Ikiwa imesalia masaa machache kabla ya kuanza kutumia vumbi kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), kati ya Mbeya City ambayo inaikaribisha Simba, na wenyeji Mbeya City ikianza kuwatupia lawama Simba kuwa inawafanyia hujuma ili ishinde, Simba nao wamewajibu.
Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe amesema Simba inafanya maandalizi kwa ajili ya mchezo na hakuna hujuma yoyote ambayo wanaifanya na kama Mbeya City watakuwa na hofu na hilo basi waende katika vyombo vinavyohusika.
“Kama kuna malalamiko waende kunapohusika, sisi kama Simba tumefika Mbeya salama na tunajiandaa kwa ajili ya kwenda kupambana katika dakika 90 na kupata alama tatu tunazozihitaji,
“Mpira unachezwa hadharani na unakuwa na wachezaji 11, mimi nadhani haya ni maneno ya kukuza mchezo lakini matokeo yatajulikana baada ya mchezo, Mbeya City ni timu nzuri na mara nyingi wamekuwa wakitusumbua,” amesema Hans Poppe na kuongeza.
“Tuna timu nzuri na hatujapoteza mechi hata moja, sisi kama uongozi wa timu tuna kazi ya kuhakikisha tunapata alama tatu kila mchezo ili tuendeleze rekodi yetu ya kutokufungwa katika michezo yetu”