Furaha tele kwa Arsene Wenger baada ya Arsenal kutwaa taji la FA huku Antonio Conte akiomboleza kipigo na kukosa taji hilo muhimu
Meneja wa Chelsea Antonio Conte amekiri kwamba Arsenal “waliishangaza” timu yake kwa mwanzo wa kasi katika mechi ya fainali Kombe la FA iliyopigwa Wembley.
Washika Mtutu waliingia kwenye mechi hiyo wakiwa hawapewi nafasi mbele ya mabingwa wapya Ligi Kuu Uingereza Chelsea, lakini iliwachukua dakika zisizozidi tano kupata goli la kuongoza kupitia Alexis Sanchez aliyefunga goli tata.
Chelsea walipunguzwa na kubaki 10 dimbani kipindi cha pili baada ya Victor Moses kuoneshwa kadi ya pili ya njano kwa kujiangusha, na licha ya kufanikiwa kusawazisha Conte anaamini Chelsea hawana cha kujitetea kwa kipigo cha 2-1 walichopata.
“Nadhani goli la kwanza lilikuwa la ajabu. Kipindi cha pili hatukuanza vizuri, hatukuwa makini na tulitaabika dakika 25 za kwanza. Tulianza kucheza vema kipindi cha pili na kadi nyekundu ikaturudisha nyuma. Sikuliona tukio vizuri kwenye runinga, ilikuwa vigumu kuelewa,” Muitaliano huyo aliwaambia waandishi.
“Goli la kwanza, mchezaji aliugusa mpira. Kuotea si jambo la msingi. Arsenal walianza vizuri na walikuwa na dhamira ya kushinda. Walitushangaza lakini narudia dakika zetu 25 za kwanza hatukuwa vizuri. Katika kipindi ambacho tulikuwa tumechangamka mwamuzi alitupa kadi nyekundu.
“Matokeo ya mwisho yanakatisha tamaa, lakini haya huwa yanatokea na presha ilikuwa kubwa. Victor Moses alikuwa katika ubora wake na amecheza kwenye msimu muhimu. Msimu wetu ulikuwa wa kupendeza kutokana na ushindi wa ligi, sasa ni vema tukatazama mbele na kuanza upya.”
Conte alikuwa akitaka kuweka rekodi sawa na Muitaliano mwenzake Carlo Ancelotti aliyetwaa mataji mawili msimu wake wa kwanza kwenye soka la Uingereza.Facebook