Katibu
Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema
kukaa kwake kimya kuna kishindo kikubwa kinakuja visiwani Zanzibar.
Maalim
Seif ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya
Umoja wa Kitaifa visiwani humo, alisema kamwe hatorudi nyuma, kwani
hajashindwa na wala haitotokea kushindwa katika maisha yake.
Kauli
hiyo aliitoa jana mjini Unguja, alipokuwa akizungumza katika uzinduzi
wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani, ambapo pamoja na mambo
mengine alisema umaskini sasa umekuwa ukiwatesa wananchi katika kila
eneo.
Katika
uchaguzi huo CUF inawakilishwa na mgombea wake Abdulrazak Khatib
Ramadhan ambaye anapambana vikali na mgombea wa CCM, Juma Ali Juma.
Maalim
Seif ni kama alikuwa akijibu mapigo ya Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Abdurhamn Kinana ambaye mwishoni mwa wiki alisema kuwa
kiongozi huyo anazungumza hali ya kuwa hajui lolote kinachoendelea
katika nchi wala katika chama chake.
“Sasa
nawaambieni musinione kimya, kimya kikuu kina mshindo mkubwa wala
usidhani kuwa tumeshaachia hapana bado kabisa tunaendelea kupigania haki
yenu na haki Inshallah haipo mbali na mimi niwaambieni vijana
sijashindwa na sitoshindwa.
“…na
kama itatokea bahati mbaya nishindwe nitawataarifuni mchukue uamuzi
wenu lakini sitegemei kufika huko kwani mambo haya yana miiko yake,’’ alisema Maalim Seif.
Akizungumzia
hali ya umaskini nchini alisema tangu uongozi wa Serikali ya Awamu ya
Tano, ulipoingia madarakani kwa kile alichodai kwa kutumia mabavu hali
ya umaskini imeendelea kuwatesa wananchi.
Alisema
hali hiyo inachangiwa na uongozi kufanya mambo yasiyokuwa na tija
ambapo kwa kushirikiana na kiongozi mstaafu wa Serikali iliyopita
walifanya mapinduzi na kubatilisha matokeo ya uchaguzi yaliyofanywa na
Wazanzibari waliyoyafanya Oktoba 25, mwaka 2015.
“Lakini
kilichotokea mwaka juzi sasa Serikali imekuwa ya dhulma wale wenye
ajira wanapokonywaa ajira zao ikiwemo kuwaondosha wafanyabiashara
darajani, Kijangwani na sasa wanakwenda Michenzani jambo ambalo ni
hatari kwa Taifa hili,’’ alisema Maalim Seif.
Katibu
Mkuu huyo wa CUF ambaye alikuwa mgombea urais katika uchaguzi uliopita,
alisema pamoja na hali hiyo lakini bado suala la mafuta na gesi
limekuwa na upungufu hasa kupitia sheria yake ambapo sasa kunaifanya
Zanzibar kuwa kama manispaa.
Naye
aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
aliyeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) Edward Lowassa, alimpongeza Maalim Seif kwa kumwalika na jinsi
alivyokuwa mvumilivu katika mambo yote wanayomfanyia.
Alisema Maalim Seif alimshinda aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Rais Dk. Ali Mohamed Shein kwa wastani wa kura 16,000.
Kutokana
na hilo aliwashukuru vijana waliosikia wito wake wa kutofanya vurugu
baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo kwani kama wangefanya hivyo
kulikuwa na hatari ya kupoteza maisha.
Akizungumzia suala la njaa alisema ni ajabu kwa Rais aliyepo madarakani kubeza suala hilo.
Lowassa
alisema kuwa wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu
Julius Nyerere, hasa pale nchi ilipokubwa na baa la njaa, alisema yupo
tayari kuzungumza na makaburu ili kuweza kukabiliana na baa hilo
lililoikumba nchi kwa wakati huo.
Alisema
ni lazima kuhakikisha katika uchaguzi mbalimbali kunakuwa na ushindi na
kila mmoja akatae azuie wizi wa kura kama uliotokea 2015.
“Lazima
kukataa kuibiwa kura ni lazima kukataa kutiwa hofu na kutishwa hii ni
nchi yetu sote tufuate sheria na uchaguzi ujao ni lazima kushinda na
viongozi wanaopambana ni lazima kuungwa mkono kama ilivyokuwa kwa Maalim
Seif ni mfano wa kuigwa,’’ alisema Lowassa.
Naye
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Mazrui alisema wanaingia
katika uchaguzi huo bila kuwa na ruzuku lakini hadi sasa tayari Sh
milioni 20.4 zimepatikana kutoka kwa wanachama wenyewe.
Aliyashukuru
majimbo yaliyochanga ikiwa ni pamoja na Nungwi, Makunduchi, Mtoni,
Magomeni, Kikwajuni, Konde, Chambani, Chakechake, Chonga, Bububu na Ole.
Naye
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Zanzibar, alisema wataendesha
kampeni kistaarabu tofauti na wa upande wa pili ambao ni CCM wanaorusha
maneno badala kueleza sera.
Alitoa
ratiba za kampeni hiyo ambapo Januari 11 atakuwepo Mbunge wa Singida
Tundu Lisu na Januari 15 Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius
Mtatiro atakuwa mgeni rasmi.
0 comments :
Post a Comment