Wawakiishi pekee wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa, Dar Young Africans imecheza mchezo wake wa pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya TP Mazembe ya Congo DRC na kukubali kichapo cha goli moja kwa bila.
Yanga ambayo ilifanya maandalizi kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuweka kambi Uturuki na kuwaruhusu mashabiki wa soka nchini kutizama mchezo huo bure katika uwanja wa Taifa, ilianza mchezo huo dhidi ya TP Mazembe kwa kasi lakini ilishindwa kutumia vyema nafasi zilizotengenezwa.
Kipindi cha pili TP Mazembe walionekana kubadilika na kuanza kufanya mashambilizi machache katika lango la Yanga na katika dakika ya 75 walifanikiwa kupata goli kupitia mchezaji wake, Merveille Bope baada ya kupigwa faulo fupi karibu na lango la Yanga, goli lililodumu hadi mchezo huo unamalizika.
Kwa matokeo hayo, Yanga sasa imepoteza michezo yake yote miwili baada ya wiki iliyopita kufungwa goli moja kwa bila na Mo Bejaia ya Algeria na leo kupoteza mchezo wa pili dhidi TP Mazembe.
Mchezo unaofuatia wa Yanga unataraji kuwa dhidi ya Medeama mchezo utakaochezwa Julai, 15.