Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema haimuogopi kumwadhibu
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na imemuonya tabia yake ya
kushindwa kufuata taratibu za kisheria anapokuwa na udhuru siku kesi
yake inapopangwa kusikilizwa.
Kadhalika
imesema Lissu anatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa jamii, mshtakiwa huyo
alishindwa kufika mahakamani mara tatu mfululizo kusikilizwa kesi yake
na wenzake watatu dhidi ya mashtaka ya uchochezi kupitia gazeti la
Mawio.
Onyo
hilo lilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya
mahakama yake kutoa amri ya kukamatwa Lissu Novemba 3, mwaka huu.
"Pamoja
na nafasi yako uliyonayo kwa jamii lakini ujue kwamba mahakama
hatukuogopi labda upande wa Jamhuri ulioshindwa kuja kukukamata ...
mahakamani hakuna kuoneana bali taratibu za kisheria zinachukua mkondo
wake" alisema Hakimu Simba.
ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya hakimu na Lissu:
Hakimu Simba ; Awali ulikwenda Ujerumani bila kutoa taarifa mahakamani unadhani tunakuogopa?
Lissu; Sina nia mbaya mheshimiwa hakimu nilipelekwa Ujerumani kwa dharula.
Hakimu Simba ; Je, kesi ya Uchaguzi wa Jimbo la Bunda nayo ilikuwa ni dharula?
Lissu;
Mheshimiwa hakimu nilipotoka Ujerumani nilikuta kesi ya Bunda imepangwa
kusikilizwa na ilikuwa na muda maalumu, niliandika barua Hakimu
Mfawidhi wa mahakama hii ya Kisutu na nakala nilielekeza kwa upande wa
Jamhuri sina nia ya kuidharau mahakama.
Hakimu;
Kutokana na nafasi yako katika jamii ujue kwamba mahakama hatukuogopi
labda upande wa Jamhuri ulioshindwa kukukamata na kukuweka chini ya
ulinzi.
Kabla
ya majibishano hayo, upande wa utetezi ukiongozwa na Mawakili, Peter
Kibatala, John Mallya na Rwekama Rweikiza ulidai kuwa mshtakiwa wa nne
Lissu, ametii amri ya mahakama amejisalimisha mwenyewe.
Kibatala
alidai kuwa Lissu alikuwa na anaendesha kesi ya Uchaguzi wa Jimbo la
Bunda na kwamba pamoja na kuwa mshtakiwa pia ni wakili wa kujitegemea.
Akijibu
hoja za utetezi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita alidai
kuwa, Lissu ni ofisa wa mahakama kama wakili na kwamba anajua taratibu
za kufuata anapokuwa na udhuru wa kufika mahakamani lakini ameonyesha
dharau kuondoka bila kibali cha mahakama hiyo.
Hakimu Simba alisema kesi hiyo itatajwa Desemba 20, mwaka huu na dhamana za washtakiwa wote zinaendelea.
Mbali
na Lissu, washtakiwa wengine ni, Wahariri wa gazeti la Mawio, Simon
Mkina na Jabir Idrisa na mchapaji wa magazeti, Ismail Mehboob.
Katika
kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, mwaka huu,
Dar es Salaam, Lisu na wenzake walikula njama ya kuchapisha
chapisho la uchochezi katika gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Pia
Lissu na wenzake walidaiwa Januari 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa
nia ya kuleta chuki na uchochezi kati ya wananchi na mamlaka halali ya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walichapisha chapisho hilo lenye
uchochezi.
Aidha,
Lissu alidaiwa siku hiyo kinyume cha sheria na bila ya mamlaka
waliwatishia na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia
kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.
Washtakiwa walikana mashtaka hayo kwa nyakati tofauti.
chanzo:Habari na Mwene Said wa Blogu ya Jamii, Dar es Salaam.



0 comments :
Post a Comment