OFISI ya Taifa ya Takwimu imechangia kiasi cha Shillingi million moja na laki sita (1,600,000/=) kwa ajili ya kusaidia wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera na kusababisha vifo vya watu zaidi ya kumi na wengine kujeruhiwa pamoja na kubomoa nyumba na kuharibu mali.
Fedha hizo zimekabidhiwa kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa ili kuiwezesha Serikali kuwafikishia wananchi huduma za msingi za kibinadamu wanazohitaji kwa wakati huu baada ya kukubwa na tetemeko lililosababisha maafa na madhara makubwa.
Fedha zilizochangiwa ni michango iliyotolewa na wadadisi waliokuwa kwenye mafunzo ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa Mwaka 2016 yaliyofanyika mkoani Dodoma.
Kufuatia tetemeko hilo, wadadisi hao waliungana na watanzania wote kuhakikisha wanachangia kile walichonacho ili kusaidia kutoa misaada ya kiutu kwa wahanga wa tetemeko walioachwa bila makazi huku mali zao nazo zikiwa zimeharibiwa vibaya na tetemeko hilo kubwa kuwahi kutokea hapa Tanzania.
Tetemeko hilo la ardhi lililotokea tarehe 10/09/2016 saa 9 na dakika 27 mchana liliathiri maeneo ya mkoa wa Kagera na maeneo jirani likiwa na ukubwa wa kipimo cha “Richter” 5.7 limeacha madhara makubwa kwa wananchi ambao wanahitaji msaada wa hali na mali ili kurejea katika maisha yao ya awali.
Na Emmanuel Ghula.
Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa akipokea kiasi cha Shillingi million moja na laki sita (1,600,000/=) kutoka kwa Mratibu wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa Mwaka 2016, Mariam Kitembe. Weingine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mh. Jenista Mhagama(wa kwanza kushoto), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa (wa kwanza kulia).
Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa mara baada ya makabidhiano ya Shillingi million moja na laki sita (1,600,000/=) fedha zilizochangwa na wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa Mwaka 2016 kwa ajili ya kusaidia wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.
(Picha zote na Robert Okanda)


0 comments :
Post a Comment