Serikali imejikuta katika wakati mgumu
wakati wa upitishaji wa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa
Umma wa mwaka 2016 baada ya wabunge kupinga baadhi ya hatua
zilizochukuliwa katika muswada huo.
Jana, Bunge lilitumia zaidi ya saa
mbili kupitisha muswada huo huku mvutano ukiibuka katika nyongeza ya
mapendekezo ya ununuzi wa dawa na vifaatiba kufanywa kwa dharura na
kupinga kwa kamati za fedha na mipango kuondolewa katika kusimamia
mchakato wa zabuni kwenye halmashauri.
Mashambulizi hayo yaliongozwa
na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia na wabunge Joseph Kakunda
(Sikonge CCM), Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini CCM) na Andrew
Chenge wa Bariadi Magharibi (CCM), kiasi cha kumfanya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG), George Masaju kukubali baadhi ya mapendekezo ya Bunge
kwa shingo upande.
Hii ni mara ya kwanza kwa wabunge wa CCM kuipinga
vikali Serikali kwa kura wakati wa kupitisha vifungu na kufanya Bunge
lirudishe uhai wa mjadala tangu Ukawa waanze kususia vikao
vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
Awali, katika mjadala
wabunge wengi walipongeza hatua ya Serikali kupunguza muda na gharama za
mchakato wa zabuni, ushirikishaji wa makundi maalumu katika jamii
kwenye zabuni za umma lakini walipinga uamuzi wa kuwaondoa madiwani
katika mchakato wa ununuzi.
Katika kifungu cha 11 cha muswada huo,
Serikali ilikusudia kuondoa jukumu la kamati ya fedha na mipango katika
usimamizi wa masuala ya ununuzi ya halmashauri.
Kabla ya Bunge zima
kukaa kama kamati kupitisha muswada huo, Waziri wa Fedha, Dk Philip
Mpango alieleza kuwa Serikali ilikuwa imeridhia kurudisha jukumu la
kamati hizo ambazo huundwa na madiwani kuwasimamia watendaji
watakaoshindwa kutekeleza kazi zao.
Licha ya Serikali kukubali hoja
hiyo, wabunge bado waliitaka kuingiza maana katika kifungu cha pili na
kuweka maboresho kifungu cha 24 ili vifaatiba na dawa vinunuliwe kwa
dharura huku Masaju akipinga kwa maelezo kuwa suala hilo lingeingizwa
kwenye kanuni atakazotunga waziri.
Ghasia alieleza kuwa vifaatiba na
dawa ni muhimu katika kuokoa maisha ya binadamu hivyo ni vyema
kianzishwe kifungu maalumu katika sheria badala ya kubaki katika kanuni na
kusubiri majaliwa ya waziri.
Kitendo cha Masaju kupinga pendekezo hilo,
kiliwafanya wabunge, Chenge, Sophia Simba (Viti Maalumu) na Kangi Lugola
wa Mwibara kusimama wakisema Serikali inataka kupitisha mambo kibabe.
“Kila
siku sheria zinakuwa mbaya kwa sababu maoni ya wabunge yanapuuzwa.
Serikali ikitaka mambo yake yapite inalazimisha, haiwezekani. Dawa ni
maisha, AG kubali hili na likileta shida mtaleta turekebishe mbona
mengine huwa mnaleta tunarekebisha?” alisema Lugola.
Chenge alisema
Serikali ingekuwa imeipatia muda kamati ya bajeti imalize kazi zake,
kusingetokea mvutano kwa kuwa mengine wangejadiliana na kuyamaliza.
Mvutano huo ulimfanya Ghasia kuhamia kwenye meza ya Chenge ili kupata
ushauri wa kisheria na hata wakati mwingine kusahau na kumweleza Naibu
Spika kuwa baadhi ya masuala angeeleza mwanasheria wake (Chenge).
Pamoja
na Serikali kukataa mapendekezo hayo, wabunge walipigia kura ya
‘Ndiyo’ maboresho ya kamati na kuwaacha Masaju na Dk Mpango wakitikisa
vichwa kwa masikitiko.
Hoja nyingine iliyomfanya Masaju kususia
kuendelea kutetea ni ile ya Profesa Tibaijuka iliyopitishwa na wabunge
ya kuongeza maneno yatakayowataka wazabuni wa kimataifa kuhusisha wazawa
katika kifungu cha 18 cha muswada.
“Msitunge Sheria kwa hasira. Hiki
kifungu kitakuwa kigumu kutekelezeka. Tungeni hivyo lakini mjue itakuja
kuleta shida,” alisema Masaju akionyeshwa kukerwa na kilichofanywa na
wabunge na kueleza maneno hayo tayari yalikuwapo kwenye Sheria ya
Ununuzi ya mwaka 2011 inayoboreshwa.
Sehemu nyingine iliyoleta mjadala
ni pendekezo la Kamati ya Bajeti kuongeza kifungu cha kuanzisha akaunti
maalumu ya ununuzi mdogo mdogo utakaozisaidia taasisi za umma kutumia
wataalamu wa ndani na kununua vifaa vya marekebisho madogo kama
kurekebisha vyoo na vitasa.
Masaju alipinga pendekezo hilo akisema
litafungua ufisadi katika halmashauri jambo ambalo wabunge wamekuwa
wakilalamikia kila siku.


Blogger Comment
Facebook Comment