Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameitaka serikali
kuwachukulia hatua viongozi mbalimbali waliohusika katika kuliingizia serikali hasara ya
mabilioni kutoka kwenye sekta ya madini.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akisoma taarifa za chama
Freeman Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai Mkoani Kilimanjaro alitoa kauli hiyo
katika Mkutano Mkuu wa CHADEMA mjini Dodoma alipokuwa akizungumzia sakata la mchanga
wa madini ambalo limepamba moto kwa sasa nchini.
Tunafukuza watu kwa makosa yaliyofanywa miaka 15 iliyopita, lakini wale waliofanya makosa
wapo uraiani, wapo huru” alinukuliwa Mbowe akizungumza.
Kwa kauli hii ya Kiongozi Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni ni kuwa, baadhi ya waliokuwa
viongozi wakuu wa shughuli za serikali wakati mikataba hii ikisainiwa na kazi hizi za usafirishaji
wa mchanga ambao ni wananchama wa chama hicho, nao watachukuliwa hatua endapo serikali
itaamua kuwashughulia wote waliohusika kwa namna yoyote.

Kama serikali ingekuwa inamchukulia kila mtu hatua tangu mikataba hii iliposainiwa, basi ni
dhahiri Mawaziri Wakuu wasataafu Frederick Sumaye na Edward Lowassa ambao nao ni
wanachama wa CHADEMA, kwa namna moja au nyingine wangehusika kwani wao pia walikuwa
wasimamizi wa shughuli za serikali.
Mbali na jambo hilo lakini Mbowe alikikosoa pia Chama cha Mapinduzi kuwa kiliingia mikataba
mibovu iliyopelekea nchi kupata hasara ya mabilioni. Mbowe alisema kuwa tatizo kubwa katika
sekta ya madini ni sheria, ambazo wapinzani wamekuwa wakipiga kelele kila mara kuwa
zirekebishwe.
Aidha, Mbowe aliwataka wanachama wa chama hicho kusimama kisawasawa na asiwepo mtu
mwenye uwoga wa aina yoyote kwani wamedhamiria kushika dola mwaka 2020Facebook