Wakati
Rais John Magufuli akiungana na Watanzania wengine wanaofurahia
kugunduliwa kwa gesi ya helium nchini, baadhi ya wataalamu wa miamba
wameshauri uchunguzi zaidi ufanyike ili kuthibitisha uwepo wa kiasi
hicho.
Juzi,
kulikuwa na taarifa za watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Oxford na kile
cha Durham kwa ushirikiano na wataalamu wa madini kutoka Norway kuwa
wamegundua uwepo wa takriban futi 54 bilioni za ujazo za hifadhi kubwa
zaidi duniani ya gesi adimu zaidi ya helium katika Bonde la Ufa, Kusini
mwa Tanzania.
Katika
ukurasa wake wa Tweeter, Dk Magufuli alisema ni jambo la kumshukuru
Mungu huku akiwataka wachumi, wanasheria na Watanzania kwa ujumla
kujiandaa.
“Tunamshukuru
Mungu Tanzania tumegundua gesi aina ya helium, wito wangu kwa wachumi,
wanasheria na Watanzania wote kwa ujumla tujipange. Ugunduzi huu
utuelekeze kujipanga hasa katika eneo la mikataba yetu ili rasilimali
hii adimu isaidie kuujenga uchumi wetu,” alisema.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikaririwa
akithibitisha ugunduzi huo na kusema Serikali itaitumia gesi hiyo
vizuri.
Hata
hivyo, akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa
Miamba (Geological Survey of Tanzania), Profesa Abdulkarim Mruma alisema
hawakushiriki kwenye utafiti huo, hivyo ni mpaka wafanye utafiti wao
kuthibitisha.
“Kwanza
tulikuwa na mradi wa kutafuta helium na Wajerumani na tuliainisha
maeneo yanayoweza kupatikana. Kwa hiyo hao watatifi walikuja kufuatilia
maeneo tuliyoyaweka, ila hatukwenda nao,” alisema.
“Unajua
mara nyingi watafiti wa madini huwa wana tabia ya kutaja viwango
vikubwa vya upatikanaji wa madini ili kuongeza hisa za kampuni zao
kwenye masoko ya madini. Kwa hiyo tutafuatilia kwa kuchimba ili
kuhakikisha kama kweli hicho kiwango walichosema kipo. Kama hakipo
tutawaeleza,” alisema Profesa Mruma.
Alisema
gesi ya helium imekuwa ikipatikana kwa kiasi kidogo nchini tangu wakati
wa ukoloni, lakini ugunduzi wa sasa ni mkubwa kidunia.
Mkurugenzi
wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk James Mataragio
alisema hawana taarifa rasmi ya ugunduzi huo, hivyo hawezi kusema Taifa
litafaidikaje.
“Tangu
jana (juzi) tumeona vyombo vya habari vimeandika kuhusu gesi hiyo.
Ukweli ni kwamba sijapokea taarifa rasmi kuhusu ugunduzi huo. Uchimbaji
wa gesi ya helium ni tofauti kidogo na gesi nyingine, ni mpaka
ithibitishwe kwanza na wataalamu kama ipo kweli ndipo tujue
tutafaidikaje,” alisema.
Mkuu
wa Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Elisante Mshiu
alisema kama kweli kiasi hicho cha gesi kipo, Tanzania itakuwa na gesi
hiyo mara mbili kuliko inayopatikana kote duniani.
Dk
Mshiu alisema gesi hiyo inayopatikana maeneo mbalimbali duniani ina
mita za ujazo 25 bilioni, hivyo iliyopo Tanzania ni mara mbili yake.
Akizungumza
kupitia mtandao wa ABC, mmoja wa wanasayansi Profesa Chris Ballentine
kutoka Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza alisema gesi hiyo
iliyogunduliwa inaweza kutumika kwa zaidi ya miaka 20 ijayo.
Profesa
Ballentine anayefanya kazi na kampuni ya Norway ya kutafuta helium,
alisema ni mara ya kwanza kuitafuta helium na kuipata kwani mara nyingi
hupatikana kwa bahati tu.



Blogger Comment
Facebook Comment