Wizara ya Nishati ya Kenya imepiga marufuku gesi ya kupikia kutoka Tanzania kuingia nchini humo. Tamko la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Kenya linasema ‘ ndani ya siku 7 kuanzia juzi tarehe 24 Aprili 2017, itakuwa ni marufuku Kwa Kenya kuagiza Gesi ya kupikia kutoka Tanzania ‘.
Uamuzi huu wa Kenya ni kinyume na misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Tanzania na Kenya ni wanachama. Kwa mujibu wa Itifaki ya Soko la Pamoja, bidhaa za nchi zetu zinaruhusiwa kusambaa ndani ya jumuiya bila vikwazo.
Gesi ya kupikia kuingia Kenya hutokea Tanzania Kwa sababu Tanzania ni nchi pekee katika ukanda huu ambayo imewekeza mitambo ya kupokea Gesi na kuiweka kwenye mitungi. Bandari ya Dar Es salaam na mfumo mzuri zaidi wa kupokea gesi kuliko Bandari ya Mombasa na hivyo kuifanya gesi inayotoka Tanzania kuwa na gharama nafuu nchini Kenya kuliko gesi inayoagizwa kupitia bandari ya mombasa.
Uamuzi wa kuzuia Gesi kutoka Tanzania ni uamuzi wenye kulenga kuilinda bandari ya Mombasa Kwa kuvunja mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kwa kutaka kuifanya Tanzania iendelee kuwa muuzaji wa malighafi kwenda Kenya badala ya bidhaa zilizokamili Kama gesi ya kupikia.
Uamuzi huu wa Serikali ya Kenya una lengo la kuathiri urari wa biashara kati ya Tanzania na Kenya ambapo Kwa miaka ya hivi karibuni Tanzania imekuwa ikiuza bidhaa nyingi zaidi huko Kenya kuliko inazoagiza kutoka nchi hiyo.
Ninamsihi Waziri wa Biashara na Viwanda wa Tanzania afuatilie suala hili na kuzungumza na mwenzake wa Kenya ili waondoe vikwazo Hivi vya biashara ambavyo havina maana yeyote na vinazuia raia wa kenya kupata bidhaa nafuu kutoka Tanzania. Viwanda vingi vya Kenya hutegemea malighafi kutoka Tanzania, kuzuia gesi ya kupikia na kuendelea kuagiza malighafi za kuendesha viwanda vyao ni sera ya Kenya kuifanya Tanzania kuwa chanzo cha malighafi tu na sio chanzo cha bidhaa zilizoongezwa thamani.
Serikali ya Tanzania isikubali hili na ianze mazungumzo mara moja na Serikali ya Kenya ili Watanzania wanaouza gesi ya kupikia huko Kenya waendelee kuuza na kutumia Bandari ya Dar Es Salaam. Kama Serikali ya Kenya ikiendelea na msimamo wake basi Tanzania ichukue msimamo kama huo Kwa bidhaa za Kenya Kama maziwa ambayo yamejaa kwenye soko letu.
Zitto Kabwe, Mb Kigoma mjini 26/4/2017
0 comments :
Post a Comment