Wakazi
wa Isanga Jijini Mbeya wamekumbwa na taharuki baada ya tukio lisilo la
kawaida ambapo maiti iliyokwenda kuzikwa katika makaburi ya zamani ya
Isanga ilikutwa ikiwa kwenye godoro ndani ya nyumba alimofia.
Taarifa
yaJeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya inasema kuwa tukio lilitokea mnamo
tarehe 16.01.2017 majira ya saa 4:30 asubuhi katika mtaa wa Igoma “A”,
Kata ya Isanga, Jijini Mbeya.
Kufuatia
taarifa hiyo Polisi walifuatilia na kubaini kuwa tarehe 16.01.2017
majira ya saa 1:00 asubuhi mtu mmoja aitwaye JAILO KYANDO na mke wake
aitwaye ANNA ELIEZA wote wakazi wa mtaa wa Igoma “A” waliamka asubuhi na
kukuta mtoto wao wa kwanza aitwaye HARUN JAILO KYANDO amefariki dunia
akiwa amelala.
Taarifa
za awali zinadai kuwa marehemu tangu utoto wake alikuwa na matatizo ya
ugonjwa wa kifafa hali iliyopelekea kuishi nyumbani pasipo kusoma.
Kufuatia
kifo hicho msiba uliendeshwa na taratibu za mazishi zilifanyika. Majira
ya saa 6:00 mchana jeneza lililetwa msibani na kuwekwa sebuleni kando
ya mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeviringishwa na blanketi na kulazwa
chini kwenye godoro, baada ya maombi yaliyoongozwa na walokole waitwao
BONDE LA BARAKA vijana walibeba jeneza hadi makaburi ya zamani ya Isanga
na kisha jeneza kuzikwa.
Waombolezaji
waliporudi nyumbani walitaharuki kuona mwili wa marehemu mtoto HARUN
JAILO KYANDO ukiwa chumbani umelazwa eneo ulipokuwa awali.
Kutokana
na hali hiyo taarifa zilifikishwa Polisi mara moja, askari Polisi
walifika na kurejesha hali ya amani kwa kuuchukua mwili wa marehemu
ambao kwa sasa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Taratibu
nyingine za mazishi zitafanyika leo tarehe 17.01.2017. Mpaka sasa bado
haijafahamika ni uzembe /bahati mbaya wafiwa kusahau kuweka mwili wa
marehemu kwenye jeneza au kulikuwa na hujuma zozote.
Upelelezi unaendelea kuhusiana na tukio hili.



0 comments :
Post a Comment