Michuano ya Kombe la Mabara inayoendelea nchini Urusi, imekumbwa na mshangao dimbani baada ya kuanza kutumika kwa mwamuzi msaidizi anayetumia video kuamua baadhi ya uamuzi wenye utata.
Mwamuzi huyo ambaye hukaa kwenye chumba maalumu, hutumia picha za marudio ya tukio lolote lililotokea uwanjani, na kutoa uamuzi ambao huwa ndiyo ya mwisho, lengo likiwa ni kumsaidia mwamuzi anayekuwa katikati ya dimba kufanya uamuzi wake kwa usahihi.
Katika mechi zilizopigwa jana, jumla ya matukio matatu yaliamuliwa kwa usaidizi wa picha za video ambapo matukio yote yalihusisha magoli yaliyofungwa, mawili yakionekana hayakuwa halali, huku moja likionekana halali.
Katika mchezo wa kwanza kati ya Ureno na Mexico uliomalizika kwa sare ya 2-2, Ureno ilipata bao kupitia kwa Pepe, lakini kupitia kwa usaidizi wa video, bao hilo lilikataliwa kwa kuonekana kuwa palikuwa offside.
Katika mchezo wa pili kati ya Chile na Cameroon ambao ulimalizika kwa Chile kupata ushindi wa mabao 2-0, bao la Vergas wa Chile lilikataliwa kwa kuonekana kuwa alikuwa ameotea, lakini katika dakika ya 90, Vergas tena alifunga bao jingine ambalo awali lilikataliwa lakini kwa msaada wa video, bao hilo lilionekana kuwa ni halali na kuhesabika kama bao la pili kwa Chile.
Michuano hiyo inaendelea leo kwa mechi mbili ambapo Australia inakabana koo na Ujerumani.
0 comments :
Post a Comment