KOCHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya
Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Idd Nassor Cheche, amesema kuwa
wanakipanga vema kikosi hicho kuelekea mchezo ujao dhidi ya Simba ili
kuifunga tena na kulinda heshima waliyoiweka Zanzibar hivi karibuni
walipoichapa na kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.
Azam FC inaendelea na maandalizi
makali chini ya Kocha Mkuu, Aristica Cioaba na wasaidizi wake, Cheche na
Kocha wa Makipa, Idd Abubakar, ambao wamekuwa wakikiweka vema kikosi
hicho kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL)
utakapofanyika Uwanja wa Uhuru Jumamosi Ijayo saa 10.00 jioni.
Cheche mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
kuwa vijana wake wanamorali kubwa kuelekea mchezo huo na wanaomba na
kutamani Jumamosi hata ingekuwa kesho kutokana na namna walivyojiandaa
vilivyo.
“Hivi sasa tunaendelea na
maandalizi vijana wako kambini na mazoezi wanafanya kwa nguvu zote kwa
kufuata maelekezo na makosa waliyofanya katika mechi zetu zilizopita
tunaendelea kuyafanyia kazi ili tubadilike kidogo na kufanya vema zaidi
katika mchezo huo.
“Hali ya vijana wangu ipo vizuri,
wanamorali kubwa na wanajitihada ya kufanya kitu, sisi tunatarajia
mchezo utakuwa mkali na wa ushindani lakini vijana wetu watapambana hadi
tone la mwisho la damu na kuhakikisha tunalinda heshima tuliyoiweka
Zanzibar,” alisema.
Nafasi ya Azam kutwaa ubingwa
Akizungumzia muelekeo wa ligi
ulivyo na nafasi waliyopo kama bado wako kwenye mbio za ubingwa, Cheche
alisema wataendelea kupambana hadi mwisho katika kusaka taji la ligi
hiyo.
“Bado tunamechi nyingi hatuwezi
kusema labda tukate tamaa, lolote linaweza kutokea kwa hiyo sisi
tunataka kuhakikisha mechi zetu zote zilizobakia tunashinda, kama
aliyetangulia atateleza basi sisi tutachukua nafasi yake,” alisema.
Timu hizo zinakutana wakati Azam
FC ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikibeba pointi 31
ikizidiwa pointi 14 na Simba iliyojikusanyia 45 kileleni, Yanga ni ya
pili ikiwa nazo 43 huku Kagera Sugar iliyocheza mchezo mmoja zaidi
ikikamata ya tatu ikiwa nazo 34
0 comments :
Post a Comment