Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Joshua Msuya, amewahimiza waandishi wa habari kufanya kazi kwa karibu na TAKUKURU,ili kuharakisha kukomesha vitendo vya kuomba na kupokea rushwa ikiwa ni kuunga mkono dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kukomesha vitendo hivyo.
Msuya ametoa wito huo leo wakati akitoa taarifa yake ya utekelezaji ya   kipindi cha mwaka jana mbele ya waandishi wa habari katika kikao kifupi kilichofanyika ofisini kwake.
Alisema kila Mtanzania ni shuhuda mzuri kwamba serikali ya rais Dk.Magufuli imedhamiria kwa dhati kukomesha  vitendo viovu vya kuomba na kupokea rushwa,ili wananchi waweze kupata haki zao za msingi bila kuzinunua kupitia vitendo  vya rushwa.
“Kama mnavyofahamu kwamba jukumu la kukomesha vitendo vya rushwa sio la TAKUKURU peke yake,ni letu sote na ninyi waandishi wa habari mkiwemo.Tumieni taaluma yenu kufichua vitendo hivi vya kuomba na kupokea rushwa,ili mamlaka husika ziweze kuchukua hatua ya kuvikomesha”,alifafanua Msuya.
Joshua Msuya - TAKUKURU Singida
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Joshua Msuya, akitoa taarifa yake ya utekelezaji kwa mwaka jana mbele ya waandishi wa habari. Msuya alisema kwa mwaka jana (2015) walipokea taarifa ya vitendo vya kuomba na kupokea rushwa 44 na kudai kuwa TAMISEMI imeongoza kwa kulalamikiwa kwa matukio 15. Kulia ni Mkaguzi wa miradi ya serikali kanda ya kati, Domina Mukama.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoani hapa,alisema katika kipindi cha mwaka jana,walipokea taarifa 44 za malalamiko dhidi ya vitendo vya kuomba na kupokea rushwa.
“Idara zinazoongoza kwa kulalamikiwa ni kutoka TAMISEMI..watendaji wa kata na vijiji malamamiko 15,halmashauri na manispaa 14,jeshi la polisi  malalamiko saba na wengineo nane”,alisema.
Aidha,Msuya alisema jumla ya kesi mbili zimeishafikishwa mahakamani mwaka jana, na kesi zingine 11 zinaendelea kusikilizwa, wakati  miradi ya maendeleo ipatayo 30, imekaguliwa.
Kuhusu kudhibiti vitendo vya rushwa katika kipindi hicho, alisema kuwa walichukua hatua mbalimbali ikiwemo na kuchambua mifumo yenye harufu ya rushwa na wametoa elimu juu ya madhara ya rushwa kwenye washara na semina mbalimbali.
Takukuru- Singida
Baadhi ya waandishi wa habari mjini Singida, wakimsikiliza Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Singida, Joshua Msuya, wakati akitoa taarifa yake ya utekelezaji kwa kipindi cha mwaka jana.Amedai jumla ya matukio 44 yaliripotiwa na TAMISEMI iliongoza kwa malalamiko 15.
Pia alisema wataendelea kuwaelimisha wananchi wasitoe rushwa kwa mtu ye yote mtoa huduma bali watoe taarifa za vitendo vya kuombwa hongo mapema iwezekanavyo.
Akisisitiza, alisema TAKUKURU mkoa inatoa wito kwa wananchi wote kwa ujumla,kujiepusha na vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu kutoa taarifa za vitendo vya rushwa pale wanapobaini kutokea/kutaka kutokea kwa vitendo vya rushwa.Vile vile watoe ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi mahakamani pale watakapohitajika kufanya hivyo.
Wakati huo huo,Msuya amewataka watumishi wote wa idara za serikali,taasisi na mashirika yote ya umma wazingatie sheria,kanuni na taratibu za kazi.Wale wote watakao jihusisha na vitendo vya rushwa,sheria kali itachukua mkondo wake.
TAIKUKURU-Singida
Jengo la ofisi ya TAKUKURU  mkoa wa Singida.(Picha na Nathaniel Limu).