Lisu Amkomalia Bashite

Wakili Tundu Lissu na wenzake wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wamelikomalia vilivyo sakata maarufu la Bashite linalohusiana na tuhuma za kughushi vyeti vya kielimu linalomkabili mmoja wa wakuu wa mikoa kwa kulifikisha kortini ili lipatiwe ufumbuzi.

Aidha, Lissu na wenzake hao wamedhamiria kuona kuwa kigogo huyo anayetuhumiwa kuliacha jina lake halisi la Daudi Albert Bashite kutokana na matokeo mabovu ya sekondari na kutumia jina la mtu mwingine, achukuliwe hatua za kisheria ikiwamo kufungwa jela kwa kosa la kughushi ikiwa itathibitika kuwa ana hatia.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Lissu ambaye ni Rais wa TLS, alisema uamuzi huo wa kulifikisha mahakamani suala la Bashite umetokana na maazimio ya baraza la uongozi la chama hicho, lengo likiwa ni kulinda utawala wa sheria na uwajibikaji nchini.

Tofauti na matarajio ya baadhi ya watu, sakata hilo la Bashite halikupatiwa jibu kutokana na ripoti ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wote wa umma iliyokabidhiwa kwa Rais John Magufuli Ijumaa kutowagusa viongozi wa kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wabunge na madiwani.

Katika kufanikisha nia hiyo ya TLS, Lissu aliyekuwa na viongozi wengine wa chama hicho wakiwamo Makamu Rais, Godwin Ngwilimi na Wakili Stephen Kuwayawaya, alisema miongoni mwa hatua walizochukua ni pamoja na TLS kufungua mashtaka binafsi ya jinai dhidi ya mkuu huyo anayedaiwa kuitwa Bashite.

Aliongeza kuwa mkuu huyo wa mkoa, anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai likiwamo hilo la kutumia vyeti feki na kwamba, kazi ya kumshtaki haitachukua miezi bali ni wiki mbili au tatu.

“Kifungu cha 128(2) cha sheria ya Mwenendo wa jinai, sura ya 20 ya sheria za Tanzania kinaruhusu mtu binafsi (pamoja na taasisi, kampuni au mashirika kama TLS) kupeleka malalamiko kwa hakimu mwenye mamlaka pale anapoamini kuna sababu za msingi zinazoonyesha kuwa kosa la jinai limetendwa,”alisema Lissu, akielezea vifungu wanavyotumia kufikisha suala hilo kortini.

Alisema dhana ya utawala wa sheria ina maana pana na kwamba, pamoja na mambo mengine, siyo tu kwamba hakuna mtu aliyeko juu ya sheria, bali pia kila mtu bila kujali cheo au nasaba na hali yake kiuchumi na jamii, yuko chini ya udhibiti wa sheria za kawaida za nchi na hivyo yuko pia chini ya mamlaka ya mahakama za kawaida.

“Kuna tuhuma za muda mrefu sasa kwamba Mkuu huyo wa mkoa ametumia vyeti vya shule ya sekondari visivyokuwa vyake. Yeye… ni Daudi (Albert) Bashite,” alisema Lissu, akiongeza kuwa jina linalotumiwa sasa na mkuu huyo linadaiwa kuwa mwenyewe yupo na ndiye mwenye vyeti halisi, na kitendo hicho ni kosa la jinai.

Akifafanua zaidi, Lissu alisema kifungu cha 120 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, kinasema “Mtu yeyote aliye kwenye utumishi wa umma ambaye, wakati akitekeleza majukumu ya ofisi yake akifanya kitendo cha udanganyifu au ukiukaji dhamana huo ungekuwa ni kosa la jinai kama ungefanywa na mtu binafsi au la, anafanya kosa na endapo atapatikana na hatia atapata adhabu ya kifungo cha miaka saba jela.”

Lissu alisema kwa kutumia vyeti vya shule visivyokuwa vyake, na kwa kutumia majina ya mtu mwingine wakati akiwa mtumishi wa umma, mkuu huyo mwenye jina halisi la Daudi Bashite ameathiri imani ya wananchi kwa serikali yao kwa kuajiri na kulinda watu wadanganyifu na wasiokuwa na vyeti halali.

“Mtu huyu amefanya kosa la jinai ambalo kwalo anastahili kushtakiwa mahakamani na endapo atapatikana na hatia anastahili kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za kawaida za nchi yetu,” alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema).

Lissu aliongeza kuwa endapo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atakataa kutoa ridhaa, TLS itamfungulia mkuu huyo wa mkoa mashtaka ya rejea ya kimahakama katika Mahakama Kuu ili alazimishwe kutoa ridhaa hiyo.

Kabla ya kumkabidhi Rais Magufuli ripoti ya uhakiki wa vyeti vya elimu na kitaluma kwa watumishi wa umma nchini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Uatawala Bora, Angela Kairuki, alisema watumishi 9,932 walikutwa na vyeti vya kughushi na kwamba, ripoti hiyo haikuwagusa viongozi wa kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge na madiuwani.

Hata hivyo, Makamu Rais wa TLS, Ngwilimi, alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha Sheria ya Utumishi wa Umma namba 3 na 5, tafsiri ya mtumishi wa umma inawahusisha pia Wakuu wa mikoa na Wakuu wa Wilaya na hivyo kina Bashite walipaswa pia kuhusishwa katika uhakiki huo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment