kama walivyoishi mababu zao”.
Kwa
mujibu wa wataalamu wa Afya wa Kimataifa, unene au uzito mkubwa ni
miongoni mwa vitu vinavyoua watu wengi duniani ambapo inakadiriwa idadi
watu takribani milioni 2.8 hupoteza maisha duniani kote kila mwaka kwa
tatizo la unene.
Hata
hivyo ripoti hiyo imeonya kuwa asilimia 30 ya watu eneo hilo bado
wanavuta sigara, kwa kiwango ambacho kinazidi maeneo mengine yote.
Mkurugenzi
wa WHO anayesimamia Bara la Ulaya Zsuzsanna Jakab amesema “Ripoti hii
imeonyesha matumaini. Lakini bado kuna hatari iwapo uvutaji sigara na
unywaji pombe utaendelea kwa viwango vya sasa. Hii inahusu sana vijana
ambao huenda wasiishi muda mrefu kama mababu zao.”
Aidha,
Jarida la kitabibu la Uingereza limeripoti kuwa, idadi ya watu wenye
uzito mkubwa na wanene kupindukia imeongezeka zaidi katika miaka 30
iliyopita, na kufikia karibu moja ya tatu (1/3) ya watu wote duniani.
Wataalamu wameitaka jumuiya ya kimataifa ichukue hatua za makusudi kwa
pamoja ili kukabiliana na tishio la afya.
Ripoti
iliyotolewa na watafiti kutoka chuo kikuu cha Washington cha Marekani
walioongoza kikundi cha watafiti cha kimataifa imesema, idadi ya watu
wanene na waliozidi uzito duniani imeongezeka kutoka milioni 857 mwaka
1980 na kufikia bilioni 2.1 mwaka 2013.
Ripoti
hiyo imeonyesha kuwa, unene ni changamoto kubwa katika huduma za afya
kwa nchi zote, na ni rahisi zaidi kwa watu wanene na wenye uzito mkubwa
kupata ugonjwa wa moyo, kansa, ugonjwa wa kisukari na maumivu ya mifupa
na kupelekea watu hao kupoteza maisha.
Inasadikiwa
kuwa mwanamke Charity Pierce, 38, anayeishi huko Iowa nchini Marekani
ndiye mwanamke mwenye uzito mkubwa kuliko wote hapa duniani 765 lbs,
akimzidi yule wa Arizona anayejulikana kwa jina la Susanne Eman
aliyekuwa na uzito wa paundi 756 mwaka 2012.
Mtu
mwenye dhamira yadhati ya kupunguza uzito si mtu mwingine wa jamii
yake, tiba halisi ya ya tatizo hili la unene ni mhusika ni muhusika
mwenyewe kujitambua na kujua kuwa ana tatizo na awe tayari kupunguza
uzito.
Mabadiliko ya tabia ni muhimu, mabidiliko hayo yanajengwa katika mfumo wa maisha ya kila siku.
Ili
kuwa na afya bora ni lazima kupunguza uzito uwe unaendana na maumbile
ya mtu na mwenyewe na weze kujilinda ikiwa ni pamoja na kutunza uzito
alionao baada ya kupunguza uzito mkubwa wa awali ambalo ni jambo la
msingi na kuzingatia kufanya mazoezi, chakula na madiliko ya tabia ya
mtu mwenyewe.
Mabadiliko
ya tabia yanachangia mtu mwenye uzito au unene mkubwa kupunguza kiwango
cha chakula anachokula azingatie kula chakula chenye chenye virutubisho
vyote muhimu vya afya na kuongeza kiwango cha kufanya mazoezi.
Kwa
mujibu wa kanuni za afya, Mazoezi husaidia kupunguza uzito hasa kipindi
cha miezi sita ya mwanzo na hutunza uzito uliokusudiwa kwa muda mrefu
ambapo hupunguza mafuta mwilini, huongeza ufanisi wa moyo, hupunguza
tatizo la shinikizo la damu na kuweka sukari katika kiwango
kinachohitajika mwilini.
Inashauriwa
kama mtu anayefanya mazoezi hajazoea kufanya hivyo, ni vizuri aanze
taratibu na kujiwekea malengo ya kufanya mazoezi kwa muda wa nusu saa
kila siku, siku tano kwa wiki ili kuufanya mwili uzoee na kufikia
malengo ya kujenga mwili na hivyo kutunza uzito kulingana na uzito
unaostahili.
Mazoezi
yanaweza kuwa ya aina tofauti tofauti kulingana na mazingira ila
dhamira ya mfanya mazoezi iendelee kuwa ni ile ile ya kupunguza uzito au
unene kwa manufaa ya afya yenye tija na maendeleo kwa mtu binafsi,
familia na taifa.
Mazoezi
hayo yanaweza kuwa ni ya kuogelea, kuendesha baiskeli, kutembea,
kunyanyua vitu vizito ambavyo havina uzito mkubwa pamoja kulinganisha na
uzito wa mwili pamoja na mazoezi ya viungo.
Ni
vema watu wanene sana wajenge tabia ya kupenda kupata ushauri na
wazungumze na madaktari wao kabla ya kuanza mazoezi mapya ili miili yao
ipate mazoezi kulingana na hali zao.
Msingi
wa kupunguza uzito au unene ni kujua kiwango gani cha “kalori” mwili
unahitaji kwa siku ili mtu huyo awe anakula chakula ambacho
hakitazidisha au kupunguza kiwango cha “kalori” zinazohitaji kwa siku.
Inakadiriwa mahitaji ya kalori siku yanatengemeana na umri, jinsia na shughuli za kimwili kwa siku husika.
Mlo
mzuri ambao unachangia mtu kutokuwa na uzito mkubwa ni pamoja na ule
wenye matunda kwa wingi, mboga za majani, nafaka ambazo hazijakobolewa,
mafuta kidogo, mayai, nyama isiokuwa ya mafuta, samaki na kuku ili mwili
upate virutubisho muhimu.
Ili
kupunguza unene au uzito uliozidi, zipo njia nyingi ikiwemo njia ya
kawaida, baadhi ya njia hizo ni kuepuka kula vyakula vya kusindika,
kupunguza ulaji wa kuongeza sugari, jenga tabia ya kunywa maji, pata
usingizi wa kutosha, tumia mafuta ya nazi na mimea zaidi kuliko ya
mifugo, kusukutua meno kila baada ya chakula, kuishinda tamaa ya chakula
unachokipenda pamoja na kula chakula taratibu.
Tabia
ya ulaji wa chakula kwa kasi zaidi ina uwezekano wa mlaji kuwa mnene
ikilinganishwa na wale ambao hula polepole zaidi, kama unakula kwa
haraka sana , unaweza kula kalori nyingi kabla ya mwili wako hujatambua
kwamba umeshiba.
Hapa
nchini Tanzania, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Sera ya Afya ya mwaka 1990 iliyopitiwa mwaka
2007 inatambua kuwa na jamii yenye afya bora itachangia kikamilifu
katika maendeleo binafsi na ya nchi.
Madhumuni
ya Sera hiyo ni kuinua hali ya afya ya wananchi wote na hasa wale
walioko kwenye hatari zaidi, kwa kuweka mfumo wa huduma za Afya
utakaokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa
Watanzania.
Hatua
hiyo itapunguza magonjwa na vifo na hivyo watu wengi kuongeza muda na
umri wa kuishi kwa kuzingatia mahitaji ya makundi maalum, hususan;
watoto wachanga na walio chini ya umri wa miaka mitano, watoto walio
katika umri wa kuanza shule na walio shuleni, vijana, watu wenye
ulemavu, wanawake walio katika umri wa uzazi na wazee.
Ni
dhahiri Tanzania imekuwa msatari wa mbele katika kuhamasisha wananchi
kuhusu masuala mbalimbali ya afya ikiwemo maradhi yanayoweza kuzuilika
ikiwemo uzito ama unene mkubwa kupitia matamasha na maadhimisho
mbalimbali ikiwemo wiki ya utumishi, maonesho ya Sabasaba, siku kuu ya
Wakuliuma maarufu kama Nane Nane pamoja na mashindano ya Shirikisho la
Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) ambapo watu
hupata huduma ya ushauri na kupima uzito wa miili yao.
Hatua
hiyo ni muhimu maana inasaidia watu wengi kuweze kuyatambua na kutafuta
mbinu za kuyadhibiti matatizo ya kiafya yanayowasumbua ikiwa ni pamoja
na kumuelimisha kila mwananchi, aelewe kuwa anawajibika moja kwa moja
kutunza afya yake na ile ya familia yake.
Ni
vema kila mtu ajiepushe na kujiua kwa kujijengea tabia ya kula vyakula
vya mafuta bila kufanya kazi au mazoezi ambayo hupunguza mafuta mwilini.
Je?
Ni sahihi ukinenepa na rafiki yako aliyenenepa kumwambia umependeza
umekuwa mnene! Lakini ukweli ni kuwa unene unamuweka mtu katika
mazingira hatarishi ya magonjwa mbalimbali ya viungo vya ndani ya mwili
kama Moyo na kuziba kwa mishipa ya damu.
Kunywa
juisi ya limao na asali ambayo inasaidia kuua bakteria ambao kwa namna
moja au nyingine watasaidia kuweka mfumo wa chakula na utoaji taka
kufanya kazi vizuri.
Epuka
kuhatarisha maisha yako fanya mazoezi, kunywa maji mengi, aliyenenepa
kupita kiasi mshauri apunguze unene maana kitambi “noma”
Je?
Nani alaumiwe? Mfumo wa maisha au tulaumiwe wenyewe kwa kushindwa
kuudhibiti mfumo wowote wa maisha ikiwemo unene au uzito mkubwa?
Mwanaadamu ni mdhibiti wa kila kitu kama akidhamiria kuwa hivyo.
Imeandaliwa na Eleuteri Mangi- MAELEZO
0 comments :
Post a Comment