Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Katika
kukabiliana na athari za ukame, Serikali imechukua hatua za makusudi
kuhakikisha kuwa hali ya chakula na lishe ni imara nchini.
Waziri
wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba ameyasema hayo jana
Mjini, Dodoma katika Kikao cha Bunge alipokuwa akitoa kauli ya Serikali
kuhusu hali ya chakula na lishe kwa mwaka 2016/2017.
“Tathimini
imebainisha kuwa Halmashauri za wilaya 55 zinahitaji jumla ya tani
1,969 za mbegu bora za mahindi, mtama na mizizi inayokomaa kwa muda
mfupi na kustahimili ukame,” alifafanua Dkt. Tizeba.
Aliendelea
kwa kusema kuwa mbegu hizo zinahitajika ziwafikie mwezi Februari 2017
iliziweze kupandwa katika msimu wa 2016/2017 katika maeneo yanayoendelea
kupata mvua wakati huu wa mwaka.
Dkt. Tizeba alizitaja hatua ambazo Serikali inazichukua kuhakikisha kuwa hali ya chakula na lishe ni imara kuwa ni pamoja na;
Kusimamia
usambazaji wa mbegu za mazao ya kilimo zinazostahimili ukame na
zinazozaa kwa muda mfupi ambazo ni pamoja na mtama, uwele na mbegu za
mazao aina ya mizizi za mihogo na viazi vitamu ili kuzitumia vizuri mvua
zinazonyesha sasa.
Kuhamasisha
wakulima kupanda mazao aina ya mizizi, mtama na uwele kwa maeneo
yanayopata mvua za masika ambazo zinaendelea kunyesha na mawakala wa
pembejeo pamoja na vivutio vya utafiti vilivyopo katika kanda mbalimbali
hapa nchini.
Vile
vile Serikali kupitia Wakala (NFRA) inaendelea kuhifadhi kwa uangalifu
chakula kilichopo ili kitumike pale kitakapohitajika.
Hatua
nyingine ni Kuhamasisha sekta binafsi kununua mazao ya chakula katika
maeneo yaliyo na ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba wa chakula.
Aidha wafanyabiashara waliohifadhi mahindi wanaombwa kusambaza chakula
hicho katika masoko ya ndani ya nchi ili kupunguza mfumuko wa bei.
Aidha
Serikali inaendelea kuhimiza usindikaji wa mazao ya chakula kwa
kuyaongezea thamani na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhiimu wa kula
vyakula vya aina zote.
Dkt.
Tizeba amesema kuwa kutokana na hali ya mwenendo wa unyeshaji wa mvua
za vuli na msimu kutoridhisha katika maeneo mengi ya nchi, Wakuu wa
Mikoa na Wilaya wanashauriwa kuendelea kuhamasisha na kusimamia wakulima
kutuma mbegu zinazokomaa mapema na kupanda mazao yanayostahimili ukame.
Aidha
Serikali imewataka wakulima kuendelea kuzitumia mvua zinazoendelea
kunyesha kwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na kukomaa kwa muda
mfupi na pia waendelee kutunza na kutumia chakula walichonacho kwa
uangalifu.
0 comments :
Post a Comment