Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe
Mhe. Mama Janeth Magufuli, leo tarehe 25 Desemba, 2016 wameungana na
waumini wa Jimbo Katoliki la Singida kusali Misa ya Krismasi
iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatatifu wa Yesu Mjini
Singida.
Misa hiyo Takatifu ya Krismasi imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida Mhashamu Edward Mapunda.
Akizungumza
mara baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu, Mhe. Rais Magufuli
amewatakia heri ya Krismasi waumini wote wa Jimbo la Singida na
Watanzania wote kwa ujumla na amewasihi kusherehekea kuzaliwa kwa Bwana
Yesu kwa kuendeleza amani na upendo na kuacha vitendo vya kubaguana kwa
misingi ya dini, kabila, itikadi na kanda zao.
Dkt.
Magufuli amewahimiza Watanzania wote kuongeza juhudi katika kuchapa
kazi kama alivyofanya Bwana Yesu na pia amesema kwa kuwa maeneo mengi ya
nchi yameonekana kukabiliwa na uhaba wa mvua, ni vema wakatumia vizuri
mvua chache zinazoendelea kunyesha kuzalisha mazao yanayokomaa haraka
ili kuepuka upungufu wa chakula.
Kwa
upande wa Mkoa wa Singida ambao ni maarufu kwa kilimo cha alizeti, Mhe.
Rais Magufuli amewasisitiza kuchangamkia fursa ya ujenzi wa viwanda
ambayo nchi inatoa kipaumbele kwa kuzalisha alizeti kwa wingi ili
zitumike kuzalisha mafuta ya kupikia kwa wingi.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Singida
0 comments :
Post a Comment