Kikosi Maalum cha Kupambana na ujambazi wa kutumia silaha cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam kimewakamata watuhumiwa watano kwa makosa ya ujambazi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Kamanda Simon Sirro amesema katika tukio la kwanza lililotokea tarehe 14/09/2016 Askari Polisi wakiwa katika ufuatiliaji maeneo ya Goba Wilaya ya kipolisi Kawe Mkoa wa Kinondoni walimkamata mwanamke mmoja mkazi wa Goba, baada ya kupata taarifa kuwa anawafahamu majambazi wanaojihusisha na uvamizi kwenye maduka makubwa.
“Katika mahojiano aliwataja washirika wake watano ambao walifuatiliwa na kukamatwa katika upekuzi walipatikana na silaha moja Bastola aina ya Browning TZCAR No.87881 ikiwa na risasi 17,Katika mahojiano zaidi watu hao walikiri kufanya matukio ya ujambazi wa kutumia silaha jijin DSM na mmoja wao alitaja silaha nyingine zilizofichwa kwenye majaruba ya Chumvi maeneo ya Ununio na kuwaongoza askari hadi kwenye eneo husika,” amesema.
Kamanda Sirro ameeleza kuwa polisi walipofika maeneo hayo mtuhumiwa alianza kukimbia kuelekea kichakani ndipo Askari walirusha risasi iliyompata mguu wa kushoto na kufanikiwa kumkamata.
“Hata hivyo mtuhumiwa alifariki akiwa njiani kuelekea hosptalini baada ya kuvuja damu nyingi kutokana na jeraha la risasi,” amesema.
Ameongeza kuwa “Aidha kati ya watuhumiwa wengine waliobaki mmoja aliwaongoza askari hadi eneo la gongolamboto anakoishi ambapo katika upekuzi alipatikana silaha nyingine aina ya Shotgun Pump action ambayo imefutwa namba za usajili, msumeno mmoja na tupa moja ya kunolea misumeno na visu.
Watuhumiwa wote wanne wanaendelea kuhojiwa mara ya upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.”
Amesema katika tukio lingine Polisi kanda Maalum Dar es salaam mnamo tarehe 05/09/2016 magomeni mtaa wa makumbusho askari wakiwa doria waliokota begi lililokuwa na silaha na kwamba wahusika wa begi hilo walifanikiwa kutoroka. Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta.
“Askari waliwatilia mashaka watu ambao walikuwa wamepakizana kwenye Pikipiki wakiwa na begi dogo mgongoni ndipo askari waliwasimamisha hawakutii amri hiyo, Polisi walifuatilia ili kuwahoji lakini watu hao baada ya kugundua kuwa Polisi wanawafuatilia walianza kukimbia kwa kasi mara wakatupa begi hilo,
“Askari waliliokota baada ya kulipekua begi hilo walikuta Bastola mbili aina ya Browning No, NE984517CAT5802 Ikiwa na risasi 11 na nyigine yenye No. CZ 2075 aina ya RAMI ikiwa na risasi 21 na magazine mbili iliyotengenezwa CZECH REPUBLIC jitihada ya kuwasaka watu hao zinaendelea,” amesema


0 comments :
Post a Comment