KAULI YA SERIKALI BUNGENI KUHUSU MWENENDO
WA HALI YA
UCHUMI WA TAIFA
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge Na. 49 (1 ) ya Kanuni za
Bunge toleo la Januari mwaka 2016, naomba kuwasiisha taarifa kuhusu hali ya
uchumi wa Taifa, hususan mwenendo wa
viashiria mbalimbali vya uchumi, ikiwemo ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei,
mwenendo wa sekta ya nje na akiba ya fedha za kigeni, mwenendo wa sekta ya
fedha ikiwa pamoja na hali ya ukwasi na deni la Taifa.
2.
Mheshimiwa
Spika, Serikali inatoa taarifa hii ili kukitaarifu chombo hiki
muhimu cha wawakilishi wa wananchi kuhusu afya ya uchumi wa Taifa letu ili
Waheshimiwa Wabunge waweze kuwafikishia wananchi ujumbe/maelezo sahihi badala
ya uvumi wa mitaani.
Ukuaji wa Pato la Taifa
3.
Mheshimiwa
Spika, ukuaji wa uchumi ni mojawapo ya viashiria
vinavyotazamwa katika kutathmini afya ya uchumi wa Taifa. Ukuaji wa uchumi unapimwa
kwa kutumia ukuaji wa Pato la Taifa yaani thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa
katika nchi katika kipindi kinachorejewa ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
Takwimu za ukuaji wa Pato la Taifa zinaonesha kuwa uchumi wa Taifa umeendelea
kukua na Tanzania imebaki kuwa miongoni mwa nchi za bara la Afrika Kusini mwa
Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa zaidi. Naomba niwape
mifano ya nchi jirani kama ifuatavyo.
Jedwali1: Ukuaji wa Pato la Taifa
Katika Baadhi ya Nchi za Kiafrika
NCHI
|
2015
|
2016 (Matarajio)
|
Burundi
|
-4.0
|
-0.5
|
Kenya
|
5.6
|
6.0
|
Rwanda
|
6.9
|
6.0
|
Tanzania
|
7.0
|
7.2
|
Uganda
|
4.8
|
4.9
|
Zambia
|
3.0
|
3.0
|
Malawi
|
2.9
|
2.7
|
Congo DRC
|
6.9
|
3.9
|
Afrika Kusini mwa Sahara
|
3.4
|
1.4
|
4.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2016
kiwango halisi cha ukuaji wa Pato la Taifa kiliongezeka na kufikia wastani wa
asilimia 6.5 ikilinganishwa na kiwango cha ukuaji cha asilimia 6.3 katika
kipindi kama hicho mwaka 2015. Kwa ujumla, sekta nyingi zilikua kwa kasi isipokuwa
sekta chache. Sekta zifuatazo zilikuwa na viwango vikubwa vya ukuaji katika
kipindi hicho: shughuli za uchimbaji madini na mawe (asilimia 15.8); shughuli
za usafirishaji na uhifadhi wa mizigo (asilimia 15.5); habari na mawasiliano
(asilimia 13.4); na huduma za fedha (asilimia 11.5).
5.
Mheshimiwa
Spika, maoteo ya ukuaji wa Pato la Taifa kwa mwaka 2016
(Januari-Desemba) yalitarajiwa kuwa asilimia 7.2. Hata hivyo, uchambuzi
uliofanywa na Serikali kushirikiana na Shirika la Fedha za Kimataifa (IMF)
unaonesha kuwa ukuaji wa uchumi tulioutegemea unaweza usifikiwe. Matarajio ya
sasa ni kufikia ukuaji wa wastani wa asilimia 7.0. Hii inatokana na mwenendo wa
uchumi katika miezi tisa ya mwanzo ambapo sekta zinazoajiri watu wengi na zenye
mchango mkubwa katika uchumi hazikukua katika kasi iliyotarajiwa ikiwemo sekta
ya kilimo ambayo ilikua kwa wastani wa asilimia 2.1 (matarajio ya mwaka ni
asilimia 2.6) na biashara ilikua kwa wastani wa asilimia 5.6 (matarajio ya
mwaka ni asilimia 7.6). Aidha,
kuzorota kwa uchumi kwa nchi za Jumuiya
ya Ulaya na China ambao ni wabia wetu wakubwa wa biashara na uwekezaji ndio
kumechangia kupunguza matarajio ya awali ya kasi ya ukuaji wa uchumi nchini. Kasi ya ukuaji wa uchumi wa
China inakadiriwa kupungua kutoka asilimia 6.9 mwaka 2015 hadi asilimia 6.6
mwaka 2016.
Mfumuko wa bei
6.
Mheshimiwa
Spika, kiashiria kingine cha jumla cha afya ya uchumi wa
Taifa ni mfumuko wa bei ambao unapima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma
zinazotumiwa na kaya nchini. Mfumuko wa bei ulipungua kutoka asilimia 6.5
Januari 2016 hadi asilimia 5.5 Juni 2016 na kupungua zaidi hadi asilimia 4.5
Septemba 2016 na baadaye kupanda kidogo mwezi Desemba na kufikia asilimia 5.0. Aidha,
mfumuko wa bei kwa mwaka mzima wa 2016 ulipungua na kufikia wastani wa asilimia
5.2 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 mwaka 2015. Maana yake ni kuwa
bei za bidhaa na huduma ziliongezeka kwa kasi ndogo zaidi ikilinganishwa na
kipindi cha nyuma. Mwenendo huu wa kushuka mfumuko wa bei ulichangiwa na kasi
ndogo ya ongezeko la bei za chakula nchini, kushuka kwa wastani wa bei za
mafuta ya petroli katika soko la dunia, utekelezaji madhubuti wa sera za bajeti
na fedha, na utulivu wa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya
kimarekani.
7.
Mheshimiwa
Spika, mfumuko
wa bei unatarajiwa kuendelea kubakia katika viwango vya tarakimu moja katika
siku zijazo na kubakia ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 5.0. Matarajio
haya yatategemea kuendelea kutulia kwa bei ya nishati nchini kutokana na
kuongezeka kwa matumizi ya gesi asilia katika uzalishaji wa umeme, mwendelezo
wa sera thabiti ya fedha na kibajeti, kutobadilika sana kwa bei za mafuta
katika soko la dunia, pamoja na kuendelea kuwepo kwa utulivu wa thamani ya
Shilingi. Hata hivyo, kuna viashiria vinavyoonesha uwezekano wa kuongezeka kwa
mfumuko wa bei kutokana na hali ya ukame uliojitokeza hapa Tanzania na kwa
baadhi ya nchi za ukanda wa nchi za
Afrika Mashariki pamoja na uwezekano wa kuongezeka
kwa bei za mafuta katika soko la dunia.
Mfumuko wa bei katika nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki
8.
Mheshimiwa
Spika, wastani wa mfumuko wa bei kwa nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki uliendelea kuwa imara na kubakia katika wigo wa
tarakimu moja mwaka 2016. Nchini Kenya, mfumuko wa bei ulipungua kufikia wastani
wa asilimia 6.3 mwaka 2016 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.6 mwaka
2015. Hata hivyo, mfumuko wa bei nchini Uganda ulipanda na kuwa asilimia 5.4
ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.2 mwaka 2015.
Thamani ya shilingi
9.
Mheshimiwa
Spika, kiashiria kingine cha afya ya uchumi ni uimara wa
thamani ya shilingi. Katika kipindi cha Julai – Desemba 2016, Serikali
iliendelea na utekelezaji wa sera za fedha na bajeti, hatua zilizowezesha
kuimarika kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani. Katika kipindi
hicho, thamani ya shilingi dhidi ya Dola
ya Kimarekani ilipungua kwa kasi ndogo kutoka wastani wa shilingi 2,144.27 kwa
dola moja mwezi Desemba 2015 hadi shilingi 2,170.44 kwa dola moja mwezi Desemba
2016. Kuimarika kwa thamani ya shilingi kulitokana na hatua mbalimbali za sera
ya fedha zilizochukuliwa na Benki Kuu katika kusimamia hali ya ukwasi kwenye
uchumi pamoja na kuimarika kwa urari wa bidhaa na huduma katika sekta ya nje. Aidha,
thamani ya Shilingi kwa Dola ya Kimarekani ilishuka (kwa takriban asilimia 2.15
katika kipindi cha miezi kumi na mbili kufikia tarehe 19 Januari 2017),
kufuatia kuimarika kwa Dola ya Kimarekani. Kuimarika kwa Dola ya Kimarekani kuliathiri
pia sarafu nyingine zikiwemo yuan ya China (iliyoshuka thamani kwa asilimia
3.55 katika kipindi cha miezi kumi na mbili kufikia tarehe 19 Januari 2017),
shilingi ya Uganda (asilimia 3.7), Faranga ya Rwanda (asilimia 8.55), na Pauni
ya Uingereza (iliyoshuka thamani kwa asilimia 13.04).
10. Mheshimiwa Spika, kuimarika kwa Dola ya Kimarekani kulitokana
zaidi na kupanda kwa riba ya sera ya fedha (policy rate/Fed Fund rate) mwezi
Desemba 2016, hali iliyosababisha wawekezaji kuongeza mahitaji yao ya Dola ya
Kimarekani kwa ajili ya kuwekeza. Aidha, kwa upande wa Tanzania mwezi Januari
ni msimu wa mapato madogo ya fedha za kigeni zitokanazo na mauzo ya mazao ya
biashara, hali ambayo imechangia pia kuwa na dola pungufu kwenye soko la fedha.
Sekta ya Nje na Akiba ya Fedha za
Kigeni
11. Mheshimiwa Spika,
hali ya uchumi inatathminiwa pia kwa kuangalia mwenendo wa biashara ya nje na
akiba ya fedha za kigeni. Katika mwaka
2016, nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za
nje (current account deficit) ilipungua kwa asilimia 48.8 na kufikia nakisi ya
Dola za Kimarekani milioni 2,054.8, kutoka nakisi ya Dola za Kimarekani milioni
4,011.6 kwa mwaka 2015. Kupungua huko kulitokana zaidi na ongezeko la thamani
ya madini hususan dhahabu, bidhaa asilia, mapato yatokanayo na utalii, pamoja
na kupungua kwa thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususan
bidhaa za kukuza mitaji, na bidhaa za matumizi ya kawaida. Katika kipindi
hicho, thamani ya bidhaa na huduma zilizouzwa nje ya nchi ziliongezeka kwa
asilimia 5.2 na kufikia Dola za Kimarekani milioni 9,381.6 wakati thamani ya
bidhaa na huduma toka nje zilipungua kwa asilimia 13.7 na kufikia Dola za
Kimarekani milioni 10,797.4
12.
Mheshimiwa
Spika, hadi mwezi
Desemba 2016, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola ya Kimarekani milioni
4,325.6 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa
takriban miezi 4.2. Aidha, rasilimali za fedha za kigeni za mabenki ya biashara
zilifikia Dola ya Kimarekani milioni 768.2, wakati amana za fedha za kigeni
zilizohifadhiwa na wakazi katika benki za biashara zilifikia Dola za Kimarekani
milioni 2,870.8. Hivyo, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya
kuridhisha.
Mwenendo wa Sekta ya Kibenki
13.
Mheshimiwa
Spika, kiashiria kingine cha hali ya uchumi ni mwenendo
wa sekta ya fedha. Katika kipindi kilichoishia Desemba 2016, tathmini ya
hali ya mabenki yetu na taasisi za fedha inaonesha kuwa mabenki yetu ni imara
na salama, yakiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha: Kiwango cha mitaji
kikilinganishwa na mali iliyowekezwa (total capital to total risk weighted
assets and off-balance sheet exposures) kilikuwa asilimia 17.8 kikilinganishwa
na kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria cha asilimia 10.0.
Hali ya Ukwasi katika uchumi
14.
Mheshimiwa
Spika, ukwasi (liqudity) ni kiasi cha fedha kilichopo katika
uchumi na unajumuisha fedha taslim, amana katika mabenki zilizopo Benki Kuu.
Utoshelevu wa ukwasi katika uchumi unapimwa kwa kuangalia viashiria mbalimbali
ikiwemo ujazi wa fedha, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi, kiwango cha
mitaji ya mabenki, uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslim
na amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi, na upatikanaji wa huduma za
kifedha. Pale ambapo imedhihirika kuwa kuna upungufu wa ukwasi katika uchumi,
Serikali kupitia Benki Kuu huchukua hatua mbalimbali za kisera kuchochea
shughuli za kiuchumi. Hatua hizi ni pamoja na kuongeza ujazi wa fedha na
kuboresha mazingira kwa sekta binafsi kukopa. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya
Fedha na Mipango inaweza kupunguza kodi na kuongeza matumizi ya Serikali.
Hali ilivyo sasa
15.
Mheshimiwa
Spika, hali ya baadhi ya vigezo vya ukwasi nchini ni kama
ifuatavyo: kwa kutumia kigezo cha uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa
kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika kwa muda mfupi (Liquid assets
to Demand Liabilities), uwiano huu ulikuwa asilimia 42.4
ukilinganishwa na asilimia 37.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2015 na
ikilinganishwa na uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia 20. Amana
za wateja katika mabenki zilipungua kidogo
kutoka shilingi trilioni 20.73 mwezi Desemba 2015 kufikia shilingi trilioni
20.57 mwezi Septemba 2016. Miongoni mwa sababu zilizochangia kupungua kwa amana
kwenye mabenki ni pamoja na uamuzi wa Serikali kuhamisha sehemu ya fedha za
taasisi na mashirika ya umma kutoka mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania.
Hata hivyo, amana za serikali kwenye mabenki ya biashara ni asilimia 3 tu ya
amana zote za mabenki. Aidha, jumla ya
rasilimali za mabenki zimeendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 26,917.2
mwezi Desemba 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 27,978.2 mwezi Desemba 2016,
sawa na ongezeko la asilimia 2.6.
Mikopo kwa Sekta Binafsi
16.
Mheshimiwa
Spika, mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia
7.2 katika kipindi cha mwaka ulioishia Desemba 2016 ikilinganishwa na ongezeko
la asilimia 24.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2015. Kupungua kwa kiwango cha ukuaji kulitokana na tahadhari iliyochukuliwa na
mabenki kufuatia kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 6.4 Desemba,
2015 hadi asilimia 9.5 Desemba, 2016.
17.
Mheshimiwa
Spika, ni vema pia ieleweke kuwa kupungua kwa kasi
ya kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi katika miezi ya hivi karibuni siyo
kwa Tanzania pekee. Kwa mfano, kiwango cha ukuaji wa mikopo kwenda sekta
binafsi katika nchi jirani ya Kenya kilipungua kutoka
asilimia 19.7 kati ya Julai na Oktoba 2015 hadi kufikia asilimia 4.1 katika
kipindi kama hicho mwaka 2016. Aidha, Nchini Uganda mikopo kwa sekta binafsi
ilipungua kutoka asilimia 25.2 mwezi Septemba 2015 hadi asilimia -1 mwezi
Septemba 2016. Pia mwenendo usioridhisha ulijitokeza katika mikopo chechefu
katika nchi hizo jirani na kusababisha baadhi ya mabenki hususan Crane Bank ya
Uganda kuwekwa chini ya uangalizi. Hali ni mbaya zaidi kwa nchi kama Nigeria na
Ghana zinazouza mafuta.
18.
Mheshimiwa
Spika, upatikanaji wa huduma za kifedha kwa
wananchi wasiofikiwa na mabenki umeendelea kuongezeka kutokana na ubunifu wa
mipango ya utoaji wa huduma za malipo ya rejareja kupitia simu za mikononi,
pamoja na huduma za uwakala wa mabenki (agent banking services).
Benki zilizopata msukosuko katika robo
ya kwanza
19.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha Julai – Desemba 2016,
CRDB na TIB Development Bank zilipata hasara. Hasara ilisababishwa na tengo kwa
ajili ya mikopo chechefu (provision for non performing loans). Aidha, Twiga
Bancorp imewekwa chini ya uangalizi wa BOT, jambo ambalo si geni. Crane Bank
Ltd ya Uganda iliwekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya nchi hiyo Oktoba 2016
kama ilivyokuwa Imperial Bank Kenya, Oktoba 2015. Licha ya hali hiyo, benki
nyingi zikiwamo CRDB na TIB Development Bank, zimebaki kuwa na mitaji na ukwasi
wa kutosha kwa mujibu wa Sheria. Aidha ni vema kukumbuka kwamba jumla ya benki
na taasisi za fedha nchini kote ni 66 na zina matawi 783. Hivyo, kwa benki tatu
(3) tu kupata msukosuko katika robo moja ya mwaka si sababu ya kuzua taharuki.
Ikumbukwe pia kuwa hiki ni kipindi cha mpito na taasisi nyingi za Kibenki
zilikuwa zinafanya tathmini ya utekelezaji wa maamuzi ya Serikali ya kuyataka
Mashirika na Taasisi za umma kufungua akaunti za mapato BOT na kuhamishia amana
za taasisi hizo hususan akiba za muda maalum (fixed deposit) kutoka kwenye
mabenki ya biashara. Matarajio ya Serikali ni kuwa mara utaratibu mpya
utakapozoeleka shughuli za kiuchumi zitaendelea katika uhalisia wake na Benki
zitaendelea na huduma za mikopo na hivyo kuongeza ukwasi katika Uchumi.
Uamuzi wa Serikali Kuzitaka Taasisi za
Umma Kufungua Akaunti za Mapato Benki Kuu kama sababu ya Kupungua kwa Ukwasi katika
uchumi.
20.
Mheshimiwa
Spika, ni vyema Waheshimiwa Wabunge na jamii ya Watanzania ikafahamu kwamba akaunti
ambazo fedha za mashirika zimehamishiwa Benki Kuu ni akaunti za kukusanya
mapato tu na amana za muda maalum. Akaunti za matumizi bado ziko katika benki
za biashara ili kuyawezesha mashirika kufanya malipo kupitia akaunti hizo.
Hivyo, bado benki za biashara ni kiungo muhimu kati ya mashirika ya umma na
watoa huduma kwa mashirika hayo. Hatua iliyochukuliwa na Serikali inalenga
kuzisukuma benki za biashara kuchukua hatua za ziada kupanua huduma za kifedha
hadi vijijini badala ya kujikita mijini zaidi kuhudumia makampuni makubwa
(corporate sector) na kufanya biashara katika soko la dhamana na hati fungani
za Serikali. Uamuzi huu umesaidia katika usimamizi wa
mapato na matumizi ya Mashirika hayo na pia kurahisisha upatikanaji wa taarifa
za fedha kupitia Benki Kuu. Aidha, Serikali imeacha kukopa fedha zake yenyewe
na kwa gharama kubwa. Kwa kuwa amana za Serikali kwenye mabenki ya biashara ni
sehemu ndogo tu (asilimia 3) ya amana zote za mabenki, madai kwamba uamuzi wa
Serikali kuondoa fedha za mashirika na taasisi kwenda kwenye akaunti za mapato
BOT umesababisha kupungua kwa ukwasi hayana uzito.
21. Mheshimiwa Spika,
naomba kusisistiza kuwa uamuzi wa Serikali kuzitaka taasisi za umma kufungua
akaunti ya mapato Benki Kuu utaendelea kubaki kama ulivyo. Kwa kifupi, fedha
hizi za umma zilikuwa zinatumika vibaya na mashirika lakini pia zilitumika
kuikopesha Serikali fedha zake yenyewe kwa riba kubwa kupitia biashara ya
dhamana na hati fungani za Serikali. Kasoro hiyo iliondoa motisha kwa mabenki
ya biashara kupeleka huduma za kifedha vijijini na hata kukopesha sekta binafsi
(crowding out credit to the private sector).
Utoaji wa fedha kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kipindi cha Julai
hadi Desemba, 2016
22.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa
kupeleka fedha katika Halmashauri zetu kwa kuwa ndiko utekelezaji wa miradi ya
maendeleo na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi unapofanyika. Katika robo
ya kwanza ya mwaka 2016/17, Serikali ilipeleka jumla ya shilingi bilioni 114.7 kwa
ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo. Aidha,
katika robo ya pili ya mwaka, Serikali iliongeza mgao wa fedha zilizoenda
kwenye Halmashauri ambapo kiasi cha shilingi bilioni 203.4 zilipelekwa.
Serikali itaendelea kupeleka fedha katika halmashauri kwa kipindi kilichobaki
kulingana na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu ili kuhakikisha
ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za halmashauri za kuwahudumia wananchi.
Ulipaji wa Madai Mbalimbali
23.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Juni 30, 2016 kiasi cha
shilingi bilioni 3, 113.7 ziliwasilishwa ikiwa ni madai ya wakandarasi,
watumishi, wazabuni na watoa huduma. Baada ya Serikali kufanya uhakiki kupitia
kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ilibainika kuwa madai halali yalikuwa
shilingi bilioni 2,934.2 na madai yaliyokosa vielelezo na hivyo kukosa uhalali
yalikuwa shilingi bilioni 179.5.
24.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha nusu mwaka wa
2016/17, Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 600.2. Kati ya kiasi hicho,
shilingi bilioni 42.35 zilikuwa ni kwa ajili ya madai ya watumishi, shilingi
bilioni 49.46 kwa ajili ya wazabuni, shilingi bilioni 11.2 kwa ajili ya watoa
huduma, shilingi bilioni 30.0 kwa ajili ya madai ya vyombo vya ulinzi na
usalama, na shilingi bilioni 467.2 kwa ajili ya wakandarasi mbalimbali
ikijumuisha shilingi shilingi bilioni 2.0 kwa ajili ya makandarasi wa maghala
na skimu za maji.
25.
Mheshimiwa Spika, kuhusu madeni ya pembejeo, Serikali
bado inaendelea na uhakiki wa madeni hayo ili kubaini madai halali na yasiyo
halali. Hata hivyo, katika kipindi cha Julai – Desemba, 2016 Serikali imetoa
jumla ya shilingi bilioni 10.0 kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo. Aidha, katika
kuhakikisha madai ya wakandarasi, wazabuni, watumishi na watoa huduma wa ndani
wanapewa kipaumbele, Serikali imeweka mkakati wa kutenga fedha kila mwezi
ambapo mwezi Januari 2017 Serikali imetenga jumla shilingi bilioni 70.0.
Jedwali Na. 2: Madeni yaliyolipwa kwa kipindi cha Julai - Desemba, 2016
Jedwali Na. 3: Deni lililobaki baada ya malipo ya hadi Desemba 2016
Mwenendo wa Deni la Taifa
26.
Mheshimiwa
Spika, Deni la Taifa linajumuisha mikopo ambayo hukopwa na
Serikali kutoka nje na ndani ya nchi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya
maendeleo pamoja na kujaza nakisi ya bajeti. Deni la nje hukopwa kutoka kwenye
taasisi za kifedha kama vile Benki ya Dunia, nchi Wahisani na pia kutoka kwenye
benki za biashara wakati deni la ndani linapatikana kwa kuuzwa kwa dhamana za
Serikali (treasury bills) na hatifungani (Treasury bonds), mikopo kutoka Benki
Kuu ya Tanzania na benki za biashara za ndani.
27.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana, na Misaada SURA 134. Aidha, katika kuhakikisha kuwa Deni la Taifa
linasimamiwa kikamilifu Serikali inakamilisha mapendekezo ya marekebisho ya
Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 ili kuimarisha usimamizi wa Deni
la Taifa.
28.
Mheshimiwa
Spika, hadi kufikia Desemba, 2016, Deni la Taifa
likijumuisha deni la ndani na la nje lilifikia Dola za Kimarekani milioni 19,021.9
(debt stock) ikilinganishwa na Dola za Kimarekani milioni 18,459.3 Juni, 2016
ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 3.05. Kiasi hiki cha deni hakijumuishi
deni la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii linalokadiriwa kufikia Dola za Kimarekani
milioni 1,725.8 ingawaje deni hilo limezingatiwa katika tathmini ya uhimilivu
wa deni la Taifa.
29.
Mheshimiwa
Spika, ongezeko la deni hilo limetokana na mikopo iliyopo na mipya iliyopokelewa na
Serikali na ambayo bado haijaiva kutoka mikopo ya ndani na nje ya nchi kwa
ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile reli ya Tazara,
daraja la Kikwete mto - Malagarasi, barabara ya Morogoro – Dodoma, barabara ya
Dodoma – Singida – Arusha, barabara ya Mwanza – Bukoba, mradi wa Maji ziwa
Victoria, Bomba la Gesi Mtwara – Dar es Salaam, barabara ya Dodoma - Singida –
Mwanza, miradi ya umeme Kinyerezi I & II, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano
n.k. Miradi ambayo iligharamiwa na mikopo hiyo imeelezewa kwa kina katika
kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/18 na
katika kitabu cha Uchambuzi wa Deni la Taifa pamoja na miradi inayofadhiliwa na
deni hilo. Pamoja na miradi iliyotajwa, naomba kuweka mezani taarifa ya
Agosti,2016 ya uchambuzi wa Deni la Taifa na miradi yote iliyofadhiliwa na deni
hilo tangu uhuru.
Ulipaji wa Deni la Taifa
30.
Mheshimiwa Spika, ulipaji wa Deni la
Taifa hauangalii ukubwa wa deni lililopo (stock of debt) bali kadri deni
linavyoiva (debt maturity). Hali ilivyo sasa sehemu kubwa ya Deni la Taifa
linaiva kwa kipindi cha muda mrefu (long term maturity). Kutokana na hali hiyo,
kwa wastani (average time to maturity) wa deni lililopo sasa litaiva katika
kipindi cha miaka isiyopungua 11.9. Hali hii inaashiria kwamba athari zake
kwenye bajeti ziko chini (low refinance
risk).
31.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imekuwa ikilipa madeni ya nje na ndani kwa
mujibu wa mikataba. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi kufikia
Desemba, 2016 Serikali ilitumia jumla ya shilingi bilioni 2,570.1 kulipia
madeni ya ndani na nje yaliyoiva. Kati ya kiasi hicho, malipo ya deni la ndani ni
shilingi bilioni 1,822.3 na deni la nje ni shilingi bilioni 747.8. Malipo ya
deni la ndani yanajumuisha malipo ya mtaji (rollover) ya shilingi bilioni
1,367.1 na malipo ya riba ya shilingi bilioni 455.2
32.
Mheshimiwa
Spika, dhamira ya Serikali ni kuendelea kulipa kwa wakati
mikopo yote ya nje inayoiva kwa mujibu wa mikataba. Aidha, Serikali itaendelea
na utaratibu wa kukopa kwa ajili ya kulipa mtaji kwa amana zinazoiva (rollover
of principal maturities of T-bonds and T-bills). Lengo la kuendelea na utaratibu
huo (rollover) ni kutoa ahueni kwenye bajeti ya kila mwaka husika na ni
utaratibu wa kawaida unaotumika na nchi nyingi duniani.
33.
Mheshimiwa
Spika, athari za kutolipa deni kwa mujibu wa mikataba ni
zifuatazo: nchi itahatarisha mahusiano yaliyopo kati yake na nchi wahisani,
taasisi za fedha za kimataifa na mabenki ya nje; nchi inaweza kushtakiwa kwenye
mahakama za kimataifa na kuisababishia hasara na kutopata mikopo; kukamatwa kwa
mali zake (Assets) zilizopo nje na ndani ili kulipia madeni ambayo yatakuwa
hayajalipwa; na kulipa gharama za ziada kama adhabu (penalty) kulingana na
makubaliano na hivyo kuongeza mzigo wa Deni kwa Taifa.
34.
Mheshimiwa
Spika, naomba ifahamike kuwa malipo yote ya
mikopo ya ndani na nje hukasimiwa katika Fungu namba 22. Kwa kuzingatia
utaratibu wa kibajeti, matumizi yote yaliyokasimiwa katika Fungu hili ni
matumizi yasiyo epukika (first charge). Kutokana na utaratibu huo wa kibajeti
na athari nilizozieleza hapo awali za kutokulipa mikopo kulingana na mikataba,
malipo yote ya mikopo ya ndani na nje hulipwa kwa wakati pindi yanapoiva.
Aidha, kwa upande wa madai ya ndani ya makandarasi, wazabuni, watumishi na
watoa huduma, malipo yake hukasimiwa kwenye mafungu mengine ya Wizara, Mikoa na
Halmashauri ambayo hayapo katika kundi la matumizi yasiyo epukika. Hivyo, madai
haya hulipwa baada ya uhakiki kukamilika.
35. Mheshimiwa Spika,
sambamba na ulipaji wa Deni la Taifa, Serikali imeendelea kugharamia utoaji wa
huduma nyingine za jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa mfano,
katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2016 Serikali iligharamia yafuatayo: Ununuzi wa ndege mbili za Serikali na
malipo ya awali ya ununuzi wa ndege 4 shilingi bilioni 234.937; Upanuzi wa
Uwanja wa Ndege wa Dodoma na Mwanza Shilingi bilioni 12.353; Usambazaji wa umeme vijijini Shilingi bilioni 267.529; Ujenzi na
ukarabati wa barabara Shilingi bilioni 916.779; na Usambazaji wa maji vijijini
na mijini Shilingi bilioni 165.213. Aidha, Serikali imeendelea kugharamia mikopo
kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu Shilingi bilioni 277.534; Mfuko wa Reli Shilingi
bilioni 58.04942; Uboreshaji wa huduma za afya katika ngazi zote ikiwemo
ununuzi wa dawa na vifaa tiba Shilingi bilioni 235.229; Mitihani Shilingi
bilioni 64.796; Kugharamia vyombo vya ulinzi na usalama shilingi bilioni 388.4;
na Chakula cha wafungwa Shilingi bilioni 9.0.
36. Mheshimiwa Spika,
mahitaji mengine yaliyopewa kipaumbele ni elimu msingi bila malipo Shilingi bilioni 124.851 (kwa kutenga
shilingi bilioni 18.777 kila mwezi);
Ruzuku ya pembejeo shilingi bilioni 10.00; Ununuzi wa chakula cha
Hifadhi ya Taifa shilingi biliioni 9.00; Deni la kuchapisha Vitabu vya Hati za
Kusafiria Shilingi 2.569; Uendeshaji wa vikao vya Kamati za
Kudumu za Bunge, Mkutano wa Bunge, Posho ya Jimbo kwa Wabunge pamoja na
shughuli za Mfuko wa Bunge Shilingi bilioni 35,262; Michango ya Taasisi na
Jumuiya za Kimataifa Shilingi billion 9.8; Ruzuku ya Vyama vya Siasa Shilingi
bilioni 8.601; Ujenzi wa majengo ya utawala kwenye halmashauri mpya bilioni 10;
Kugharamia balozi zetu nje ya nchi shilingi bilioni 40.7; Ujenzi na ukarabati wa ofisi za Halmashauri Shilingi bilioni 30.10; Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo Tanzania bara Shilingi bilioni 9.0
na Tanzania Zanzibar ni shilingi bilioni 1.4; na Uboreshaji wa miundombinu ya
shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum Shilingi bilioni 2.5.
Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Taifa
37.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo Dhamana na Misaada Sura
134, Serikali inawajibu wa kufanya tathimini ya uhimilivu wa deni (Debt
Sustainability Analysis) kila mwaka ili kupima hali ya deni na uhimilivu wake kwa kipindi cha muda mfupi,
wa kati na mrefu. Kwa kuzingatia matakwa ya Sheria hiyo timu ya wataalamu
wamekamilisha tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa kwa mwaka 2016/17. Matokeo
ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa deni ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na
mrefu. Matokeo hayo yanafanana na yale yaliyotolewa katika taarifa ya IMF ya
uhimilivu wa deni la Taifa iliyotolewa Juni 2016– United Republic of Tanzania Staff report for the 2016 Article IV Consultation, and Fourth Review under Policy Support Instrument ambayo ipo kwenye tovuti
ya IMF.
38.
Mheshimiwa
Spika, katika tathmini iliyofanyika Novemba 2016, viashiria
vinaonesha kuwa: thamani ya sasa ya jumla ya deni la Taifa (Present Value of
Total Public Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.2 ikilinganishwa na ukomo
wa asilimia 56, thamani ya sasa ya Deni la nje pekee (Present Value of External
Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 19.9
ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 97.7
ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa
mapato ya ndani ni asilimia 145.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimi 250.
39.
Mheshimiwa
Spika: kazi ya viashiria hivyo vinne ni kupima uwezo wa nchi kukopa
(solvency threshhold). Viashiria vilivyobaki vinapima uwezo wa nchi kulipa deni
(Liquidity Indicators). Kutokana na tathimini,
ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani umefikia asilimia
11.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20 na Ulipaji wa deni la nje kwa
kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia
20. Kwa kuzingatia vigezo hivyo,
Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea kukopa toka ndani na nje ya nchi ili
kugharamia shughuli zake za maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo
inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje kwa wakati.
40.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na muundo wa deni la Tanzania (debt structure)
sehemu kubwa ya madeni yake yanaiva kwa muda mrefu (miaka 5 hadi 50). Hivyo,
upimaji wa deni la Taifa huangaliwa kwa kutumia thamani ya sasa ya deni
(Present value of debt) badala ya kutumia thamani halisi ya deni (nominal value
of debt) hii inaiwezesha tathmini
iweze kufanyika kwa madeni yanayoiva kwa muda mrefu kinyume na thamani halisi
ya deni kwa pato la Taifa (nominal value of debt to GDP), ambayo inaangalia
hali ya deni kwa muda mfupi. Kwa kuzingatia
hali hiyo, viashiria vilivyooneshwa hapo juu ndio viashiria sahihi
vilivyokubalika kimataifa katika upimaji wa uhimilivu wa Deni la Taifa.
41.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuzingatia vigezo hivyo, uwiano wa deni lote la
ndani na nje kwa thamani ya sasa kwa pato la Taifa (PV of total public
debt/GDP) kwa mwaka 2015/16 Kenya ilikuwa asilimia 45.6, Tanzania asilimia
34.2, Uganda asilimia 24.1, na Rwanda asilimia 22.7. Vile vile, uwiano wa deni la nje kwa thamani
ya sasa kwa Pato la Taifa: Kenya ilikuwa asilimia 19.4; Tanzania asilimia 19.9;
Uganda asilimia 10.7; Rwanda asilimia
17.3 (PV of external debt/GDP) ambavyo vyote bado viko chini ya ukomo.
42.
Mheshimiwa
Spika, vigezo vinavyoelezwa na baadhi ya wadau kama Mhe.
Kishoa kuhusu uhimilivu wa deni la Taifa kwa kutumia uwiano wa nominal debt to GDP siyo sahihi kwa kuwa
upimaji wa uhimilivu wa deni la Tanzania sehemu kubwa ya deni lake linaiva
katika kipindi cha muda mrefu. Vigezo vinavyotumia uwiano wa nominal
debt to GDP ni vizuri kwa kuangalia
mwenendo wa deni badala ya uhimilivu wa deni.
43.
Mheshimiwa
Spika, taarifa ya IMF review mission iliyotolewa Oktoba 31,
2016 inasema hivi naomba kunukuu:
‘‘The mission held discussions on how to address these macroeconomic
challlenges. In particular, the importance of mobilising external financing to
step up the pace of planned capital spending. Tanzania is at low risk of
external debt distress and has room to borrow externally on concessional and
nonconcessional terms to meet its financing needs….It also recommended …acquiring
a sovereign credit rating to expand Tanzania’s opportunities to borrow
abroad…’’
44.
Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha kwamba Deni la Taifa linadhibitiwa na linaendelea kuwa himilivu,
Serikali inatoa kipaumbele kwa mikopo yenye masharti nafuu. Hata hivyo, pamoja
na mikopo hiyo kuwa na masharti nafuu ya kifedha, lakini kuna masharti mengine
ambayo yanagusa maslahi ya nchi na hivyo kusababisha kuchelewa au kushindwa
kuchukua mikopo hiyo. Kwa mfano, masharti ya mkopo kwa ajili undelezaji wa
Bandari ya Dar es salaam kutoka Benki ya Dunia ambapo serikali inasita
kuyaridhia kutokana na maslahi ya taifa.
45.
Mheshimiwa
Spika, katika kuhakikisha kwamba Deni la Taifa linadhibitiwa
na linaendelea kuwa himilivu, Serikali inatekeleza mikakati ifuatayo:
(i)
Kuhakikisha kwamba mikopo inayopewa
kipaumbele ni ile yenye masharti nafuu, na kwamba mikopo yote yenye masharti ya
kibiashara inakopwa kwa uangalifu mkubwa ikiwemo kuhakikisha kwamba mikopo hiyo
inatumika kwenye maeneo ambayo yana vichocheo vya ukuaji wa uchumi;
(ii)
Kuboresha mikakati ya kukusanya kodi ili
kuhakikisha sehemu kubwa ya bajeti yetu inagharamiwa na mapato ya ndani pamoja
na kupunguza matumizi yanayoweza kuepukika;
(iii) Kusimamisha
kabisa utoaji wa Dhamana za Serikali kwa Taasisi za Serikali ambazo zinategemea
ruzuku kujiendesha. Hii itasaidia kupunguza deni linalotokana na taasisi hizo
kushindwa kulipa madeni hayo; na
(iv)
Kuimarisha Usimamizi wa deni kwa kuwa na
Idara maalum ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango itakayokuwa na jukumu la
kusimamia deni la Taifa. Aidha, Serikali inarekebisha Sheria ya Mikopo, Dhamana
na Misaada ili iweze kuwiana na hali ya sasa.
46.
Mheshimiwa
Spika, katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika
usimamizi wa Deni la Taifa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anaendelea
kufanya ukaguzi maalum na yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha taarifa
ambayo itatoa hali halisi ya Deni la Taifa.
Hatua
iliyofikiwa kwa makampuni ya simu kujisajili katika soko la hisa
47.
Mheshimiwa Spika; kwa
mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 kifungu cha 26 kinaeleza kuwa:
(i)
Makumpuni
ya mawasiliano yenye leseni ya kujenga miundombinu ya mawasiliano (Network
Facilities) na yenye leseni ya kutoa huduma za mawasiliano (Network Services or Application
Services) yawe na umiliki wa watanzania usiopungua asilimia 25 ya mtaji wa kampuni
katika kipindi chote cha uhai wa leseni yake;
(ii)
Makampuni
yenye leseni ya huduma ya utangazaji (Content Service Licensee) yawe na umiliki
wa kitanzania usiopungua asilimia 51 ya mtaji katika kipindi chote cha leseni;
(iii) Kiwango cha chini cha asilimia 25 ya
umiliki upatikane kupitia umiliki wa umma kwa mujibu ya Sheria ya Soko la mitaji na
Dhamana;
(iv) Makampuni yaliyotajwa hapo juu ambayo
tayari yalikuwa yanafanya kazi nchini kabla ya tarehe 01 Julai, 2016, yanatakiwa yajisajili
katika soko la hisa ndani ya kipindi cha miezi 6 kuanzia tarehe 1 Julai, 2016;
na
(v)
Makampuni
ambayo yatasajiliwa nchini kuanzia tarehe 01 Julai, 2016 yatatakiwa kujisajili katika soko la hisa ndani
ya miaka miwili toka kuanzishwa kwake.
48.
Mheshimiwa Spika; kuna jumla ya kampuni 80
zilizopewa leseni za miundombinu
ya mawasiliano na huduma za mawasiliano ambazo zinahusika na Sheria hii. Hadi
tarehe 03 Januari, 2017 kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na
Dhamana (CMSA) ni Kampuni tatu tu za VODACOM, AIRTEL na TIGO ndizo
zilizowasilisha nyaraka za usajili ambapo kampuni ya VODACOM ndiyo
iliyowasilisha nyaraka zilizokamilika na kampuni nyingine ziliwasilisha nyaraka
zenye mapungufu. Kampuni nyingine zilitoa taarifa kuwa wapo katika hatua
mbalimbali za kuorodhesha hisa zao ikiwa ni pamoja na kupata ushauri kutoka
CMSA na kwa wataalamu wa masuala ya kuandaa hati maalum za kuorodheshwa kwenye
soko la hisa.
49.
Mheshimiwa Spika; mnamo tarehe 13
Januari, 2017, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kama msimamizi wa Sheria ya
Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (EPOCA) ilitoa notisi kwa kampuni za simu
kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha EPOCA, na kuziagiza kampuni za simu
kuorodhesha hisa zao kwenye soko la hisa, katika kipindi cha siku 30. Baada ya
siku 30 kupita toka notisi kutolewa, TCRA itachukua hatua za kisheria dhidi ya
kampuni ambazo hazijakamilisha usajili wa hisa zao.
Wafanyabiashara kusita kuagiza bidhaa kutoka nje ya Nchi kwa kigezo cha
kwamba uchumi wa Nchi haueleweki.
50.
Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2016, thamani ya uagizaji wa bidhaa
ilipungua kwa asilimia 3.9 kufikia Dola za Kimarekani milioni 4,422.4
ikilinganishwa na Dola za Kimarekani milioni 4,603.7. Hata hivyo, kupungua kwa
uagizaji wa bidhaa hakuwezi kuhusishwa moja kwa moja na wasiwasi walio nao
wafanyabiashara kwamba uchumi wa nchi haueleweki. Zipo sababu kadhaa za
kupungua kwa uagizaji ikiwemo hatua za kiutawala zilizochukuliwa na Serikali
kudhibiti mianya ya biashara ya magendo.
51. Mheshimiwa Spika, kuzibwa
kwa mianya hiyo kumesababisha upungufu wa bidhaa ambazo zilikuwa zinauzwa kwa
bei ya chini kutokana na kutokutozwa kodi stahiki. Wafanyabiashara ambao
wanasemekana kusita kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa kigezo cha kwamba
uchumi wa nchi haueleweki, baadhi yao ni wale waliokuwa wanatumia mwanya wa
kukwepa kulipa kodi ambao sasa umezibwa kwa kiasi kikubwa. Hivyo, sababu za
baadhi ya wafanyabiashara kusita kuagiza mizigo zinaweza kuwa ni pamoja na
kushindwa kuingiza bidhaa nchini bila kulipa kodi stahiki, kushindwa kulipa au
kulipwa madeni, kubadilisha aina ya biashara, kushindwa kusimamia biashara,
gharama kubwa za uendeshaji, kuibuka kwa washindani wa kibiashara wenye nguvu
au huduma bora zaidi n.k. Ni matarajio ya Serikali kwamba wafanyabiashara na watanzania kwa ujumla
watazoea mfumo huu wa kulipa kodi stahiki na hivyo kuongeza uagizaji wa bidhaa
na huduma. Serikali itaendelea kuboresha mfumo wa kodi ili uwe
rafiki zaidi kwa wafanyabiashara.
Hitimisho
52. Mheshimiwa Spika, kama
tulivyoona katika viashiria mbalimbali vya kiuchumi, uchumi wa Tanzania uko
imara na tulivu, mfumuko wa bei umedhibitiwa katika wigo wa tarakimu moja,
Benki zetu bado zina ukwasi wa kutosha kuweza kukopesha wananchi na Deni la
Taifa linaendelea kuwa himilivu. Taarifa huru ya IMF iliyotolewa tarehe
9 Januari, 2017 inathibitisha ukweli huu kwa kusema:
‘‘Tanzania’s macroeconomic performance remains strong. Economic growth
was robust during the first half of 2016 and is projected to remain at about 7
percent this fiscal year. Inflation came down below the authorities’ target of
5 percent and is expected to remain close to the target, while the external
current account deficit was revised down on account of lower imports of capital
goods.”
53.
Mheshimiwa Spika, ziko changamoto kadhaa ambazo
Serikali inaendelea kuzifanyia kazi hususan zile ambazo zipo ndani ya uwezo wa
Serikali. Ninawasihi Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kwa pamoja katika masuala
yote ya maendeleo ya nchi yetu na tutumie taarifa rasmi katika kuwafikishia
wananchi ujumbe ulio sahihi. Aidha, kama nilivyoeleza awali, napenda
kuwahakikishia waheshimiwa wabunge na watanzania kwa ujumla kwamba uchumi wetu
ni tulivu, uko imara na tunategemea utaendelea kuwa hivyo katika kipindi cha
muda wa kati. Nirudie kwa kuwahakikishia kuwa hakuna mdororo wa uchumi nchini.
54.
Mheshimiwa
Spika, naomba kuwasilisha.
0 comments :
Post a Comment