Leo
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaungana na dunia nzima
kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, siku ambayo ilipitishwa na
Umoja wa mataifa mnamo Oktoba 11, 2011. Kauli mbiu ya kitaifa kwa
mwaka huu ni ‘‘Mimba na ndoa za Utotoni zinaepukika, Chukua hatua
kumlinda mtoto wa kike’’.
Hivyo
basi katika kuadhimisha siku hii Kituo kimeangazia mtoto wa kike hapa
Tanzania na changamoto anazokumbana nazo. Kwa mujibu wa takwimu za sensa
ya watu na makazi ya mwaka 2012, idadi ya watoto wa kike kati ya umri
wa miaka 0-17 hapa Tanzania ni 11,263,891 idadi ambayo ni sawa na
asilimia 48.8 ya watoto wote chini ya miaka 17, ambapo Tanzania bara
kuna watoto wa kike elfu 10,943,846 na Tanzania visiwani idadi yake ni
laki 320,045.
Hivyo
basi nusu ya idadi hii ni wanawake na watoto ikilinganishwa na idadi
ya watanzania wote ambao ni milioni 44,928,923 ambapo kati yao wanawake
ni milioni 23,058,933.
Inasikitisha
kuona kuwa mtoto wa kike hapa nchini bado amekuwa akikabiliwa na
changamoto nyingi na cha kusikitisha zaidi mtoto huyu anaanza kubaguliwa
kuanzia katika ngazi ya familia.
Katika
familia nyingi za kitanzania mtoto wa kike amekuwa akikosa fursa ya
kupata Elimu ukilinganisha na mtoto wa kiume na katika mazingira mengine
wazazi wamediriki hata kuwaozesha watoto wao wa kike kwa ajili ya
kupata fedha ya kusomesha watoto wa kiume. Ukiangalia pia katika suala
zima la Elimu ni ukweli usiofichika kuwa idadi ya wasichana wanaoshindwa
kumaliza masomo kwa sababu za kupata mimba imekuwa ikiongezeka.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Shirika la watoto duniani UNICEF kumekuwa na
ongezeko la mimba mashuleni kutoka asilimia 23 hadi 26 yaani takribani
watoto wa kike 8000 hapa Tanzania kila mwaka hukatisha masomo kwa ajili
ya ujauzito. Vile vile idadi ya watoto wa kike ambao wamekuwa wakimaliza
Elimu ya msingi lakini kutokupewa nafasi ya kujiendeleza kielimu hata
pale wanapokuwa wamefaulu nayo pia imekuwa ikiongezeka na badala yake
mabinti hawa wamekuwa wakilazimika kuingia katika ndoa katika umri
mdogo.
Hali
hii ya Watoto wakike kutokupata fursa ya elimu husababisha ongezeko
kubwa la watoto wa kike wanaosafirishwa kutoka vijijini na kuletwa
mijini kwa minajili ya kuja kuendelezwa kielimu na matokeo yake mabinti
hawa wamejikuta katika wakati mgumu kwa kufanyishwa kazi za ndani bila
malipo stahiki na wakifanyiwa vitendo vingi vya kikatili na vya
kuwadhililisha.
Hali
hii imepelekea mabinti wengine kutoroka kutoka kwa waajiri wao na
kuanza kuishi mtaani na hivyo kurubuniwa na kujiingiza katika biashara
za ngono na wengine hata madawa ya kulevya.
Tumeendelea
pia kushuhudia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kingono kama
ubakaji na ulawiti kwa Watoto wa kike na cha kusikitisha zaidi vitendo
hivi vimekuwa vikifanywa na Ndugu wa karibu sana wa Watoto hawa wakiwemo
wazazi, walezi, majirani na hata walimu huko mashuleni. matukio haya
yamekuwa hayafikishwi Katika vyombo vya Sheria kwani mengi huzungumzwa
kifamilia na kuwaacha watuhumiwa wakiendelea na maisha yao.
Tanzania
pia ni nchi moja wapo yenye idadi kubwa ya ndoa za utotoni kwa
takribani ya asilimia 35 watoto wa kike hapa nchini huozeshwa nchini ya
umri wa miaka 18 na hivyo kukatishwa ndoto zao za kujiendeleza kielemu
na hata ustawi mzima wa maisha yao.
Inasikitisha
zaidi kuona pia pamoja na juhudi mbalimbali za utetezi na ushawishi wa
wanaharakati katika kupinga vitendo hivi viovu na mila kandamizi bado
Ukeketaji umekuwa ni tatizo kubwa sana hapa nchini. Kwa mujibu wa
takwimu za Viashiria vya Idadi ya watu na afya 2010, asilimia 14.6% ya
wanawake Tanzania wamekeketwa na wengi wao ni watoto wa kike.
Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa mbinu mpya zimekuwa zikibuniwa ikiwemo kukeketa watoto mara wanapozaliwa.
Vilevile,
kwa mujibu wa taarifa ya haki za Binadamu ya mwaka 2015 inayotolewa na
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kila mwaka ongezeko la matukio ya
Ukatili kwa watoto ikiwemo watoto wa kike kupewa adhabu kali ambazo
hazilingani na makosa waliyoyafanya, mfano unakuta mtoto anachomwa
mikono moto kwa kosa la kuunguza mboga.
Kwa kifupi watoto wa kike wanapata athari mbalimbali ikiwemo;
- Kuendelea kudidimiza nafasi ya mwanamke katika Jamii na taifa zima kwa ujumla na kuendeleza mfumo dume kwani ukatili mwingi huanzia katika ngazi ya familia
- Kutokuendelezwa kielimu kwa mtoto wa kike na hii hupelekea kuendelea kuwa na idadi kubwa ya Wanawake ambao hawana Elimu na hivyo kuendelea kuwa tegemezi kwa wanaume na pia kushindwa kujikwamua kiuchumi.
- Idadi kubwa ya athari za kiafya zinazowapata watoto wa kike kwa ajili ya kujifungua katika umri mdogo ambayo husababisha wengine kupoteza maisha, kupatwa na fistula na maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na magonjwa mengine ya zinaa.
- Malezi duni ya watoto kwa kuwa watoto hawa wanakuwa bado ni wadogo kuweza kukabiliana na jukumu kubwa la malezi na matunzo ya familia.
- Kuendelea kuongezeka kwa Ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwani watoto hawa mara nyingi huolewa na watu waliowazidi umri sana na hivyo kutokuwa na maamuzi yoyote katika nyumba.
Hivyo basi tunapendekeza yafuatayo:
- Katika ngazi ya familia wazazi na walezi kuthamini na kuwajali watoto bila ubaguzi wa jinsi zao. Watoto wote wapewe fursa sawa kielimu na kujiendeleza kimaisha. Wazazi kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili hasa Ukatili unaoanzia majumbani,sambamba na hilo kutoa taarifa za matukio ya Ukatili wanayofanyiwa watoto na sio kutatua matatizo haya katika ngazi ya familia ilihali haki ya mtoto inapotezwa.
- Wito kwa Jamii kuwajibika katika kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili. Kuthamini nafasi ya kila mtoto na kuona mtoto wa mwenzako ni wa kwako; pia kutoa taarifa ya matukio ya Ukatili katika maeneo wanayoishi na sio kufumbia macho na kuwaficha waovu.
- Serikali kuhakikisha kuwa sheria zilizopo zinasimamiwa na zinatekelezwa pale zinapovunjwa kwa kuweka mifumo iliyowazi na rahisi ya kupata na kufuatilia haki
- . Vile vile kubadilisha sheria ambazo bado zimekuwa ni kandamizi kwa mtoto wa kike ikiwemo Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoafiki mtoto wa kike kuolewa katika umri wa miaka 15. Serikali itekeleze agizo lilitolewa na Mahakama Kuu Julai 8 2016 la kubadili kifungu na 13 cha sheria ya ndoa 1971 juu ya ndoa za utotoni
- Serikali kwa kupitia taasisi zake kama polisi na mahakama kuhakikisha kuwa Mashauri yanapolekwa Mahakamani yanasikilizwa bila vikwazo na kutolewa maamuzi kwa wakati stahiki maana ‘justice delayed is justice denied’ – ‘kuchelewesha haki ni kunyima haki’.
- Wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa ya matukio ya Ukatili wanayofanyiwa watoto ili wale wanaofanya vitendo hivi waaibishwe na waadhibiwe kwa mujibu wa sheria; tunavitaka vyombo vya Habari visiishie tu kuripoti matukio haya pindi yanapofanyika bali hata kuendelea kufuatilia mashauri yaliyopo mahakamani ili kusaidia mashauri haya yafanyiwe kazi kwa wakati.
- Pamoja na hilo tunaviomba vyombo vya habari kuwa makini jinsi wanavyoripotia matukio haya ya Ukatili kwa watoto kwani utoaji wa taarifa hizi wakati mwingine umekuwa pia ukiendelea kuwavunjia haki watoto hawa kwa kutozingatia sheria inayotaka utoaji wa taarifa za watoto kutunza majina halisi ya watoto na hata sura zao.
- Na mwisho kabisa tunaomba viongozi wetu katika ngazi zote za kijamii na hata kitaifa kuibeba ajenda ya haki za watoto na hususani haki za watoto wa kike kama ajenda ya kitaifa ili kuhakikisha wanalindwa dhidi ya vitendo viovu na wana mazingira salama ya kukua na kuwa watu wema na mustakabali mzuri wa maisha yao ya sasa na ya baadae.
Tunawashukuru sana.
Wasalaam, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
Dr. Helen Kijo-Bisimba Mkurugenzi Mtendaji


0 comments :
Post a Comment