Uhaba wa walimu wa shule za msingi katika halmashauri ya wilaya ya Singida, umechangia baadhi ya shule kutoa ajira za muda za walimu kwa watu wasio na utaalamu wowote wa kufundisha.
Imelezwa baadhi ya shule hizo hutoa ajira za muda kwa wahitimu wa kidato cha nne na cha sita wasiokuwa na taaluma ya ualimu, kitendo kinachochangia taaluma kushuka.
Hayo yamesemwa juzi kwenye mkutano wa wadau wa elimu katika halmashauri hiyo, ulioitishwa kwa ajili ya kujadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazozikabili shule za msingi.
Wadau hao wamesema shule za msingi zilizoanzishwa kisheria katika miaka ya hivi karibuni, ndizo zenye upungufu mkubwa zaidi wa walimu.
Mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Misuna kata ya Mgori, Elisante Issa, amesema wao wameajiri kwa muda walimu watatu ambao wanawalipa kila mmoja shilingi 50,000 kwa mwezi.
“Tunajua wazi vijana hawa ni wahitimu tu wa kidato cha nne, na hawajahudhuria chuo chochote cha walimu. Lakini sasa tunafanyaje, shule yetu ya msingi ina walimu wawili tu, na wote ni wa kiume. Mmoja akiwa nje ya shule kikazi, anabaki mmoja, huyu atahudumiaje shule yenye madarasa hadi saba,” alisema Elisante kwa masikitiko.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Sagara, Salimu Shabani, amesema shule yao ya Gairo, ina walimu watatu tu, na wote ni wa kiume wanafundisha wanafunzi 291.
“Baada ya kuelimishwa na mashirika yetu ya Action Aid na Medo, kuwa shule za msingi na hata sekondari ni mali yetu na sio za serikali, tumebadilika. Sasa tunashiriki kikamilifu kuhakikisha miundombinu ikiwemo vyumba vya madarasa na nyumba za walimu, zinakidhi mahitaji,” alisema kwa kujiamini.
Kwa hali hiyo, amesema serikali nayo inapaswa kuendelea kuwaunga mkono kwa kumalizia ujenzi wa vyumba vya madasa na vyumba za walimu kwa wakati.
Amedai kwamba kuna wakati wanamaliza kujenga maboma ya vyumba vya madarasa au nyumba za walimu, serikali inachukua muda mrefu kukamilisha, jambo linalowavunja moyo.
“Pia serikali itoe kipaumbele suala la kuzalisha walimu kwa wingi, ili sisi tuondokane huu mzingo wa kuajiri vijana wasiokuwa na taaluma ya ualimu. Kuwatumia vijana hawa waliohitimu kidato cha nne, ni kwa sababu hatuna namna ya kukabiliana na huu uhaba mkubwa wa walimu,” alisema.
Kwa upande wake kaimu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Emmanuel Sima, alisema wamejipanga vizuri kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kwa changamoto mbalimbali zinazokabili shule za msingi ni sekondari.
Alisema kutokana na ufinyu wa bajeti watatoa kipaumbele kwa shule zenye changamoto zilizo na madhara zaidi.
“Tunatenga bajeti maalumu kwa ajili ya ujenzi wa vyoo bora kwenye shule zetu na vitakuwa na chumba maalum kwa wanafunzi wa kike waliopevuka. Tunapenda bahati ya kupata mfadhili Saving and Friends kutoka Korea ambaye anatuchimbia visima virefu katika shule zetu zote. Kwa hiyo vyoo vya shule vitakuwa na maji ya kutosha,” alisema Sima ambaye ni diwani (CCM) kata ya Msisi.
Kaimu Afisa Elimu wilaya ya Singida, Hussein Shalari, amezishauri kamati za shule za msingi zinazotoa ajira za walimu za muda, kuwasiliana na ofisi ya elimu ya wilaya, ili pamoja na mambo mengine, kujua uwezo wa walimu hao wa muda.
“Endapo tutashirikiana hatua hiyo itasaidia kwa sababu ofisi yetu itaweza kuandaa mafunzo mafupi kwa waajiriwa hao, ili kuwajengea uwezo zaidi wa kufundishia”,alisema afisa huyo ambaye ni afisa taaluma katika halmashauri hiyo,” alisema Shalari.