![]() | |||
|
SERIKALI imesema inaangalia uwezekano wa kuviruhusu vituo vya redio nchini, kurusha matangazo ya vikao vya Bunge moja kwa moja.
Hatua hiyo imekuja baada ya serikali kupokea maoni ya wadau
mbalimbali ikiwemo wanahabari waliokwenda Dodoma, kuonana na Uongozi wa
Bunge kujadili suala hilo la matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa studio ya
kuzalishia vipindi ya Mtandao wa Redio za Jamii nchini (COMNETA) iliyopo
Chuo Kikuu Huria (OUT) jijini Dar es Salaam.
“Jambo moja ni kwamba kupitia studio za Bunge matangazo yatarushwa
moja kwa moja na redio zote zinaweza kupokea matangazo hayo na zenyewe
zikarusha. Hii itasaidia hata kupunguza gharama kwa sababu zamani
ilikuwa ni lazima utume wa waandishi upeleke vifaa, sasa hii redio
nyingi hasa hizi za kijamii haziwezi kumudu,” alisema Nape.
Alisema jambo hilo ni jipya na kwa sababu ni jipya, litakuwa na
mapungufu mengi na kadri siku zinavyoenda lazima kuna wadau
watakaojitokeza kwa ajili ya kuelezea mapungufu hayo, ambayo serikali
itakuwa ikiyafanyia kazi.
Nape alisema serikali iko tayari kukaa katikati ya Bunge, wananchi na
wadau wengine kwa ajili ya kuhakikisha wanapata haki yao ya kupata
taarifa.
Hata hivyo, Nape aliwataka waandishi wa habari kuongeza uzalendo kwa
nchi, kwani wanatakiwa kutambua kuwa mambo wanayoyaandika mwisho
yanakuwa na matokeo chanya au hasi.
Akizungumzia studio hiyo, Nape alisema redio za jamii, zina mchango
mkubwa hasa katika kukuza demokrsaia nchini na kuongeza uelewa kwa
wananchi katika masuala mbalimbali.
Aliongeza kuwa uwekaji wa studio hiyo, utawasaidia hata wanafunzi
wanaosomea fani ya uandishi wa habari katika chuo hicho, kuitumia katika
kujitolea ili kuongeza uelewa wao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sanyasi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira
Rodriguez alisema, shirika hilo linafurahishwa na maendeleo ya redio
hizo nchini.
Alisema, wamefurahishwa na jinsi serikali ilivyorudisha heshima kwa
kuzitumia redio hizo katika kutoa taarifa mbalimbali bkwa wananchi na
hata katika kipindi cha uchaguzi hilo lilionekana.
“…tunapongeza hilo lakini tunaiomba serikali iendelee kuzitumia redio
hizi za kijamii ili kuifikia idadi kubwa ya wananchi hasa wale walioko
pembezoni, sisi UNESCO tunaunga mkono redio hizi,” alisema Rodriguez.



Blogger Comment
Facebook Comment