Ikiwa mgogoro wa kiuongozi unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) umefikishwa mahakamani kwa ajili ya kupatikana suluhu ya kisheria. Chama hicho kimedai kusikitishwa na mwenendo wa Jeshi la Polisi kwa madai kuwa lina mlinda aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba kwa kushindwa kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya wafuasi wake, iliyodai kuwa walifanya fujo katika mkutano mkuu wa chama hicho, walivamia ofisi kuu ya chama na wale waliohusika na jaribio la utekaji wa Naibu Katibu Mkuu wake Joran Bashange.
Chama hicho kimedai kuwa, kiliripoti kesi zaidi ya mbili kwa jeshi la Polisi lakini hadi sasa hakuna shauri hata moja lililofunguliwa dhidi ya wahusika, na kudai kuwa badala yake limekamata wanachama wake 23 waliokuwa wakitokea Zanzibar kwa madai ya kuimarisha ulinzi, na kuwapeleka mahakamani.
Naibu Mkurugenzi wa Uenezi na Habari CUF, Mbarara Maharagande amewaambia waandishi wa habari kuwa chama hicho kinashangazwa kwamba, hadi sasa Polisi haijafikisha watuhumiwa hao mahakamani na wala hakuna shauri lolote lililofunguliwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Maharagande amedai kuwa “Kiitendo kinachofanywa na jeshi la Polisi ni cha ukiukwaji wa sheria, sisi chama tumesikitishwa na mwenendo wa jeshi hilo sababu linaonyesha kuna watu wanaotakiwa kushughulikiwa haraka, na wapo wanaolindwa ili wasichukuliwe hatua za kisheria.”
Amedai kuwa, katika tukio la jaribio la utekaji wa Bashange lililotokea Septemba 16, 2016 watuhumiwa wake walifikishwa katika kituo cha Polisi cha Buguruni kisha kuachiwa huru, pia amedai kuwa gari ambalo ndiyo kielelezo cha ushahidi wa tukio hilo limeondolewa kituoni hapo.
“Gari la ushahidi lilotumika katika siku ya jaribio la kutekwa naibu katibu wetu, limeondolewa katika kituo cha Buguruni, watuhumiwa wako huru inaonyesha kuna ubabaishaji katika jeshi la Polisi. Hata hivyo katika masijala ya DPP hakuna shtaka la jaribio la utekaji wa Jorani Bashange,”
“Kesi za mwanzo ziko wapi? Lipumba alifanya fujo Agosti 21, 2016 na wafuasi wake tuliripoti hakuna mashtaka, baadhi ya walinzi wake walifanya jaribio la utekaji lakini waliohusika wako huru, walivamia ofisi hakuna shauri lililofunguliwa, walisema yako kwa DPP lakini tulipofuatilia tulikuta hakuna mashitaka,” amesema.
Amedai kuwa “Suala hili linahusiana na kadhia ya jinai vilivyofanywa na wafuasi wa Lipumba,mashitaka tuliyapeleka katika vyombo vya dola yaani jeshi la polisi na mpaka sasa watuhumiwa wa makosa hayo hawajafikishwa katika mahakama, badala yake walipeleka mahakamani wanachama wetu 23 ambao ni walinzi waliotokea zenji kuja kushirikiana na wa bara kulinda ulinzi wa chama. Tumestaajabishwa kwa nini tuhuma za nyuma hazijashuhulikiwa.”
Maharagande ameeleza kuwa, siku ya Jumatatu baadhi ya viongozi wa CUF walikwenda katika ofisi ya ZCO ili kujua maendeleo ya mashauri yaliyofunguliwa na chama hicho, na kwamba walielekezwa kwenda katika ofisi ya DPP kwa kuwa ndipo mashauri hayo yalipofunguliwa.
“Tuliambiwa hakuna shauri linalohusiana na watu wa nne waliohusika na jaribio la utekaji wa naibu katibu mkuu wetu, itambulike kuwa, maelezo ya kuja kwa DPP tumeyapata katika ofisi ya ZCO kwa hiyo Jumatatu tulilazimika kwenda kujua limefikia wapi shauri hilo ndipo tulipofika tukaambiwa hakuna kinachoendelea,” amesema.
Hata hivyo, Joran Bashange amesema waliitwa na polisi kwa ajili ya kuhojiwa lakini walikakataa kujieleza, na kudai kuwa walibaini kwamba wanataka kupewa tuhuma mpya.
“Walitaka kutuhoji kwa tuhuma tusizozifahamu, na ndio wito tulioitiwa lengo la wito lilikuwa kutufungulia mashtaka mapya ambayo hatujayafahamu, walituambia kwamba wamepokea malalamiko kutoka kwa Lipumba, sisi hatukutaka kuwajibu zaidi ya kuwaambia kesi ya Lipumba iko mahakamani kisheria hatuwezi ongea au kutoa maelezo yoyote kuhusu Lipumba,” amesema.
Licha ya tuhuma hizo, Bashange amedai kuwa wamepata taarifa ya kwamba kutokana na ukata wa fedha, wafuasi wa Lipumba wameanza kuuza mali za ofisi ya chama zilizopo Buguruni Jijini Dar es Salaam.
“Sasa hivi Lipumba hana fedha za kulipa wafanyakazi, kuna ukata na wameshaanza kuuza mali za ofisi ili wapate fedha za kujikimu,” amesema Bashange ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi CUF.
0 comments :
Post a Comment