Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) leo imekifungia kipindi cha ‘Take One’ kinachorushwa na kituo cha runinga cha Clouds tv, kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo kuanzia leo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Joseph Mapunda amesema kuwa kipindi hicho kimefungiwa baada ya kilichorushwa Agosti 9, 2016 kukiuka kanuni za huduma za utangazaji (Maudhui).
Kutokana na mtangazaji wake Zamaradi Mketema kufanya mahojiano na Gift Stanford ‘Gigy Money’ ambayo kamati hiyo imeyatathimini na kubaini kuwa yalikiuka maadili na kanuni za utangazaji.
Mapunda amesema, kipindi hicho pia kimeingilia masuala binafsi ya watu kwa kuyaweka wazi na kutaja majina bila ya ridhaa yao. Kipindi hicho pia kimedaiwa kuwa na mwelekeo wa kuhamasisha vijana kufanya biashara ya ngono ili kujipatia fedha.
Pia amesema kamati hiyo imetoa onyo kwa kituo cha Clouds Television kwa kukiuka Kanuni za Huduma za Utangazaji (maudhui) 2005.
“Clouds Television inapewa onyo kali kwa kukiuka kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) 2005 Na. 5 (c,d,e,f,) na 9 (1), 14 (1) na 15 (c),” amesema na kuongeza.
“Kipindi cha Take One kinafungiwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia leo, katika muda huo wa kufungiwa, Clouds inatakiwa kukitathimini kwa lengo la kupata njia bora ya kukiendesha na kupeleka mapendekezo TCRA kwa ajili ya kuridhia kabla ya kipindi hicho kufunguliwa,” amesema.
Aidha, Mapunda amesema kabla ya kamati hiyo kutoa maamuzi hayo, uongozi wa Clouds Television ulitoa utetezi wake.
Hata hivyo, Mapunda amesema haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo katika Baraza la Ushindani wa Haki na Biashara uko wazi ndani ya siku 30 kuanzia leo.