Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa onyo kali kwa wananchi wanaotumia vibaya simu za dharura namba 111 na 112 kwa kutoa taarifa za uongo, kuwapa watoto wadogo kupiga simu waongee au kuweka muziki kutokana kwamba kitendo hicho hupunguza utendaji kazi wa askari.
Kamanda wa Kanda hiyo Kamishna, Simon Sirro amewatahadharisha wananchi wote wa jiji la DSM kuwa kutoa taarifa za uongo ni kosa la jinai, na kwamba Jeshi la Polisi litaanza kuwafuatilia wenye tabia hizo kupitia mitandao yake ya General Packet Radio Service (GPRS).
“Mitandao ya GPRS inaonyesha maeneo walipo walengwa na simu wanazotumia tutawakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa za kweli pindi wanapoona viashiria vya hatari.
“Pia tunapenda kuwafahamisha wananchi wote watumie simu zetu kutoa taarifa zenye ukweli na zitafanyiwa kazi kwa wakati na kuona matokeo ya muda mfupi pale wanapoona viashiria vya uhalifu ama tukio lolote linaloleta uvunjifu wa amani,” amesema.