Habari zilizotufikia hivi punde ni kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw.Freeman Mbowe,  na wenzake akiwemo Mzee Edward Lowasa waliokuwa wamekutana kujadili mkutano wa ndani mchana wa leo Jijini Dar es Salaam wameamuliwa kufika Kituo cha Polisi Kati kwa ajili ya kutoa maelezo.
Kwa mujibu wa chanzo cha taarifa hizo zinaelezwa kuwa mbali na Mbowe na Edward Lowasa, wengine ni Makamu Mwenyekiti Bwana Mohamed, Katibu Mkuu, Bw. Mashinji, Pia yupo John Mnyika Mbunge wa Kibamba, Mh. Tundu Lissu na Wabunge wengine pamoja na makada wa juu wa chama hicho.
Hali hii inafuatia viongozi hao wa CHADEMA kukutana katika mkutano wao huo wa ndani licha ya kuwa awali Jeshi la Polisi lilishapiga marufuku mikutano hiyo.
Hivi karibni kutokana na matukio ya kihalifu yanayoibuka maeneo mbalimbali nchini, Jeshi la Polisi lilitangaza kuzuia Mikutano yote ya Ndani ya Vyama vya Siasa hapa nchini mpaka hapo itakapotoa taarifa.
Tukio hilo lilitolewa siku moja tu tangu askari wanne wa Jeshi la Polisi wauawe na majambazi katika jaribio la wizi katika tawi la Benki ya CRDB Mbande nje kidogo ya jiji la Dar es salaam ambapo Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nsato Marijan, alitoa taarifa kuwa Mikutano ya ndani ya vyama vya siasa inatumika kuhamasisha wananchi kuvunja sheria za nchi na kupambana na Askari
Pia aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa wakiwataka wafuasi wao kuwashambulia Maafisa wa Jeshi la Polisi.
Mtandao huu wa Modewjiblog.com, unawahimiza watanzania wote kuwa kitu kimoja na kuachana na mambo ya uvunjifu wa Amani. Pia unatoa rai kwa Wananchi wema kushirikiana na vyombo vyote vya Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu hapa nchini..
WhatsApp Image 2016-08-29 at 18.30.21
Baadhi ya Makada wa CHADEMA  katika moja ya picha kutoka eneo la tukio..