Kamati
ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF) imedai kubaini njama za Prof.
Ibrahim Lipumba waliyemfuta uanachama na kwamba anashikilia kinyume cha
sheria wadhifa wa uenyekiti wa chama hicho, kuwa ana mkakati wa kuchukua
ruzuku ya chama hicho kinyume cha sheria na kuitisha baraza feki ili
kufanya maamuzi ya uvunjaji wa Bodi ya Wadhamini iliyoundwa kihalali na
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa CUF.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi CUF, Julias Mtatiro amedai kuwa Ofisi ya Msajili
wa Vyama vya Siasa imemhakikishia Lipumba kwamba, akishafanikiwa
kuivunja bodi ya wadhamini ya chama hicho, Msajili wa Vyama vya Siasa
Jaji Francis Mutungi atabariki maamuzi ya baraza hilo aliloliita feki.
Mtatiro
amesema baraza lolote litakaloketi kutokana na wito wa Lipumba waliye
mvua uenyekiti, litakuwa si halali na kufafanua kuwa halitakuwa na akidi
halali ya wajumbe kwa kuwa walio wengi hawamuungi mkono Lipumba hivyo
hawatahudhuria.
Ameeleza
kuwa, Baraza halali linalotambulika kisheria na kwa mujibu wa katiba ya
chama hicho, ni lile lililochaguliwa mwaka 2014 ambalo litamaliza muda
wake 2019 ambapo amesema kuwa halimtambui Lipumba kama mwenyekiti wake.
Amesisitiza
kuwa, baraza halali linatakiwa liwe na wajumbe halali 53 na hii ni
kutokana na baadhi ya wajumbe wake 6 kuvuliwa uanachama huku nafasi
nyengine 4 zikiachwa wazi na kwamba idadi kamili ya wajumbe wa baraza
hilo inatakiwa kuwa 63.
Kutokana
na hoja hiyo, Lipumba hatokuwa na mamlaka ya kuitisha baraza halali kwa
kuwa wajumbe 43 kati ya 53 waliohudhuria katika kikao waliliridhia
Lipumba kuondolewa katika chama hicho.
“Chama
chetu kinapata taarifa ya kila kitu kinachoendelea, tuna taarifa mpya
kuwa Lipumba amekaa kikao na Jaji Mutungi katika kuendeleza mikakati ya
kuivunja CUF, awali alikwenda Sakaya katika Ofisi ya Msajili kutafuta
namna ya kupata ruzuku ya chama na kwamba wana wasiwasi kuwa ruzuku
ikiingia itachukuliwa na wengine, ” amesema.
Mtatiro
amedai kuwa Lipumba amepewa maelekezo kutoka kwa ofisi ya msajili wa
vyama vya siasa ya kutengeneza utaratibu wa kuvunja kurugenzi za CUF na
kwamba baada ya kufanikisha hilo, atafute wakurugenzi wapya aliowadai
kuwa ni feki.
“Lipumba
hawezi itisha Bodi halali ya Wadhamini ikasikia wito wake na kutekeleza
maagizo yake sababu hana mamlaka, jana aliita watendaji wa Baraza Kuu
la Uongozi Taifa lakini kwa sababu hana wajumbe halali walioitikia wito
ni hawazidi 6, ila leo hii kamati yangu ikiita watendaji wanakuja wote
hata iwe saa nane usiku, ” amesema.
Aidha,
Mtatiro ametoa onyo kwa Jaji Mutungi kutoendelea kujihusisha na mgogoro
wa chama hicho na kumtaka kutomdanganya Lipumba kuwa ana uhalali wa
kuendelea kuwa mwenyekiti kwa kuwa hatambuliki kisheria.
“Msajili
hawezi akaamua mambo ya CUF, hiki ni chama kinaendeshwa kisheria, na
wala uamuzi wake siyo wa mwisho unaweza pingwa mahakamani,” amesema.
Licha
ya tuhuma hizo kwa jaji Mutungi, wabunge wa CUF wameomba kuonana nae na
kwamba wanataraji kupeleka barua rasmi katika ofisi yake ili kufanya
nae mazungumzo kwa ajili ya kutaka kumshauri kutoruhusu ofisi yake
kukihujumu chama hicho.
Akizungumza
kwa niaba ya wabunge wa CUF, Riziki Ngwale amesema wabunge wa cuf
wataendelea kumsihi jaji Mutungi kutoingilia mgogoro wa chama hicho
unaoendelea sasa.
“Tuanendelea
kumsihi jaji Mutungi kuacha kuhujumu demokrasia kwa kumtambua mtu
ambaye chama chetu hakimtambui. Na sisi wabunge tunaomba kuonana nae kwa
ajili ya mazungumzo naamini atatuelewa,” amesema.


0 comments :
Post a Comment