CHAMA
cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimevunja ukimya
na kuwataka viongozi wa Serikali, hasa wakuu wa mikoa na wilaya kuacha
mara moja kutumia madaraka yao vibaya dhidi ya wafanyakazi.
TALGWU
imesema kuwa viongozi hao wamekuwa wakitumia kile wanachodai utumbuaji
kwa watendaji kiuonevu na ukiukwaji sheria za nchi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TALGWU,
Rashid Mtima, alisema baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitumia
nafasi hiyo kama njia ya kujipatia sifa ama kuonyesha mabavu ya mamlaka
yao.
Alisema
viongozi hao wamethubutu kutumia vibaya nafasi zao kwa kuendeleza
manyanyaso kwa wafanyakazi wa kada ya watendaji wa vijiji, mitaa na
kata, wakiwaadhibu bila kufuata utaratibu wa kiutumishi, huku mamlaka
zinazopaswa kutumika kwa kazi hiyo zikiporwa madaraka yake kwa nguvu ya
kisiasa.
“Jambo
hili ni baya na la hatari kwa mujibu wa mustakabali wa utawala wa
sheria na linapaswa kukemewa mara moja na kwa nguvu zote kwa sababu
likiachwa lina madhara makubwa.
“Tumeshuhudia
matukio ya udhalilishaji na ukiukwaji wa taratibu za kazi wakifanyiwa
kada hii, maofisa watendaji wamekuwa wakiwekwa ndani ovyo kana kwamba
wametenda makosa ya jinai, kutukanwa na kudharauliwa hadharani na
wanasiasa, kusimamishwa kazi ovyo bila kuzingatia mamlaka zao za ajira.
“Kwa
mfano Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, aliwaweka ndani watendaji
wanne wa Kata ya Mikocheni kwa kushindwa kutekeleza maagizo yake,
vilevile Hapi alipotembelea Kata ya Kawe aliwaweka ndani watendaji
watatu wa mtaa kwa kosa la kuwapa mashine za kukusanyia fedha
wakandarasi na kutounda vikundi vya ulinzi shirikishi,” alisema Mtima.
Katibu
mkuu huyo alisema kuwa sheria ya tawala za mikoa ya mwaka 1997 inampa
mamlaka mkuu wa mkoa katika kifungu cha 7 (1) hadi (9) na mkuu wa wilaya
katika kifungu cha 15 (1) hadi (9) ya kuamrisha mtu yeyote kuwekwa
ndani kwa kuona mbele yake au ufahamu wake mtu huyo kuwa ametenda kosa.
Alisema
kifungu kidogo cha (2) cha sheria hiyo kinamtaka mkuu wa mkoa au wilaya
kufanya hivyo pale ambapo atakuwa amejihakikishia kuwa kosa
lililotendwa na mhusika ni lazima litasababisha uvunjivu wa amani kwa
mtendaji na jamii kwa jumla na hakuna njia mbadala zaidi ya kumuweka
ndani.
“Pia
kifungu (3) kinamtaka mtu aliyekamatwa kwa amri au maelekezo ya mkuu wa
mkoa au wilaya afikishwe mahakamani ndani ya saa 48 kwa ajili ya
kufunguliwa mashtaka ya jinai. Endapo hatofikishwa mahakamani kwa muda
unaopaswa na kuisha, anapaswa kauchiwa na hapaswi kukamatwa tena,”
alisema.
Alisema
kwa tafsiri hiyo ya kisheria, ni kwamba viongozi wa kisiasa
hawazingatii sheria hiyo kikamilifu na ni uonevu mkubwa kwa watumishi
waliowekwa ndani.
“Swali
la kujiuliza je, uchunguzi ukishakamilika na ikaonekana watendaji
waliotangazwa hadharani na kudhalilishwa walionewa, viongozi hao wa
Serikali watatumia vyombo vya habari kusafisha majina ya watendaji hao?”
alisema na kuhoji.
Mtima
alisema kuwa TALGWU haitetei wafanyakazi ambao wanakwenda kinyume na
sheria, kanuni na taratibu za kazi, lakini inataka utaratibu ufuatwe na
hatimaye watuhumiwa wachukuliwe hatua stahiki.
“Wito
wetu viongozi wa kisiasa wenye tabia hiyo watambue dhamana kubwa
waliyopewa na Taifa, watumie mamlaka yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na
taratibu za nchi vinginevyo kama chama hatutasita kuchukua hatua za
kisheria,” alisema Mtima
0 comments :
Post a Comment