Msuva amebakiza mwaka mmoja na nusu kwenye mkataba wake wa kuitumikia Yanga. Credo ambaye anafanya shughuli zake nchini Sweden, amesema kwa kiwango cha mchezaji huyo anatakiwa kuondoka hapa nchini na kwenda nchini humo kwani uwezo wake ni mkubwa.
Credo Mwaipopo
“Nimekuwa nikifuatilia Ligi Kuu Bara na Msuva ni mmoja kati ya wachezaji ambao wanafanya vizuri, nimekuwa nikiwasiliana naye muda mrefu na kumwambia kuwa hatakiwi hivi sasa kuwa hapa nchini kutokana na uwezo wake.
“Soka la sasa linalipa na kwa uwezo wake alionao hastahili kuwa hapo na ukizingatia umri wake bado mdogo ambao ndiyo unaohitajika zaidi Ulaya, Watanzania wengi tumeshindwa kufanya vizuri huko kutokana na kuchelewa kutoka nchini hivyo tulipofika huko tayari umri umeshatutupa mkono.
“Naamini kabisa Yanga ni waelewa watamruhusu aondoke akajaribu bahati yake katika kipindi hiki ambacho bado umri wake unamruhusu na sisi tupo huko tunajua jinsi gani ya kumsaidia akishakwenda Sweden.
“Nafikiri huyu ni Mtanzania na sisi kama Watanzania ni jukumu letu kumsaidia,” alisema Mwaipopo. Alipoulizwa Msuva kuhusiana na suala hilo, alisema:
“Ushauri wake huo nimeusikia ni mzuri na ameutoa muda mzuri ambao na mimi nilikuwa na ndoto za kwenda huko mara tu baada ya kumalizika kwa mkataba wangu na Yanga.”
Msuva amekuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha Yanga, kwa sasa ana mabao tisa sawa na Shiza Kichuya na Amissi Tambwe kwenye Ligi Kuu Bara.
0 comments :
Post a Comment