Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi na Usalama Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 21 Novemba, 2016
amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni Kuu ya
Ulinzi ya Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA) Jenerali Fan
Changlong, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao wamezungumzia uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na China katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika masuala ya ulinzi ambapo Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) limekuwa na ushirikiano na Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA)
Rais
Magufuli amemueleza Jenerali Fan Changlong kuwa Tanzania inathamini
ushirikiano huo ambao umechangia kufanikisha juhudi za kuimarisha JWTZ
zinazolenga kuwa na Jeshi la Kisasa na vifaa bora.
Dkt.
Magufuli amemuomba Jenerali Fan Changlong afikishe salamu na shukrani
zake kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Xi Jinping na
kumhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika
kuimarisha majeshi ya ulinzi na pia katika masuala mengine ya maendeleo
ya kijamii.
“Nimefurahishwa
na ziara yako hapa nchini kwetu, ujio wako unazidi kuimarisha uhusiano
na ushirikiano kati ya nchi zetu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa haya
Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Mwenyekiti
Mao Tse-tung wa China.
“Naomba
unipelekee salamu zangu kwa Rais Xi Jinping na umwambie kuwa pamoja na
kuendeleza uhusiano na ushirikiano wetu katika kuimarisha majeshi pia
tunatarajia kuona China inakuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono
juhudi zetu za maendeleo kwa kujenga viwanda na kushiriki katika miradi
mingine ukiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani
Standard Gauge” amesema Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Jenerali Fan Changlong amempongeza Rais Magufuli kwa
uongozi imara aliouonesha katika Awamu ya Tano na amemhakikishia kuwa
China itaendeleza na kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika
masuala ya usalama hasa kuimarisha JWTZ.
Jenerali
Fan Changlong amesema Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China na Jeshi
la Wananchi Tanzania yana uhusiano wenye manufaa makubwa na kwamba hivi
sasa yanafanya uboreshaji utakaoyaimarisha zaidi na kuwa majeshi ya
kisasa.
Mazungumzo
hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga, Mkuu wa Majeshi
ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange na Makamanda wa Majeshi wa Tanzania
na China.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
21 Novemba, 2016



0 comments :
Post a Comment