Mwenyekiti
wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo amemshangaa
aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwa kuendelea kung’ang’ania siasa
hadi sasa hivi, badala yake anastahili kukaa kimya kula maisha ili
afaidi uzee wake vizuri.
Bulembo
aliyasema hayo wakati akifunga kampeni za udiwani Kata ya Mateves
iliyopo Wilaya ya Arusha juzi, ambako walitarajiwa kumchagua diwani wao
katika uchaguzi mdogo. Mbunge huyo mteule wa kuteuliwa, alisema
anashangaa Lowassa kung’ang’ania madaraka, badala yake anastahili kula
maisha ili kufaidi uzee wake vizuri.
Alisema wapinzani wataruhusiwa kutumia barabara, maji, shule na vinginevyo, lakini kwenda Ikulu haiwezekani.
Aidha,
Bulembo alilaani kitendo cha wafuasi wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), kuingilia msafara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
uliokuwa ukielekea Uwanja wa Ngorbob Sokoni kwa ajili ya kufunga kampeni
za chama hicho.
Alisema
wafuasi wa CCM ni wastaarabu na wavumilivu, hawakufanya fujo, bali
waliwapita kwa mbele na kuelekea kwenye mkutano wa kufunga kampeni.
Mgombea
Udiwani wa Kata ya Mateves, Julius Saing’ore maarufu kwa jina la Sovoyo
na mgombea uenyekiti wa serikali ya kijiji, Mohamed Nassoro maarufu kwa
jina la Arsenal, waliomba kura kwa wananchi hao ili walete maendeleo.
Mgombea
udiwani Saing’ore aliwasihi wananchi wa kata hiyo, kumpa kura ili
waliokwenda mahakamani kudai uchaguzi uliokuwa na kasoro wajue kuwa CCM
ndio yenyewe.
Awali,
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shabani Mdoe alisema
wananchi wana imani kubwa na chama hicho na hawataki porojo, bali
wanataka maendeleo.
Alisisitiza
kuwa awali alipokuwa madarakani aliyekuwa diwani wa CCM kabla ya
kutenguliwa na mahakama mwaka jana, Saing’ore maarufu kwa jina la
Sovoyo, alifanya kazi mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuhakikisha
wananchi wanapata maji safi na salama.
Alisema
diwani huyo ambaye sasa anagombea tena, alikaa madarakani kwa siku 63
kama Diwani wa Kata ya Mateves kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha
Vijiji (Arusha DC) hivyo kurudi kwake kama diwani kutawezesha wananchi
kupata maendeleo.
0 comments :
Post a Comment