October 7,
2016 Mtu wangu nimeipata hii kutoka Serikali ya Burundi ambayo imeamua
kuchukua uamuzi wa kujiondoa kuwa mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya
Uhalifu (ICC). Uamuzi huu unakuja baada ya wataalamu huru wa Umoja wa
Mataifa kutoa orodha ya viongozi 12 serikalini ambao wanatuhumiwa
kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu nchini Burundi.
Inaelezwa
kuwa watu hao karibu wote ni washirika wa karibu wa Rais Pierre
Nkurunziza, na na uamuzi wa kujiondoa kuwa mwanacahama wa ICC
ulichukuliwa katika kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika Alhamisi
wiki hii.
Uamuzi wa
Burundi umekuja wakati huu ambapo baadhi ya nchi za Afrika
zinazishawishi nchi nyingine kujitoa kwenye mahakama hiyo kwa sababu ya
kile wanachodai kuwa mahakama hiyo inawalenga viongozi wa Afrika peke
yake. Msemaji wa serikali ya Burundi, Philippe Nzobonariba,
amethibitisha kutoka mjini Bujumbura kwamba uamuzi huo umechukuliwa na
kwamba kinachosalia ni kupitishwa na Bunge pamoja na baraza la seneti.
Itafahamika
kwamba maafisa wa ngazi ya juu katika jeshi, polisi na baadhi ya
maafisa serikalini nchini Burundi wanatuhumiwa na mashirika mbalimbali
ya kimataifa ya haki za binadamu kuhusika na vitendo viovu mbalimbali
ikiwa ni pamoja na mauaji na mateso dhidi ya wanaharakati wa haki za
binadamu, wanasiasa na wafuasi wa upinzani.
Wakati huo
huo Mwendesha mashataka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa
kivita ya ICC, amesema kuwa, itakuwa siku ya huzuni kubwa ikiwa nchi za
Afrika zitaamua kujitoa kwenye mkataba Roma unaotambua mahakama hiyo.
Fatou
Bensouda ametoa wito kwa wakuu wa nchi za Afrika kuachana na mpango wao
wa kujiondoa kwenye mahakama ya ICC, akisema kufanya hivyo kutawanyima
wananchi wengi wa Afrika haki na wahalifu kuendelea kulindwa.


0 comments :
Post a Comment